Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Dk Nchimbi atua Mtwara, kutembelea kaburi la Mkapa

Katibu Mkuu wa CCM, Dk Emmanuel Nchimbi amewasili Wilaya ya Masasi mkoani Mtwara kuanza ziara ya siku nne katika mikoa ya Mtwara na Lindi.

Muktasari:

  • Hii ni ziara ya kwanza ya Dk Emmanuel Nchimbi katika mikoa ya Mtwara na Lindi tangu alipoteuliwa kushika nafasi ya Katibu Mkuu wa CCM, Januari 15, 2024, akichukua nafasi ya Daniel Chongolo aliyejiuzulu.

Masasi. Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Emmanuel Nchimbi amewasili Wilaya ya Masasi mkoani Mtwara kuanza ziara ya siku nne katika mikoa ya Mtwara na Lindi.

Dk Nchimbi amewasili katika uwanja wa ndege wa Masasi leo Jumapili Julai 28, 2024 na kupokelewa na viongozi wa CCM Mkoa wa Mtwara pamoja na mamia ya makada wa chama hicho.

Wengine waliompokea mtendaji huyo mkuu wa chama ni pamoja na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalumu), George Mkuchika, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Patrick Sawala na kamati za siasa mkoani humo.

Lengo la ziara hiyo ni kukagua uhai wa chama, kusikiliza kero za wananchi na kuzungumza na wanachama na viongozi wa CCM katika maeneo atakayotembelea.

Akiwa Masasi, Dk Nchimbi atakwenda kuzulu kaburi la Rais wa awamu ya tatu, hayati Benjamin Mkapa aliyefariki dunia Julai 24, 2020, jijini Dar es Salaam na kuzikwa Julai 29 katika Kijiji cha Lupaso wilayani hapa.

Baadaye, kiongozi huyo wa chama, atafanya mkutano wa ndani na viongozi wa CCM Wilaya ya Masasi na Mkoa wa Mtwara kabla ya kuelekea Mtwara mjini.

Akiwa Mtwara Mjini, Dk Nchimbi atafanya mkutano wa hadhara ambapo anatarajiwa kuzungumza na wananchi na kusikiliza kero zao.

Akiwasalimia wanaCCM waliofika uwanja wa ndege kumpokea, Dk Nchimbi amesema wana wajibu wa kuhakikisha Watanzania wanapata viongozi bora wanaotokana na chama hicho.

"Tukumbushane kwamba wanaCCM tuna wajibu wa kuwapatia wananchi viongozi wazuri na tunategemea tukiwapa heshima hiyo, watalinda heshima ya nchi yetu na chama chetu," amesema Dk Nchimbi.

Hii ni ziara ya kwanza ya Dk Nchimbi katika mikoa ya Mtwara na Lindi tangu alipoteuliwa na Halmashauri Kuu ya CCM chini ya Uenyekiti wa Rais Samia Suluhu Hassan kushika nafasi hiyo Januari 15, 2024, akichukua nafasi ya Daniel Chongolo aliyejiuzulu.


Endelea kufuatilia mitandao ya Mwananchi kwa taarifa zaidi.