Dk Biteko: Uchaguzi serikali za mitaa usitugawe Watanzania

Muktasari:
- Wakati Tanzania ikitarajiwa kufanya uchaguzi wa serikali za mitaa baadaye mwaka huu, Naibu Waziri Mkuu, Dk Doto Biteko ametaka uchaguzi huo usiwagawe Watanzania.
Dar es Salaam. Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko amesema uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika baadaye mwaka huu, usiwe kigezo cha kuwagawa wananchi.
Badala yake ametaka wananchi waungane, wapendane na wathaminiane ili kuendelea kudumisha amani iliyopo.
Ametoa kauli hiyo leo Januari Mosi, 2024 alipojumuika na baadhi ya wananchi wa Wilaya ya Bukombe katika sherehe za kuukaribisha mwaka 2024 zilizofanyika nyumbani kwake kitongoji cha Bulangwa mkoani Geita.
Amesema mwaka huu utakuwa na uchaguzi wa serikali za mitaa, hivyo ni vyema usitumike kugawa wananchi kupitia misingi ya vyama vya siasa, badala yake uwaunganishe.
"Watu wote tunapaswa tupendane, tuthaminiane na tushirikiane, tunazo tofauti nyingi ikiwemo za makabila, dini na vyama vya siasa, lakini kamwe visitugawanye, tuungane wote na tushikamane," amesema Dk Biteko.
Kila baada ya miaka mitano, Tanzania hufanya uchaguzi wa serikali za mitaa ambapo vyama vya siasa huchuana kuwania nafasi za wenyeviti wa mitaa na vitongoji.
Akizungumzia hotuba ya Rais Samia Suluhu Hassan aliyoitoa jana Desemba 31, 2023 iliyogusa pia sekta ya nishati, Dk Biteko amesema ataiishi kauli ya Rais kuwa mwaka 2024 ni wa vitendo na si maneno.
"Tutatafanyia kazi maelekezo yake kwa nguvu zote na ubunifu ili wananchi wapate huduma bora," amesema Dk Biteko.
Alipokuwa akitoa salamu za kufunga mwaka 2023, Rais Samia alisema Februari mwaka huu mtambo wa kwanza wa kuzalisha umeme katika mradi wa Bwawa la Umeme la Julius Nyerere, utawashwa rasmi na mwingine utawashwa mwezi unaofuata.
Mitambo hiyo miwili itazalisha megawati 470 na itasaidia kufidia upungufu wa sasa. Uwashwaji wa mitambo hiyo miwili utakwenda sambamba na kuwasha mtambo wa Rusumo utakaoongeza megawati 27.
‘Ni imani yangu na Serikali kwa ujumla kuwa, hatua hizi zitaleta ufumbuzi wa kudumu kwa suala la mgao wa umeme nchini. Serikali inaendelea kuwekeza kwenye vyanzo vingine vya umeme kama vile gesi, jua, na upepo, ili kuongeza uhakika wa umeme,” alisema Samia.
Sherehe za kukaribisha mwaka 2024 wilayani Bukombe zimehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigella, wabunge , madiwani na viongozi wa vijiji.