Dk Gwajima awavaa wanaomshukia

Muktasari:
- Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Dorothy Gwajima ametetea kauli na msimamo wake wa awali kuhusu njia za kukabiliana na Uviko-19, huku akiwavaa wanaomkosoa.
Musoma/Dar. Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Dorothy Gwajima ametetea kauli na msimamo wake wa awali kuhusu njia za kukabiliana na Uviko-19, huku akiwavaa wanaomkosoa.
Dk Gwajima aliteuliwa kushika wadhifa huo mwishoni mwa mwaka 2020 akimrithi Ummy Mwalimu, (sasa waziri Tamisemi) kipindi ambacho ugonjwa huo ulikuwa unaingia katika wimbi la pili.
Katika kipindi hicho, Dk Gwajima alikuwa anasisitiza zaidi wananchi kujikinga kwa kutumia njia za asili ikiwa pamoja na kujifukiza na kutumia dawa za miti, huku mwenyewe akionyesha mfano wa kujifukiza na kunywa dawa hizo hadhaani.
Hata hivyo, baada ya kuingia kwa Rais Samia Suluhu Hassan kufuatia kifo cha Rais John Magufuli, Dk Gwajima ameweka pembeni njia hizo na kusisitiza msimamo mpya wa Serikali kwenye utoaji wa chanjo, huku akitetea uamuzi wake wa awali.
Akifafanua suala hilo jana mjini Musoma, Mara, Dk Gwajima alisema hajutii kutumia dawa za asili kama ambavyo alionekana siku za nyuma akifanya, kama njia mojwapo ya kujikinga na ugonjwa huo, hatua ambayo imekuwa ikikosolewa na kudaiwa kuwapotisha wananchi.

“Kwa nini hamsemi kuwa Hayati (Magufuli) aliitaka Wizara ya Afya kujiridhisha kwanza kabla ya kuruhusu chanjo hizo?
“Yaani ninyi mnasema tu kwamba alisema chanjo ni mbaya, wakati alisema hivyo na kutoa angalizo kwamba kabla hazijaruhusiwa lazima wataalamu wetu wajiridhishe na ubora wake na ndiyo kazi iliyofanyika kabla ya Serikali ya awamu ya sita haijaruhusu chanjo,” alisema Dk Gwajima.
Gwajima aliendelea kuwavaa wanaomkosoa kwa maswali: “Hivi mbona mnanisema tu mimi? Kwani nilikuwa najifukiza na kutumia dawa za asili mimi mwenyewe? Kwani nyie hamkujifukiza? Wangapi mlikuwa mkitembea na dawa za bupiji, covidal na nyingine nyingi za asili?”
“Mbona ninyi hamjisemi, maana sote tulitumia na kutembea nazo kwenye mikoba. Mimi wala sijutii ,maana dawa zile zile zimethibitishwa na maabara ya tiba za asili nchini,” alisisitiza.
Alisema aliamua kutumia njia hizo za asili kutokana na ukweli kuwa tiba za asili zimethibitshwa na mamlaka husika.
Gwajima aliwataka Watanzania kutopotosha maelekezo aliyoyataoa aliyekuwa Rais wa awamu ya tano, hayati Magufuli.
Alisema wakati janga la corona linaingia nchini Machi 16, 2016, hakukuwa na namna ambayo watu wangeweza kujikinga na ugonjwa huo kutokana na ukweli kuwa chanjo hazikuwepo duniani.
Msimamo mpya
Katika msimamo wake mpya, Waziri Gwajima alisema baada ya wanasayansi kufanya utafiti na kuja na chanjo, hakuna haja ya kubishana nao isipokuwa watu wanatakiwa kuchanjwa ili kuondokana na athari za ugonjwa huo kwa kuwa hakuna mtu wa kushindana na sayansi.
Pamoja na kauli hiyo, wachambuzi wamesema msimamo waliokuwa nao awali viongozi dhidi ya ugonjwa huo umechangia kwa kiasi kikubwa watu kudharau hatua za kisayansi.
Mwanaharakati wa masuala ya kisiasa na kijamii, Bubelwa Kaiza alisema, “ugonjwa ulipoingia kwa mara ya kwanza haukuonekana kama tatizo, viongozi wakasimama kuhamasisha watu kutumia njia za asili za kujikinga pamoja na maombi na ikaonekana kusaidia, wananchi wamesimama hapo, ni vigumu kuwabadilisha.
“Wamekuwa wagumu kwa sababu wanahisi kuchanganywa kwa kuwa viongozi walewale waliokuwa wanawaambia corona inaisha kwa nyungu leo wanawaam waache, sasa hawajui washike lipi waache lipi,” alisema.
Agosti 10, Kiongoni wa ACT- Wazalendo, Zitto Kabwe alikosoa kauli za viongozi wa Serikali kuhusu ugonjwa huo akiwataka mawaziri wa afya kujiuzulu.
“Niweke bayana kuwa ni lazima kuwepo na mkakati maalumu wa uhamasishaji dhidi ya corona utakaongozwa na watu wanaoaminika kwenye jamii, sio watu walewale waliotuambia Tanzania imeishinda corona. Au watu walewale waliotuaminisha kuwa kunywa malimau na tangawizi ni kutibu corona,” alisema Zitto wakati akihutubia kwenye ufunguzi wa kikao cha Kamati Kuu ya chama hicho mjini Unguja.
Hata hivyo, mhadhiri na mchambuzi wa masuala ya siasa, Dk Faraja Kristomus alisema si ajabu kwa misimamo ya mawaziri kubadilika baada ya kuingia utawala mpya.
“Siyo jambo la ajabu kwa mawaziri wa JPM kuwa na msimamo tofauti kipindi hiki cha Samia kwa sababu dhana ya uwajibikaji wa pamoja ndani ya Serikali inaongozwa zaidi na sera na falsafa za kiongozi mkuu wa nchi.
“Sasa hivi falsafa ya Rais Samia inawafanya nao kuwa na mtazamo unaoendana na falsafa ya Rais aliyeko madarakani,” alisema Kristomus alipozungumza na Mwananchi Agosti 10.
Mjadala huo umeibuka siku mbili baada ya taarifa ya Wizara ya Afya ya Agosti 15 kuonyesha kuwa hadi Agosti 14 kulikuwa na Watanzania 207,391 waliojitokeza kwa hiari kupatiwa chanjo ya ugonjwa huo tangu shughuli hiyo ilipoanza Agosti 3, mwaka huu.
Takwimu hizo zilizotolewa na katibu mkuu wa wizara hiyo, Profesa Abel Makubi, zinaonyesha kuwa kati ya waliochanjwa, wanaume ni 121,002 sawa na asilimia 58.3 na wanawake ni 86,389 sawa na asilimia 41.7. Hii ni baada ya Serikali kusambaza dozi 1,008,400 za chanjo hiyo.
Mara ina wagonjwa 34
Akitoa taarifa ya hali ya afya mkoani Mara jana, wakati wa ziara ya Dk Gwajima, Mganga mkuu wa mkoa huo, Dk Juma Mfanga alisema mkoa huo ulikuwa na jumla ya wagonjwa 34 hadi jana.
Alisema kati ya wagonjwa hao saba wapo kwenye mitungi ya gesi ya oksijeni huku akisema taarifa zinaonyesha maambukizi yamepungua mkoani Mara, ingawa hakutoa takwimu.
Alisema tangu kuanza kwa chanjo ya ugonjwa wa Uviko-19 mkoani humo Agosti 5, watu 4,856 wamejitokeza na kupata chanjo hiyo na kwamba mkoa unajitahidi kuhakikisha kila anayetaka kuchanjwa anapata huduma hiyo kwa ukaribu zaidi na vituo vya kutolea huduma hiyo vimeongezwa kutoka 22 vya awali hadi 34.
Mara una mitungi ya gesi ya oksijeni 62 huku ukitarajia kupokea msaada wa mingine 200 kutoka kwa mdau ambaye hakumtaja jina.
Imeandikwa na Beldina Nyakeke, Elizabeth Edward na Bakari Kiango.