Dk Kahangwa: Vyama viweke kitengo kushughulikia rushwa

Muktasari:
Dk Kahangwa pia ameitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), kuongeza mapambano dhidi ya rushwa, kwani yanayojitokeza hayapaswi kufumbiwa macho.
Dar ea Salaam. Mhadhiri wa elimu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk George Kahangwa ameshauri vyama vya siasa kuweka vitengo vya maalum vya kashughulia vitendo vya rushwa inayotajwa kukithiri ndani ya vyama hivyo.
Dk Kahangwa ametoa kauli hiyo leo Jumatano Novemba 30, 2022 alipokuwa akichangia mjadala wa nini kifanyike kukithiri kwa vitendo vya rushwa kwenye chaguzi za vyama vya siasa ulioandaliwa na kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL).
Hivi karibuni katibu mkuu wa CCM, Daniel Chongolo ametangaza kufutwa kwa matokeo ya chaguzi za ndani za chama hicho tawala akisema sababu kubwa ni vitendo vya rushwa vilivyotajwa katika maeneo mbalimbali yaliyofanya mchakato huo.
"Ni wakati mwafaka kwa vyaka vya siasa kurejea utaratibu wa ndani kujua wapi wanakosea ili kukabiliana na vitendo hivi, lazima kuwepo na vitengo vya kushughulikia na kukemea rushwa maana madhara yake ni makubwa," amesema Dk Kahangwa.
Mbali na hilo, Dk Kahangwa amesema ni wakati pia kutumia mijadala mbalimbali ikiwemo Twitter Space kuhimiza viongozi wa serikali kuchukua hatua dhidi ya vitendo vya rushwa nchini.
Mbali na hilo, Dk Kahangwa ameitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), kushughulikia vitendo vya rushwa, akisema mambo yanayojitokeza hayapaswi kufumbiwa macho.
Mdau mwingine aliyechangia katika mjadala huo, Richard Kanje, amewataka Watanzania kubadilika na wasikubalia kumchagua viongozi anayetoa rushwa.
"Tanzania tubadili fikra ya kuachana na vitendo vya rushwa, tumpinge kiongozi mtoa rushwa tumpige chini," amesema Kanje