Familia zaidi zalia watoto kupotea mikononi mwa polisi

Halima Said ambaye ni mama mzazi wa Salmin Shams akizungumza wakati wa mahojiano na mwandishi wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) jijini Dar es Salaam hivi karibuni. Kushoto ni mke wa Salmin, Mariam Dotto. Picha na Said Khamis
Muktasari:
- Wingu limetanda katika familia ya Salmin Shame (33) kijana anayedaiwa kupotea katika mazingira ya kutatanisha tangu usiku wa Desemba 24 mwaka jana.
Dar es Salaam. Wingu limetanda katika familia ya Salmin Shame (33) kijana anayedaiwa kupotea katika mazingira ya kutatanisha tangu usiku wa Desemba 24 mwaka jana.
Kijana huyu akiwa na wenzake wawili, Elisante Eneza na mwingine aliyefahamika kwa jina moja la Khamis kwa mara ya mwisho walikuwa pamoja nyumbani kwa Salmin ambaye alimuaga mzazi mwenzie wanakwenda kutembea kwa ajili ya mkesha wa Sikukuu ya Krismasi lakini tangu siku hiyo, wote watatu hawajaonekana tena, hivyo kuziacha familia zao kwenye sintofahamu.
Hili limeibuka ikiwa imepita wiki moja baada ya familia tano jijini Dar es Salaam kujitokeza kwenye vyombo vya habari kuiomba Serikali kuingilia kati suala la kupotea kwa vijana wao waliotoweka tangu Desemba 26 mwaka jana na licha ya kupata taarifa kuwa walikamatwa lakini walipotafutwa katika kwenye vituo vya polisi jijini Dar es Salaam na hawajapatikana hadi sasa.
Kuhusu tukio la Salmin na wenzake, familia yake ilieleza kuwa baada ya kufuatilia, Desemba 26 walibaini kuwa vijana hao wanashikiliwa katika Kituo cha Polisi Osterbay kwa tuhuma za kuiba simu lakini siku iliyofuta waliporejea tena kituoni hapo kwa ajili ya kuwatolea dhamana waliambiwa hawapo na hadi sasa haifahamiki waliko.
Akizungumza na Mwananchi, mke wa Salmin, Mariam Dotto alisema jioni ya Desemba 24 mumewe na rafiki zake wawili walikuwa nyumbani kwake wakicheza na mtoto wao wa miezi tisa na baadaye wakamuaga kuwa wanakwenda matembezini.
“Waliondoka wakisema wanakwenda
kutembea mkesha wa Krismasi, mume wangu ni mtu wa kupenda starehe hivyo sikuona shida, lakini hakurudi siku hiyo jambo ambalo si kawaida nikabaki na maswali lakini kwa kuwa ni vijana nikasema nisionyeshe wivu niwaache tu. Krismasi ikapita, Disemba 26 akaja Zuhura ambaye ni mwanamke wa Elisante kuniuliza kama nimemwona mwanaume wake, nikamwambia hata wangu hajarudi hapo ndipo tukaanza kuhisi kuna hatari kwa kuwa si kawaida yao, tukakubaliana twende polisi lakini mwenzangu akanihurumia hadi nimuandae mtoto hivyo akaniambia ngoja aende yeye,” alisema Mariam.
Kituo cha kwanza alichokwenda Zuhura alisema ni Osterybay kwa kuwa wiki chache zilizopita mumewe huyo alikamatwa kwa kosa la uzururaji hivyo akaona bora aanzie huko inawezekana wamekutwa na kosa hilo tena.
Alipofika pale kituoni, alisema askari aliyemkuta alikiri kuwakamata vijana hao watatu akiwaelezea kutokana muonekano wao, majina na hata eneo walilotokea kuwa wamekamatwa kwa kosa la wizi wa simu.
“Yule askari akamuuliza ndiyo umekuja kuwachukulia dhamana, wameiba simu ngoja nikupe namba ya waliyemuibia uwasiliane naye ikiwezekana myamalize wenyewe. Alitoa namba yule mwenzangu akarudi nyumbani kuja kunijuza na tukawasiliana na huyo anayedaiwa kuibiwa simu akasema jambo hilo ameliacha polisi. Niliwasiliana na ndugu wa mume wangu kuhusu dhamana na wakatambua inahitajika fedha wakasema tumuache kwanza ajifunze maana wiki chache zilizopita alitolewa polisi, nikamjuza yule mwenzangu kuhusu hilo hivyo yeye akaanza hatua za kumchukulia dhamana mume wake,” alisema.
Desemba 27, alisema Zuhura alirudi tena Kituo cha Polisi Oysterbay kwa mara ya pili kwa ajili ya kukamilisha taratibu za dhamana ila cha ajabu akakutana na jibu liliwaacha vinywa wazi hadi sasa.
“Tuliambiwa hawapo. Tukabaki tunajiuliza hawapo vipi wakati jana yule askari alisema wamekamatwa na wapo hapa basi majibu yakawa hayo, mara hawajawahi kuwepo pale ikabidi tuanze kutafuta kwenye vituo vingine vya polisi lakini kote hawakuonekana,” alisema.
Kuanzia hapa, anasema waliona suala hilo linazidi kuwa zito hivyo akamtaafiru mama mkwe wame ambaye alisema waanze kuangalia kwenye hospitali kama wamepata ajali au kwenye vyumba vya kuhifadhia maiti lakini hawakufanikiwa kuuona mwili wa mpendwa wao huko kote.
Baada ya kupata taarifa hizo, mama mzazi wa Elisante, Tina Abraham aishiye mkoani Kilimanjaro alifunga safari hadi jijini Dar es Salaam kuja kufuatilia kwa kina na kupata uhakika zaidi ili kurahisisha kuweka mikakati ya kumsaka mwanaye.
Kwanza, alisema alikwenda Kituo cha Polisi Oysterbay kujua hatima ya mtoto wake lakini kama ilivyokuwa kwa waliotangulia, hakupewa majibu yaliyomridhisha.
“Nililazimika kufanya fujo siku hiyo pale kituoni ndipo nilipokutanishwa na mpelelezi na hatimaye nikaambiwa kweli watoto wetu walikuwa pale na walikamatwa kwa uzururaji ila kuna siku waliruhusiwa watuhumiwa wengine na wao wakatoroka. Nikawauliza inawezekana vipi watuhumiwa watoroke kituoni tena kwenye kituo kikubwa kama kile,” alisema.
Baada ya hapo, Tina alisema “nikaomba kuonana na OCD nikazungumza naye wakasikiliza maelezo yangu lakini bado sikupata majibu yanayoeleweka binafsi nataka tukutanishwe na Mkuu wa Jeshi la Polisi Simon Sirro atuambie watoto wetu wako wapi.”
Mama Salmin alia
Halima Said, mama mzazi wa Salmin anaiomba Serikali kuingilia kati suala hilo ili waweze kutambua hatima ya watoto wao ambao mpaka sasa wanaamini wamepotea wakiwa mikononi mwa polisi.
“Hatuwezi kuwa tumekaa wazazi tunaangalia watoto wanapotea kirahisirahisi namna hii, tunaomba Serikali iingilie kati na sheria ifuate mkondo wake kama hawa watu walikamatwa sheria inaweka wazi walitakiwa kufikishwa mahakamani ndani ya saa 24 sasa tangu Disemba 24 hadi sasa ni zaidi ya mwezi, tunataka kufahamu wako nao au kama wamekufa tumshukuru Mungu kuliko hivi tunakaa roho juu,” alisema mama huyo akibubujikwa machozi.
Kauli ya Jeshi la Polisi
Baada ya kusikia malalamiko ya familia hizo Mwananchi lilimtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Ramadhan Kingai ili kuzungumzia undani wa madai hayo lakini alijibu kwa kifupi kuwa taarifa zote za kipolisi za mkoa zinawasilishwa kwa Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Murilo.
Alipopatikana Kamanda Murilo alionyesha kutolifahamu suala hilo ila akaahidi kulifuatilia ili kutoa taarifa za uhakika.
“Kiukweli unachoniambia sikifahamu ila nashauri waende wakamuone RPC halafu mimi nitafuatilia kutokea kwake...ila unaweza kuwaelekeza waje ofisini kwangu niwasikilize niweze kuelewa vizuri hilo suala lao kwa hatua zaidi,” alisema Muliro.
Familia ya Salmin ilienda ofisini kwa Kamanda Murilo ambaye aliwasikiliza na kuelekeza mtu wa chini yake kuchukua maelezo yao kwa ajili ya kuyafanyia kazi ya kumtafuta mtoto huyo pamoja na marafiki zake wawili.