Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Fadina anavyoendesha maisha bila kuwa na viganja

Fadina Mussa akiwa katika eneo lake la biashara

Katika toleo la lililopita la  tuliona kuvunjika ndoa ya Fadina na Mtepa na uamuzi wa Mahakama wa kugawana mali ulivyotolewa na hatimaye mwanamke huyo akakatwa viganja na mtalaka wake. Nini kiliendelea? Fuatilia makala haya kujua kilichojiri.

Mtwara. Fadina alikaa hospitalini takribani siku 19 kabla ya kuruhusiwa kutoka na kuanza maisha mapya akiwa hana viganja.

Mfumo wa maisha yake ya kila siku ulibadilika kutoka mwanamke wa kuchakarika hadi tegemezi anayehitaji msaada wa kila kitu.

Si hayo tu, kukosa mikono kunamfanya ashindwe kufanya shughuli za kumuingizia kipato, huku akiwa na watoto wawili wanaosoma.

Anapoyatafakari hayo, Fadina humlilia Mungu ampe mwongozo wa kuishi katika hali hiyo ya ulemavu.

“Nilipoteza mwelekeo na kukata tamaa ya maisha, lakini nashukuru madaktari na watoa huduma pale hospitali walinipa maneno ya kunitia moyo na kunifariji.

“Niliporuhusiwa nilikwenda nyumbani kwetu kijijini Lyenje, watu wa kwetu waliponiona na hali ile waliumizwa mno, wengine waliokuwa wanakuja kuniona walishindwa kuficha hisia zao na kumwaga machozi. Ukiachana na hao, napata simu za wengine wasionifahamu wakinifariji na kunitaka nimuachie Mungu,” anasema Fadina.

Anasema baada ya muda mfupi alikwenda Mtwara mjini kwa matibabu zaidi, huko aliungana na watoto wake wanne waliochukua jukumu la kumhudumia.


Zawadi anavyomhudumia

Zawadi Mkavilima (20) ni mtoto wa nne wa Fadina aliyebeba jukumu la kumhudumia mama yake. Alianza kazi hiyo akiwa mwanafunzi wa kidato cha tano.

Binti huyu aliyehitimu kidato cha sita akisubiri kujiunga na elimu ya juu, ndiye anayemuangalia mama yake kwa ukaribu.

Alikuwa karibu na mama yake tangu alipopata fahamu akiwa hospitali baada ya kujeruhiwa na Mtepa.

“Naumia kufanya ninayoyafanya lakini siwezi kumuacha mama yangu ahudumiwe na mtu mwingine mimi nikiwapo. Nilipata maumivu makali niliposikia mama amepatwa na kadhia hii, tulikuwa Mtwara ila tulifahamu anakwenda kukutana na baba kwa ajili ya mgawo wa mali.

“Taarifa kwamba hakuna kilichogawiwa zaidi ya mama kushambuliwa ilinifanya nilie kupita kiasi. Nilipofika hospitali sikuamini nilichokiona, mama yangu alikuwa ameharibika mno usoni na hana viganja,” anasema.

Tofauti na dada yake mkubwa, Zawadi anaeleza alionekana jasiri, hivyo madaktari walishauri akae na mgonjwa wodini kumhudumia.

“Bahati tukio lilitokea siku ambayo shule zinafungwa, hivyo likizo yote niliitumia kumuuguza mama kuanzia hospitali hadi tuliporejea kijijini Lyenje na tukaenda Mtwara kwa matibabu zaidi.

“Dada mkubwa anaishi Masasi, hivyo kwa wanawake mimi ndiye nilikuwa mkubwa sikuwa na namna ya kukwepa jukumu la kumhudumia mama,” anaeleza.

Anasema shule zilipofunguliwa, aliamka alfajiri kumhudumia mama yake kabla ya kwenda shuleni, hivyo alichelewa vipindi vya mwanzoni.

Anasema, “Nilikuwa naamka alfajiri nachemsha maji, namuogesha, namvalisha na wakati mwingine namfunga kitenge kwa kutumia kamba ili kisidondoke. Nahakikisha nimeandaa chakula kisha naondoka namuacha na kaka yangu.”

Anasema walimu walielewa changamoto aliyokuwa akipitia, hivyo hata alipochelewa hakuadhibiwa.


Matokeo mabaya shuleni

“Nilikuwa najitahidi nikifika darasani namuomba rafiki yangu anifundishe walichofundishwa vipindi vya awali,” anasema.

Anasema mambo yaliendelea hivyo hadi alipofanya vibaya mtihani wa nusu muhula kidato cha sita, ndipo walimu walipomuita mzazi wake na kumwambia kuna haja ya binti huyo kukaa shuleni ili kupata muda wa kujiandaa vizuri na mitihani yake ya mwisho.

Hii ilikuwa habari mbaya kwa Zawadi. Anasema licha ya kupenda elimu, alifikiria akikaa shuleni maisha ya mama yake yatakuwaje?

“Nani atampatia huduma muhimu kama kumwogesha na mambo mengine yote yanayohusu mwili wake. Haikuwa rahisi kukubali lakini sikuwa na jinsi nililazimika kukaa bweni,” anasema.

Hata hivyo, anasema mama yake alikuwa akimtembelea shuleni kwa kuwa ilikuwa jirani na nyumbani kwao.

“Kuna wakati mama alikuwa anakuja kunitembelea nikimuona hayupo vizuri namwambia aingie kwenye bafu la matroni namwogesha anarudi nyumbani akiwa msafi. Hakuna kitu nimekikataa kama kumuona mama yangu akiwa mchafu au akihudumiwa na mtu baki.

“Sisi ndiyo tunamfahamu mama yetu, ni mchapakazi si mtu wa kufanyiwa kazi ndiyo maana nilikuwa naumia kuona imefika wakati anashindwa hata kujihudumia. Nimechukua jukumu hilo na nitafanya hadi pale Mungu atakapotuletea njia nyingine,” anasema.

Zawadi aliyehitimu kidato cha sita katika shule ya Amanah Islamic Seminary iliyopo Mtwara, akisoma masomo ya sanaa, mchepuo wa HKL (History, Kiswahili, Language) na kupata daraja la pili, ndiye anayeishi na mama yake wilayani Tandahimba.

Pamoja na kazi za nyumbani za kupika, kufua na usafi, Zawadi kila asubuhi ana jukumu la kumwogesha mama yake, kumvalisha, kumkuna anapohisi kuwashwa na kuhakikisha anamsaidia kwa kila alilo na uwezo nalo.

Hayo yakiendelea, kuna uwezekano muda wowote akaenda kujiunga na masomo ya chuo kikuu. Zawadi anasema amechagua kusoma Mtwara ili awe karibu na mama yake

“Kabla hili halijatokea ndoto yangu ilikuwa kusoma katika mojawapo ya vyuo vikuu vilivyopo Dar es Salaam au Morogoro lakini mawazo hayo yamebadilika nahitaji kuwa karibu na mama, ndiyo maana nimeomba vyuo vya Mtwara. Hii itanirahisishia kuwa karibu naye pale itakapotokea dharura kwa kuwa hali yake kiafya bado si nzuri,” anasema.


Uhakika wa kusoma

Hata hivyo, Zawadi hana uhakika wa kuendelea na masomo endapo hatapata mkopo. Anasema familia yake haina uwezo wa kumudu gharama za kumsomesha elimu ya juu.

Analeza, “kumaliza kwangu kidato cha sita haikuwa rahisi. Mama alipita huku na kule kuomba msaada, akajitokeza mtu mmoja kupitia shirika lake akanilipia ada ya mwaka mzima. Sasa natakiwa kwenda chuo lazima nijiandae, maandalizi yanahitaji fedha hivyo niwaombe Watanzania wenzangu wanisaidie.

“Sitamani kuendelea kuomba misaada maisha yangu yote, ndiyo sababu natamani nisome niweze kumudu kumsaidia mama na familia yangu kwa ujumla. Elimu ndiyo njia pekee itakayonisaidia kufanikisha lengo hili. Hii inanifanya kila siku nimuombe Mungu awezeshe safari yangu ya kupata elimu iwe nyepesi.”

Kilio cha elimu kwa familia hii si kwa Zawadi pekee. Mdogo wake Zainab aliye kidato cha kwanza naye anamtegemea mama yake.

Licha ya kusoma shule ya Serikali ana mahitaji kadhaa yanayomuwia vigumu kuyapata kutokana na hali ya mama yake.

Fadina anasema anapata maumivu mtoto wake anapohitaji kitu cha shule na akakikosa kwa sababu ya kutokuwa na fedha.

“Kwa mfano, huyu Zainab wa kidato cha kwanza shuleni kwao wanatakiwa wapate fulana na inauzwa Sh15,000 lakini hadi sasa bado hajapata, kuna siku nilimsikia akijisemea haya yote ni kwa sababu mama yangu hana mikono isingekuwa hivyo ningeshapata. Kauli ile ilinifanya machozi yanidondoke na kumuuliza Mungu kwa nini aliruhusu hili, ni kweli wanangu wanaelewa hali niliyonayo lakini haibadilishi ukweli kwamba bado ni watoto,” anasema Fadina.


Maisha bila viganja

Ni katika maumivu hayo, mwaka mmoja na miezi minane sasa vidonda vimepona na makovu yamekauka Fadina anapambana kuhakikisha anafanya baadhi ya shughuli mwenyewe.

Usemi kwamba, ‘Mungu akikupa kilema anakupa na mwendo’ unajidhihirisha kwake. Licha ya ulemavu anajitahidi kutumia sehemu ya mikono iliyobaki kufanya vitu vidogo vidogo.

Anajitahidi kufunga kitenge, inawezekana kisikaze vizuri lakini angalau anaweza kukishika na kukizungusha mwilini na kukibana kwapani.

Hivi sasa anamudu kula mwenyewe tofauti na awali alihitaji kulishwa. Anasema vingi anavyofanya ni matokeo ya kuikubali hali aliyonayo na kuamua kuishi kulingana na alivyo.

“Nilivyotoka hospitali kichwa kilipata moto, nikiwaza nitawezaje kuishi katika hali hii, kila kitu nilikuwa nafanyiwa. Nimeendelea kuishi hivyo kwa muda nikajiuliza itakuwa hivi hadi lini, itakuwaje kama watoto hawapo na nilikuwa naumia kuona mtoto anaacha kula, ananilisha.

“Tena afadhali Zawadi ana ujasiri, mtoto wangu wa kiume aliyekuwa na jukumu la kunipa chakula ana moyo mwepesi, alikuwa akinilisha vijiko viwili anaanza kulia. Zawadi alikuwa anahangaika kunilisha chakula chake kinapoa, mwisho wa siku hali. Nikaona nina kila sababu ya kukubaliana na hali niliyonayo, nianze kujifunza kufanya vitu mwenyewe kwa kutumia viungo vyangu vilivyobaki kwa sasa naweza kula,” anasema.

Wakati wa kula anachohitaji Fadina ni kuandaliwa chakula, kinawekwa juu ya kidoga mbele yake na anakula taratibu bila msaada wa mtu yeyote.

Nikiwa nyumbani kwa Fadina nilishuhudia akila mwenyewe. Kazi ya Zawadi ni kupika na kuhakikisha chakula kinakuwa na kiwango cha joto ambacho hakiwezi kumuunguza.

Baada ya kutenga chakula, Zawadi anamnawisha mikono akimwagia maji. Fadina huitakasa kwa kuisugua kama ambavyo angefanya kwenye viganja na kuanza kula.

Kama ni ugali, utakatwa matonge naye atakula. Unaweza kujiuliza inakuwaje anapokula wali, jibu ni kwamba, kwa kutumia sehemu ya mikono yake iliyobaki anamudu vyema kuweka chakula mdomoni.

Iwe ni nyama au samaki ili mradi imepikwa ikaiva vizuri, Fadina anakula akishika kwa umakini kwa kutumia sehemu hiyo hiyo ya mikono iliyobaki.

Vivyo hivyo katika mlo wa asubuhi, kinachofanyika ni chai kupozwa kwa kiwango kinachomfaa, naye hunywa akishushia vitafunwa vilivyoandaliwa iwe ni viazi, maandazi, chapati au hata vitumbua anashika na kula mwenyewe.

Fadina pia hula matunda kama vile embe, papai na chungwa, ambalo huweza kulikamua vyema kinywani mwake akafyonza majimaji yake. Mbali na hayo, sasa anaweza kusafisha kinywa chake.

“Naendelea kujizoeza kufanya vitu mbalimbali. Mswaki hivi sasa napiga mwenyewe, anachofanya Zawadi ni kuniwekea dawa kwenye mswaki na maji, basi nasafisha kinywa changu. Namshukuru Mungu angalau kuna vitu naendelea kuvifanya.

“Kuna wakati najiuliza, haya wanayonifanyia watu ingekuwa ni mimi ningeweza? Sipati majibu maana kuna muda nashikwa haja naendaje chooni mwanangu hayupo? Nafikiria kumfuata jirani ila ndiyo hivyo kibinadamu inaniuma maana si jambo rahisi na wao wana majukumu yao katika familia zao. Kwa kweli namuomba Mungu azidi kunipa maarifa,” anaeleza.

Licha ya anayofanya kuleta tumaini kwa Zawadi, binti huyu anaumizwa na jitihada hizo za mama yake kukabiliana na ulemavu wake akizieleza kuwa ni mateso.

Anasema kwa anavyomfahamu mama yake na aina ya maisha aliyozoea kuishi awali, ni wazi anapitia kipindi kigumu katika jitihada za kujikwamua na hali hiyo.

“Namfahamu vyema mama yangu, si mtu wa kupenda kufanyiwa kitu. Vitu vyake hufanya mwenyewe ndiyo maana hata sisi ametulea katika misingi ya kupenda kufanya kazi. Inapofikia hatua ni lazima apate msaada wa mtu mwingine naelewa ni kiasi gani anaumia.

“Hii ndiyo sababu kila siku anapambana kujaribu kufanya vitu kulingana na hali yake, ukimwambia umlishe hataki anachotaka umwekee chakula ahangaike nacho. Kuna siku nimerudi nimekuta katoa nguo anataka kufua nikamwambia hapana.

“Unaweza kukuta anapambana kunyanyua ndoo ya maji ya lita 10, kwa kifupi anajaribu kwa kila hali kuishi maisha yake ya uchakarikaji.”

Si hayo tu Fadina ni mzungumzaji mzuri kwenye simu, kama hauko jirani na ukampigia simu unaweza usihisi kuwa ana changomoto yoyote.

Ili azungumze kwa simu ni lazima kuwapo mtu jirani atakayemsaidia kupokea na kukata atakapomaliza mazungumzo.


Kauli za majirani

Jukumu la kumhudumia Fadina kwa kiasi kikubwa linafanywa na Zawadi na ikitokea hayupo, husaidiwa na Kuruthum Chindema ambaye ni jirani yake.

“Kwangu sioni ni jukumu kubwa kwa sababu yapo mengi tunafanya kwa ushirikiano, huyu ameshakuwa kama mama yangu na tunaishi vizuri ndiyo maana si kitu cha ajabu kumsaidia katika changamoto anazopotia.

“Mama huyu anahitaji msaada, sasa binti yake yupo hata sisi majirani tupo lakini kuna wakati anahitaji kufanya vitu vyake kama binadamu wengine. Nikiwaza hayo naumia sijui kwa nini alifanyiwa ukatili wa namna hii,” anasema Kuruthum.

Jirani mwingine, Shani Mbage anayefahamiana na Fadina kwa miaka mingi, anamwelezea kuwa ni mchapakazi aliyejulikana zaidi kwa ujasiriamali na kilimo.

Anasema kukatwa viganja si tu ukatili, bali kumerudisha nyuma jitihada za kujikwamua kiuchumi.

“Nimehamia Tandahimba miaka 14 iliyopita, namfahamu mama huyu ni miongoni mwa wanawake wachakarikaji kwenye kilimo na biashara ndogo ndogo, sielewi hata kwa nini mume wake aliona kumkata viganja ndiyo adhabu anayostahili. Kwa kutumia mikono yake alikuwa analima na kubangua korosho anapata chochote kwa ajili ya wanawe,” anasema.

“Masuala haya ya ukatili dhidi ya wanawake huku kwetu yapo, na pale unapojaribu kupambana au kwenda kushtaki ndiyo haya unaambulia vipigo, kufukuzwa na kila aina ya mateso kama aliyopitia mwenzetu. Mama huyu anateseka na hata majirani tunamsaidia bado msaada wetu hauwezi kuwa wa kukidhi mahitaji yake,” anasema Shani.


Fadina na ujasiriamali

Mazoea yana taabu. Usemi huu unaakisi maisha ya Fadina ambaye bado hamu yake ni kufanya biashara ndogo ndogo ipo juu.

Anaeleza ujasiriamali si jambo aliloanza ukubwani, bali tangu akiwa mtoto alijishughulisha kupata fedha zilizomsaidia hadi akahitimu elimu ya msingi.

“Nilipenda kusoma lakini elimu haikuwa kipaumbele cha wazazi wangu, hivyo nilifanya kazi ili kupata mahitaji muhimu  ya kujisomesha. Nililima baadaye nikaingia kwenye biashara ya nyanya.

“Nilikuwa naenda bondeni kijiji cha jirani na wasichana wenzangu tunachukua nyanya na kuziuza kijijini kwetu. Fedha nilizopata kwenye biashara ziliniwezesha kulipa ada na kununua mahitaji ya shule. Nilifanya hivyo hadi nikamaliza elimu ya msingi, sikupata bahati ya kuendelea na masomo nikaolewa,” anasema.

Anaeleza magumu aliyopitia katika maisha ya utotoni na usichana wake yalimfanya apambane kwa hali na mali kuhakikisha watoto wake hawapitii hayo kwa kuwapa elimu katika mfumo sahihi.

Katika kufanikisha hilo, anasema aliwekeza nguvu kubwa kwenye kilimo na biashara ndogo ndogo.

Mikono ndiyo ilikuwa nyenzo yake, hata hivyo kwa hali aliyo nayo sasa anasema bado anaweza kujaribu tena biashara.

Kupitia mikopo inayotolewa na halmashauri kwa wenye ulemavu alipata fedha za kuanzisha biashara.

Uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tandahimba ulimshika mkono kama anavyoeleza; “Nashukuru baada ya kuhangaika huku na kule, mwanzoni mwa mwaka huu nikapata mkopo wa wenye ulemavu Sh2 milioni. Fedha hizi nilichukua kwa ajili ya biashara.”

Anasema kwa hali yake aliumiza kichwa ni biashara gani atafanya ili arejeshe mkopo.

“Kwa bahati kuna kaka ambaye sina undugu naye lakini tumeishi vizuri kwa muda mrefu anaitwa Hassan Liyanga, nilienda kumuomba ushauri akanishauri nianzishe biashara ya kuuza vyombo vya nyumbani. Hakuishia kunishauri akanisaidia kupata eneo jirani kabisa na eneo lake la biashara na kwa kiasi kikubwa ananisaidia katika uendeshaji,” anasema Fadina.

Mwandishi wa gazeti hili alifika eneo hilo la biashara lililopo mwendo wa dakika 20 kutoka nyumbani kwa Fadina na kukutana na Liyanga akiendelea na biashara katika vibanda viwili, chake na cha Fadina.

Liyanga anasema Fadina ni sawa na dada yake waliyefahamiana kwa muda mrefu lakini ukaribu wao umeimarika baada ya kupatwa na tatizo hilo.

“Tulikuwa tunafahamiana ila hatukuwa tumeshibana kama ilivyo sasa, alivyopatwa na tatizo lile nilikwenda hospitali kumjulia hali, bahati mbaya nilikuta hana fahamu. “Alipoamka aliambiwa nimekwenda kumjulia hali, kuanzia hapo udugu wetu ukaimarika maradufu tukawa tunazungumza vitu vingi,” anasema na kuongeza;

“Alivyokuwa kwenye mchakato wa kufuatilia mkopo alinieleza nikamshauri kuhusu biashara ya vyombo vya plastiki, nikiamini atakaa tu kwa sababu yupo jirani ningemsaidia kwa kiasi kikubwa kuifanya. Lengo ni aweze kuingiza senti mbili, tatu maisha yaendelee.”

Anasema alimshauri asikodi eneo la biashara bali watafute kibanda atakachokiweka jirani na eneo lake bila malipo yoyote.

Liyanga anasema baada ya kibanda kupatikana alikwenda Mtwara mjini kufungasha mzigo wa vyombo ndipo walipoanzisha biashara hiyo.

Licha ya biashara hiyo kutokuwa na muda mrefu tangu ianzishwe wengi hununua bidhaa ili kumuunga mkono Fadina.

Tofauti na matarajio ya Liyanga kwamba Fadina angekaa dukani kuuza bidhaa, mama huyo amejiongeza kwa kutembeza bidhaa barabarani ili kuongeza kipato.

Anawezaje kupokea fedha na kurudisha chenji pale inapohitajika kufanyika hivyo, ni swali nililomuuliza Fadina.

Huku akitabasamu anajibu, “Eeeh! mimi mjanja siibiwi. Nimekatwa viganja siyo macho wala akili, kwanza ninavyotoka nahakikisha nimepachika kipochi changu cha kuning’inia. Mteja anapokuja namsoma kwa haraka kuona nimuamini au nimtilie shaka, kama nitamuamini nitamwelekeze atumbukize kwenye mkoba na hata akihitaji chenji nitakuwa makini kuhakikisha anachukua anayostahili.     

                       

Alivyopata mkopo

Ofisa Maendelo ya Jamii wa Wilaya ya Tandahimba, Aloyce Masau anasema ofisi yake iliguswa na kumweka Fadina miongoni mwa wanufaika wa mikopo ya halmashauri katika kundi la wenye ulemavu baada ya kuona anakidhi vigezo.

“Kabla hajakatwa mikono Fadina alikuwa mjasiriamali na hata changamoto ilivyotokea akasema bado anahitaji kuendelea na ujasiriamali. Kama halmashauri tulimsaidia kwa namna mbalimbali, kubwa ni kuhakikisha anapata mkopo afanye kile anachotamani.

Masau anasema bado hajaanza kurejesha lakini yupo ndani ya muda na halmashauri inatambua changamoto anazopitia.

Itaendelea kesho

Imeandikwa kwa kushirikiana na Bill & Melinda Gates