Elimu ya watu wazima yatumbua majipu

Muktasari:
Wakuu wa vituo washindwa kuisimamia inavyotakiwa
Dar es Salaam. Sera ya elimu bure imeibua jipya baada ya wazazi waliotakiwa kulipa ada kwenye vituo vya Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima wakidhani watoto wao wamechaguliwa kujiunga na shule za sekondari za Serikali, kugundua kuwa walidanganywa.
Wanafunzi hao waliohitimu darasa la saba mwaka jana na kushindwa kufikisha wastani wa ufaulu unaoanzia alama za ufaulu 100 - 250, walianza masomo baada kuchaguliwa kujiunga na vituo vya taasisi hiyo kinyume cha sheria.
Ada walizotakiwa kulipa wanafunzi hao ni kati ya Sh80,000 hadi Sh200,000 kwa mwaka kulingana na kituo kilipo.
Akizungumza na waandishi wa habari, Kamishna wa Elimu wa Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Eustella Bhalalusesa alisema wazazi na walezi wa wanafunzi hao walishtuka walipotakiwa kulipa ada wakati wakijua Serikali iliagiza elimu iwe bure.
Kutokana na ulaghai huo, kamishna huyo alimuagiza Mkurugenzi wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima, Dk Fidelis Mafumiko kuwavua madaraka wakufunzi wakazi wa mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma, Mwanza na Geita kwa kukiuka taratibu za kuwachagua wanafunzi hao.
Waliovuliwa madaraka ni Kamishna Mkazi wa Mkoa wa Dar es Salaam, Wotugu Muganda, Kamishna Mkazi wa Mkoa wa Dodoma, Senorina Kateure na Kamishna mkazi aliyekuwa akisimamia mikoa ya Mwanza na Geita, Steward Ndandu.
Profesa Bhalalusesa alisema utaratibu unawataka wanafunzi wanaotaka kujiunga na vituo vya taasisi hiyo kuchagua kwa hiari yao kama ilivyo kwa shule nyingine zisizo za umma.
Alisema kilichotokea ni kwamba, wakufunzi hao kwa kushirikiana na ofisi za halmashauri waliwatangazia wanafunzi ambao hawakufikisha wastani wa ufaulu kuwa wamechaguliwa kujiunga na vituo vya taasisi hiyo kama chaguo la pili kinyume na sheria.
Profesa Bhalalusesa alisema utaratibu huo umesababisha mkanganyiko kwa wazazi na walezi ambao wamekuwa wakiamini watoto wao wamechaguliwa kujiunga na elimu ya sekondari katika shule za umma, hivyo kuwa na matumaini ya kuhusika na utaratibu wa elimu bure. “Huu ni ukiukwaji wa sheria uliofanywa kwa makusudi na wakufunzi hawa kwa sababu walitakiwa kutangaza nafasi ili watakaotaka kujiunga wafanye hivyo kwa hiari,” alisema.
Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Dk Mafumiko alisema vituo vingi vya wanafunzi wa taasisi hiyo viko kwenye shule za sekondari za kata.
“Wazazi walipojulishwa watoto wao wamechaguliwa kujiunga na Kituo cha Pugu Sekondari wakajua walifaulu na hiyo ni shule ya Serikali, hapo ndipo ulipoanza mkanganyiko,” alisema.