Dk Ndumbaro atoa maagizo ujenzi Kituo Jumuishi cha Sheria

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Muktasari:

Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Damas Ndumbaro amemwagiza Mkandarasi Suma JKT kuhakikisha utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa Kituo Jumuishi cha Taasisi za Kisheria za Serikali mkoani Mwanza unakamilika ifikapo Oktoba, 23 mwaka huu.

Mwanza. Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Damas Ndumbaro amemwagiza Mkandarasi Suma JKT kuhakikisha utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa Kituo Jumuishi cha Taasisi za Kisheria za Serikali mkoani Mwanza unakamilika ifikapo Oktoba, 23 mwaka huu.

Akizungumza jijini Mwanza wakati wa ziara ya wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria waliotembelea mradi huo, Dk Ndumbaro amemtaka mkandarasi kuongeza kasi baada ya kupata taarifa utekelezaji wa mradi umefikia asilimia 45 badala ya asilimia 55.

“Tuliwapa kazi hii (Suma JKT) tukifahamu mnao uwezo wa kufanya kazi kwa Saa 24; hatutegemei ucheleweshaji wa aina yoyote kwa sababu hatutoongeza muda. Hakikisheni mnakamilisha mradi huu ifikapo Oktoba 23, mwaka huu kwa mujibu wa mkataba ili wananchi waanze kupata huduma,” amesema Dk Ndumbaro

Kituo Jumuishi cha Taasisi za Kisheria za Serikali mkoani Mwanza kinachojengwa eneo la Buswelu Manispaa ya Ilemela kitakuwa na ofisi za taasisi nne ikiwemo Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Ofisi ya Taifa ya Mashitaka (DPP), Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita).

Ujenzi wa jengo hilo la ghorofa nne lililobuniwa, kusanifiwa na kusimamiwa na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) utakaogharimu zaidi ya Sh3.1 bilioni ulianza Aprili 29, 2022 una unatakiwa kukamilika ndani ya miezi 18.

Mbunge wa Singida Kaskazini, Ramadhan Ighondo ameunga mkono agizo la Serikali kwa kumtaka mkandarasi kuongeza nguvu kazi na muda wa kufanya kazi kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati.

“Mnapopata changamoto ya malipo aiambieni Serikali ili mradi usikwame. Msitegemee kuongezwa muda kwa sababu gharama zitaongezeka,” amesema Ighondo

Mbunge wa Viti Maalum, Khadija Kaaya ‘Keisha’ ameitaka Serikali kutafuta suluhisho la tatizo la utekelezaji wa miradi kuchelewa kwa sababu zile zile zinazojirudia kutoka mradi mmoja hadi mwingine.

Hoja ya kutafutwa dawa ya kukomesha ucheleweshaji wa miradi imeungwa mkono na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Utawala Bora, Katiba na Sheria, Florent Kyombo akisema ucheleweshaji huo unakwamisha juhudi za Serikali za kuwaletea maendeleo wananchi.

Akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo, Kapteni Ferdinand Sira kutoka Suma JKT amesema mradi huo umechelewa kuanza kwa muda wa miezi miwili kutokana na eneo la mradi kubainika kuwa na miamba mikubwa chini ya ardhi iliyobidi itolewe kabla ya kaunza ujenzi.

“Tutaongeza idadi ya mafundi, vibarua na muda wa kufanya kazi kufidia ile miezi miwili iliyopotea; lengo ni kukamilisha mradi kwa wakati,” amesema Kapteni Sira