Dk Nchimbi awaonya viongozi wabinafsi CCM

Muktasari:
- Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk Emmanuel Nchimbi amesema siku zinahesabiska kwa viongozi wa chama hicho ambao hawatimizi wajibu wao.
Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Emmanuel Nchimbi amesema viongozi wa chama hicho wanaotanguliza maslahi binafsi, siku zao zinahesabika.
Dk Nchimbi amesema viongozi wanatarajiwa kuwa watumishi wa wananchi waliowachagua wakiweka maslahi ya umma na Watanzania mbele wakati wote kabla ya masuala yao binafsi.
Nchimbi ametoa kauli hiyo leo Februari 20, 2024 wakati akitoa salamu za rambirambi za CCM kwenye shughuli ya kutoa heshima za mwisho kwa hayati, Balozi mstaafu, Dk Deodorus Kamala kijijini kwao Rwamashonga, kata ya Bwanjai, wilaya ya Misenyi, mkoani Kagera.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kitengo cha Habari, Ofisi ya Katibu Mkuu Katibu huyo, amesema uwezo wa uongozi aliokuwa nao hayati Kamala ni pamoja na saikolojia ya kutafuta suluhisho la changamoto za watu.
Amesema tangu Balozi Kamala akiwa rais wa wanafunzi katika Chuo Kikuu cha Mzumbe, alikuwa muadilifu na kwamba alichukia rushwa kwa vitendo.
“Alikuwa tayari kupoteza ubunge wa jimbo la Nkenge katika Uchaguzi Mkuu 2010 kwa sababu hakuwa tayari kupokea fedha kuwasaliti wananchi wa jimbo hilo aliokuwa anawatetea kwenye changamoto zao.
“Kamala hakuwa mla rushwa, hata alipopoteza ubunge hakuwahi kulalamika kwa sababu alijua zile zilikuwa ni hela za udhalimu, hela za usaliti kwa wananchi wake, watu wa namna hii lazima tuwaenzi vizuri kwa kutambua mchango wao mkubwa,” amesema.

Katibu mkuu wa CCM, Dk Emmanuel Nchimbi akiweka udongo kwenye kaburi la Dk Deodorus Kamala aliyezikwa kijijini kwao Rwamashonga, kata ya Bwanjai, wilaya ya Misenyi, mkoani Kagera.
Dk Nchimbi amesema viongozi na vijana wa sasa wana mengi ya kujifunza kwa Dk Kamala, hasa jinsi ya kutimiza wajibu kwa kuwatumikia wananchi kwa kuweka maslahi ya nchi mbele.
Amesema kwa wale viongozi wachache wanaotanguliza maslahi yao binafsi mbele na wasiotimiza wajibu wao, siku zao zinahesabika.
Dk Kamala, ambaye aliyewahi kuwa mbunge wa Nkenge kwa nyakati tofauti, aliwahi pia kuwa Naibu Waziri wa Afrika Mashariki na Waziri wa Afrika Mashariki.
Pia, aliwahi kuhudumu kama Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji, Luxembourg na Jumuiya ya Ulaya, mjini Brussels.
Kiongozi huyo alifariki dunia Februari 12, 2024 na amezikwa leo Jumanne, Februari 20, 2024, kijijini kwake, Rwamashonga, Bwanjai.