Dk Biteko ataka Watanzania waige Wachaga

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Dotto Biteko akiwa na Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia ambaye ni Mbunge wa Rombo, Profesa Adolf Mkenda kwenye mazoezi baada ya kumalizika kwa mbio za Rombo marathon zilizofanyika katika uwanja wa mpira wa Rongai, uliopo wilayani Rombo. Picha na Janeth Joseph
Muktasari:
- Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Dotto Biteko amesema utaratibu wa Wachaga kurejea kwao sikukuu za mwisho wa mwaka ni jambo la kujivunia na kuigwa na makabila yote nchini.
Rombo. Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Dotto Biteko amesema utaratibu wa Wachaga kurejea kwao sikukuu za mwisho wa mwaka ni jambo la kujivunia na kuigwa na makabila yote nchini.
Amesema utaratibu huo ni mzuri kwa kuwa wanaporudi nyumbani wanakutana ndugu jamaa na marafiki na kujadili mambo mbalimbali, kuangalia ni wapi waboreshe na kuona upungufu katika familia zao na kuzifanyia kazi.
Dk Biteko ameyasema hayo jana Desemba 23 wakati wa mbio za Rombo Marathon zilizofanyika katika uwanja wa mpira wa Rongai, uliopo wilayani hapo, zikiwa na lengo la kuchangia fedha kwa ajili ya ujenzi wa matundu ya vyoo kwa shule za msingi na sekondari pamoja na upanuzi wa hospitali ya Huruma ili iwe hospitali ya rufaa ya wilaya hiyo.
"Utamaduni wenu watu wa Rombo wa kuja nyumbani wakati wa mwisho wa mwaka ni jambo ambalo tunatakiwa kujifunza au kufundishwa na watu wengine kote nchini.
"Ndugu zangu, ukirudi nyumbani utaona upungufu uliopo na wapi uboreshe," amesema.
Ameendelea, "Nimeambiwa hapa mmeanzisha utaratibu wa kujenga vyoo kwenye shule ambazo vyoo vyake ni chakavu lakini mmeanzisha mchakato wa kupandisha hadhi hospitali ya Huruma iwe ya hufaa, jambo hili kwa watu ambao hawarudi nyumbani hawawezi kuliona, hongereni sana watu wa Rombo."
Amesema Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan inafuatilia mambo wanayokusudia kufanya kwa ajili ya maendeleo ya watu.
"Nataka niwapongeze viongozi wanaotokea Rombo waliokuja kuungana na Mbunge kwa ajili ya Marathon hii, kurudi nyumbani ni jambo jema."
Dk Biteko alimpongeza Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda kwa ubunifu huo mkubwa alioufanya na kuwataka wengine kuiga ubunifu huo wenye tija kwa jamii.
"Ndugu zangu Wanarombo, nikitoka hapa bila kumshukuru Profesa Mkenda nitarudi nyumbani kichwa kikiniuma, nasema hivyo sio kwa sababu ni Mbunge mwenzangu, na sio kwa sababu ni Waziri mwenzangu au sio kwa sababu ni kaka yangu anayenifundisha mambo mengi, nasema hivyo kwa sababu ni jambo ambalo linahitaji ubunifu."
Kwa upande wake, Profesa Mkenda amesema fedha zitakazopatikana katika marathon hiyo zitasaidia kupunguza uhaba wa matundu ya vyoo 360 katika shule za msingi na sekondari katika wilayani humo.
Pamoja na mambo mengine Profesa Mkenda amesema fedha zitakazopatikana kutokana na mashindano hayo yaliyoandaliwa na ofisi yake, zitasaidia kupanua hospitali ya Huruma ili iwe ya rufaa.
Naye mmoja wa washiriki wa marathon hiyo, Fabian Oisso, amesema kama wadau wa maendeleo wataendelea kuhakikisha wanaunga mkono juhudi zinazofanywa na viongozi wa serikali ili kuhakikisha wanaleta maendeleo chanya katika jamii.
"Tunamshukuru Mbunge wetu kwa ubunifu huu mkubwa alioufanya wa kuhakikisha anawakutanisha Warombo wote waliopo ndani na nje ya wilaya hiyo, hii ni hatua kubwa mno kwetu sisi."