Familia, Serikali wamzungumzia Askofu Sendoro

Mjane wa marehemu Askofu Chediel Sendoro (katikati aliyevaa nguo nyeusi) akifarijiwa na baadhi ya waombolezaji waliofika nyumbani kwake leo Septemba 11, 2024. Picha na Omben Daniel
Muktasari:
Mwili wa Askofu Sendoro utatolewa katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini KCMC siku ya Jumatatu Septemba 16, 2024 na kupelekwa katika Kanisa Kuu Mwanga ambapo saa nne asubuhi taratibu za kutoa heshima za mwisho zitaanza na kuzikwa Jumanne septemba 17, mwaka huu.
Florah Temba
Mwanga. Familia ya Askofu Chediel Sendoro imeeleza namna ndugu yao alivyoishi kwa upendo katika familia na jamii na kwamba hakuwahi kuinua mabega licha ya kwamba alikuwa ni askofu.
Askofu Sendoro alifariki dunia Septemba 9, 2024 kwa ajali ya gari iliyotokea katika eneo la Kisangiro, Wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro saa 1:30 usiku baada ya gari alilokuwa akiendesha, aina ya Toyota Prado, akitokea Kileo kuelekea nyumbani Mwanga, kugongana uso kwa uso na lori.
Historia inaonyesha kuwa Askofu Sendoro ndiye askofu wa kwanza wa Dayosisi ya Mwanga ambaye aliingizwa kazini Jumapili ya Novemba 6, 2016 baada ya kuzaliwa kwa dayosisi hiyo mpya iliyotokana na kugawanywa kwa dayosisi mama ya Pare.
Akimzungumzia askofu huyo, leo Septemba 12, 2024 msemaji wa familia ambaye ni kaka wa marehemu, Jeremiah Sendoro amesema Askofu Sendoro alikuwa mtu wa kanisa, familia na jamii na katika maisha yake alimuweka Mungu mbele katika kila jambo.
Amesema watamkumbuka katika mambo mengi lakini kubwa ni upendo na ushirikiano wake kwa familia na jamii yote iliyomzunguka.
“Tumepokea msiba huu kwa mshtuko na masikitiko makubwa kibinadamu, mioyo imeumia, tumeumia lakini maneno ya Mungu yanatuambia tushukuru kwa kila jambo maana ndiyo mapenzi ya Mungu na sisi tumelipokea, hivyo tunamshukuru Mungu kwa hilo kwa sababu hatuwezi kubadili chochote.
“Askofu Sendoro alikuwa ni mtu wa Kanisa, mtu wa familia na mtu wa jamii, alimuweka sana Mungu mbele katika kila jambo na mkikutana kabla hamjazungumza mtafanya sala kwanza ili mambo mengine yaendelee,” amesema Jeremiah.
Amesema katika shughuli za familia alishiriki kama mwanafamilia na hakuwahi kuinua mabega kuonyesha kwamba yeye ni askofu.
“Kwenye familia alishiriki kama mwanafamilia, hakuinua mabega kwamba yeye ni askofu pamoja na kwamba alikuwa ni mdogo kwetu lakini alikuwa anashiriki na kuchangia kila jambo tulilokubaliana kwenye familia kwa usawa uleule tuliokubaliana nao,” amesema.
Ameongeza: “Akiwa na wazo tofauti, alieleza kwa heshima na kwa staha, kwa hiyo kwenye familia alikuwa ni mtu wa familia na kwenye jamii alikuwa ni mtu wa jamii kwa maana ya kwamba kila anapokwenda anaangalia changamoto zilizopo na kutafuta utatuzi wake.”
Ameeleza kuwa, pia, ameweza kuwasaidia wasichana 37 wanaotoka jamii ya wafugaji Wamasai kupata ufadhili wa kusoma shule ya sekondari na kwamba lengo lake lilikuwa ni kuhakikisha wanasoma na kuendelea na maisha yao.
“Pia ameangalia ujenzi wa shule za ufundi na vitu vingi, aliangalia jamii inataka nini na kuona mchango wake ni upi katika kuhakikisha jamii inasonga mbele, hakika hatutamsahau kwa upendo na ushirikiano wake mkubwa kwa familia na jamii,” amesema.
Ameeleza kuwa yeye na ndugu yake walikuwa wakizungumza kila siku na mara ya mwisho walijadiliana kuhusu watoto wao kuona namna ya kuwaongoza ili wampende Mungu na kuwa na bidii ili kufanikiwa katika maisha.
“Mimi na mdogo wangu tulizungumza kila siku na mara ya mwisho tulikuwa tunaangalia watoto wetu wamekuwa wakubwa sasa, hivyo tulijadili namna ya malezi yao na kuwaongoza ili waweze kwenda katika kumpenda na kumjua Mungu, lakini pia kuwa na bidii ili waweze kufanikiwa katika maisha,” ameeleza.
Ratiba ya maziko
Akizungumzia ratiba, Jeremiah amesema mwili wa marehemu utatolewa katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini (KCMC) Jumatatu Septemba 16, 2024 na saa 4 asubuhi, utapelekwa katika Kanisa Kuu la Mwanga kwa ajili ya heshima za mwisho zitakazoanza siku hiyo.
Amesema heshima za mwisho zitaendelea mpaka Jumanne Septemba 17, 2024, saa 3 asubuhi na saa 4 kamili asubuhi, ratiba rasmi ya maziko itaanza.
Alishirikiana na Serikali
Akimzungumzia Askofu Sendoro, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu amesema enzi za uhai wake alikuwa na ushirikiano mkubwa na Serikali na siku zote alipenda kuona mambo yanasonga mbele.
“Serikali ya Mkoa tumepokea kwa masikitiko kifo hiki kwa sababu alikuwa ni mtu mwema na alikuwa na ushirikiano sana na Serikali, alikiwa na upendo mkubwa na hata pale Mwanga pamoja na kwamba yeye alikuwa kiongozi mkubwa kwenye ile dayosisi lakini alikuwa anatoka anakwenda hadi ofisi za serikali katika kuhakikisha mambo yanakwenda.
“Natoa pole nyingi kwa Askofu Dk Alex Malasusa (Mkuu KKKT), familia na wanamwanga wote, tutaendelea kuenzi jinsi alivyokuwa anashirikiana nasi katika shughuli za Serikali, tupo pamoja na familia katika kipindi hiki cha maombolezo,” amesema.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mangondi, Hendry Chaki amesema walishirikiana kwa karibu na Askofu Sendoro katika shughuli za kijamii na alipambana kuhakikisha watoto wa shule wanapata chakula cha mchana shuleni.
“Tuna majonzi, tumepotelewa na baba yetu, hatutamsahau hasa katika kupeleka chakula kwa wanafunzi, alitupenda na alitoa misaada mbalimbali, alikuwa ni lulu kwetu.”
Amesema: “Alikuwa ni mtu wa maendeleo na alihudhuria vikao mbalimbali vya kiserikali, alijitoa sana na katika kitongoji hiki alishauri tuwe na mpango wa chakula cha kutosha kila kaya na alikuwa amenieleza kuwa atanisaidia kuleta mtu wa kutoa elimu kwa jamii ili waweze kuwa na chakula cha kutosha.”