Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Dk Mwigulu ataka suluhu ya mafuriko Kilosa


Muktasari:

  • Dk Mwigulu amewataka Tanroads badala ya kuweka utaratibu wa kuondoa mchanga kila mwaka, sasa wanapaswa kuja na mpango utakaokuwa suluhu ya kudumu ya changamoto hiyo.

Dar es Salaam/Morogoro. Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba amewaagiza watendaji wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), kujifungia ili kutafuta suluhu ya kudumu itakayowezesha watumiaji wa Daraja la Mkundi linalounganisha mikoa ya Morogoro na Dodoma kupita kwa ufanisi wakati wote.

Kwa mujibu wa Dk Mwigulu, changamoto iliyopo katika daraja hilo lililopo barabara kuu ya Morogoro Dodoma ni kujaa mchanga unaosababisha muda mwingine eneo hilo kujaa maji na kukata mawasiliano baina ya pande mbili za mikoa hiyo miwili.

Ametoa agizo hilo leo Mei 8, 2026 wakati wa ukaguzi wa Mto Mkundi lililopo Dumila wilayani Kilosa mkoani Morogoro wakati wa ziara ya kikazi mkoani humo.

Dk Mwigulu amesema badala ya Tanroads kuweka utaratibu wa kuondoa mchanga kila mwaka, sasa wanapaswa kuja na mpango utakaokuwa suluhu ya kudumu ya changamoto hiyo.

Mbali na hilo, mchanga huo umekuwa ukisababisha maji kujaa na kwenda kuhatarisha mazao na makazi ya wananchi wa maeneo mbalimbali ya Dumila.

“Mheshimiwa Waziri (Profesa Palamagamba Kabudi), bahati nzuri unahusika na uratibu na mbunge hapa, wafungie hawa mahali watafute jawabu la kudumu. Hii ni barabara kubwa haiunganishi tu mikoa ya Tanzania bali nchi na nchi, si kila siku tulale roho mkononi kwamba Dumila pakoje, haya mambo gani.”

“Ongea na wenzako, haya mambo ya kuja na chepe kila siku, haya mambo ya kizamani,” amesema Dk Mwigulu.

Waziri Mkuu, Mwigulu Nchemba akizungumza baada ya  ukaguzi wa daraja la Magole lililopo Dumila katika Mto Mkundi wilayani Kilosa



Eneo hilo limekuwa likikumbwa na mafuriko mara kwa mara kutokana na kujaa kwa maji katika mto huo wakati wa mvua kubwa, jambo ambalo huathiri usafiri kati ya Dar es Salaam na mikoa ya kati pamoja na kaskazini mwa Tanzania.

Moja ya matukio makubwa yaliyowahi kutokea ni Januari mwaka 2014 ambapo mafuriko makubwa yaliharibu Daraja la Mkundi na kusababisha kusimama kwa huduma za usafiri katika barabara kuu ya Morogoro Dodoma.

Serikali ililazimika kufanya ukarabati wa dharura ili kurejesha mawasiliano baada ya magari mengi na wasafiri kukwama.

Katika hatua nyingine, Dk Mwigulu amesema mchanga ukijaa katika eneo hilo unahatarisha usalama wa Daraja la Mkundi, lakini wanaochukua mchanga huo wanawatoza fedha, akihoji kwanini wasiwaruhusiwe kuendelea na shughuli ya kuondoa mchanga huo.

Kwa mujibu wa Tanroads, bajeti ya kuondoa mchanga katika eneo hilo baada ya kujaa inagharimu takribani Sh400 milioni kwa kutumia mkandarasi na huwa inafanyika mara mbili kwa mwaka ili kunusuru miundombinu ya Daraja la Mkundi.

Kutokana na hilo, Dk Mwigulu ameagiza viongozi wa Halmashauri ya Kilosa kuwakatia eneo wananchi ili kuvuna mchanga huo, akisema hatua hiyo itapunguzia Serikali gharama za kuchukua matrekta kwa ajili ya kuuondoa.

Amemwagiza Profesa Kabudi kuitisha kikao cha wadau kitakachojadili na kuweka mipaka itakayowezesha wananchi kuondoa mchanga haraka na eneo jingine walipange kwa ajili ya biashara ya madini hayo.

“Meneja wa Tanroads, mkurugenzi na mkuu wa mkoa, hili jambo sitaki kusikia kelele watu wanataka mchanga na sisi hatuna bajeti ya kuondoa, waelekezeni watoe ili uondoke. Nitarudi tena, malizeni hili, Jumatatu waanze kuchimba mchanga,” amesema Dk Mwigulu.

Waziri Mkuu, Mwigulu Nchemba akizungumza baada ya  ukaguzi wa daraja la Magole lililopo Dumila katika Mto Mkundi wilayani Kilosa

Awali Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima amesema utaratibu uliowekwa na Tanroads ni kuondoa mchanga kila mwaka ili kulinusuru daraja hilo, akisema maji yanayotoka milimani yanafika kwa wingi katika eneo hilo na kupita juu ya daraja.

“Mheshimiwa Waziri Mkuu, siku moja yatasomba hili daraja na kukata mawasiliano baina yetu na Tanzania yote kuanzia Dumila kuendelea mbele. Kila mwaka tunahakikisha tunaondoa mchanga wote chini ya daraja ili kupata kina kirefu cha kupitisha maji,” amesema Malima.


Historia ya mafuriko

Historia ya mafuriko ya Mto Magole wilayani Kilosa mkoani Morogoro imeendelea kubaki alama ya hofu kwa wasafiri na wakazi wa eneo hilo kutokana na athari kubwa zinazojitokeza kila msimu wa mvua, zikiwamo kuharibika kwa miundombinu ya barabara na madaraja katika barabara kuu ya Morogoro Dodoma.

Mto huo umekuwa ukifurika mara kwa mara kutokana na ongezeko kubwa la maji pamoja na kujaa mchanga ndani ya mkondo wake, hali inayopunguza uwezo wa maji kupita kwa urahisi na kusababisha mafuriko makubwa yanayoathiri usafiri na shughuli za kiuchumi.

Tukio kubwa lililobaki kwenye kumbukumbu za wengi ni la mwaka 2014, baada ya mafuriko makubwa kuharibu vibaya Daraja la Mkundi lililopo eneo la Magole na kusababisha mawasiliano ya barabara kati ya Dar es Salaam, Morogoro na Dodoma kukatika kwa muda.

Kutokana na hali hiyo, mamia ya wasafiri walikwama njiani huku magari makubwa, mabasi na malori yakishindwa kupita katika barabara hiyo muhimu inayounganisha mikoa ya kati na Dar es Salaam.

Mbali na mvua kubwa, wadau wa usafiri na wakazi wa eneo hilo wamekuwa wakieleza kuwa kuongezeka kwa mchanga ndani ya Mto Magole ni miongoni mwa sababu zinazochochea mafuriko hayo kwa kupunguza kina cha mto na kuzuia maji kupita kwa kasi inayotakiwa.

Hali hiyo husababisha maji kuongezeka kwa haraka wakati wa mvua kubwa na kuathiri kingo za daraja, makaravati pamoja na barabara kuu, jambo linaloendelea kuweka hatarini mawasiliano ya usafiri katika eneo hilo kila msimu wa mvua unapowadia.