Dk Kimei azungumzia benki ilivyojifunza kupitia mitandao ya simu

Mkurugenzi Mtendaji Benki ya CRDB, Charles Kimei.
Muktasari:
Mkurugenzi mkuu wa benki ya CRDB Charles Kimei amesema mitandao ya simu ndiyo iliyozionyesha benki kuwa zinaweza kufanya biashara na wateja wadogo licha ya changamoto zilizopo, hivi sasa benki nyingi zimeanzisha huduma mahususi kwa ajili kundi hilo.
Dar es Salaam. Mkurugenzi Mtendaji Benki ya CRDB, Charles Kimei amesema mitandao ya simu kupitia huduma zake za miamala ya fedha zilifungua macho benki kuanza kufanya kazi na wateja wadogo zaidi.
Kemei ametoa kauli hiyo jana Septemba 27, 2018 wakati benki hiyo ikizindua shindano la bahati nasibu kwa ajili ya wateja wake wanaotumia simu akaunti.
Katika shindano hilo zitakuwa zikichezeshwa droo kila saa, siku, wiki na mwezi kwa kipindi cha miezi minne kuanzia jana.
“Kampuni za simu zinazotoa huduma za kifedha zilituonyesha inawezekana kufanya biashara na watu wenye kipato kidogo sana jambo ambalo katika huduma za kawaida za benki lilikuwa haliwezekani,” amesema Kimei.
“Benki hazikuwahi kujua kama wateja hao wanaweza kupatiwa huduma na kutozwa japo kidogo, unaweza ukawatoza hata Sh1 kwa muamala wakishakuwa wengi na kufanya miamala ya mara kwa mara inalipa ndiyo maana tukaanzisha simu akaunti.”
Kimei amesema teknolojia ya habari na mawasiliano imewapatia fursa ya kuwafikia watu wengi zaidi kulingana na mahitaji yao na kwa urahisi tofauti na awali ambapo ulihitajika uwekezaji mkubwa.
Kuhusu simu akaunti Kimei amesema huduma hiyo ambayo mpaka sasa ina watumiaji 240,000 inaratibiwa na kampuni ya CRBD Microfinance Company iliyoko chini ya Benki ya CRDB, lengo ni kurahisisha zaidi huduma kwa wateja wadogo.
“Mtumiaji wa simu akaunti anaweza kupata huduma za msingi kama kufungua akaunti kwa kutumia simu, kuweka akiba,” amesema.
“Kulipia huduma na mikopo kulingana na vigezo na masharti na kwa akaunti ambayo itakuwa imefunguliwa kwa kutumia kitambulisho cha Taifa matumizi yake yatakuwa ya muda mrefu.”
Amesema zawadi zitakazokuwa zikitolewa katika shindano hilo nasibu fedha tasilimu Sh5,000 kwa mshindi wa droo ya saa, Sh20,000 kwa droo ya asubuhi na jioni, Sh2 milioni kwa droo ya wiki, Sh10 milioni kwa droo ya mwezi na Sh20milioni kwa droo ya jumla.