Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Dk Biteko: Tutaendelea kuwatambua, kuwapa tuzo watafiti bora

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko akifungua kongamano la 14 la kimataifa la kisayansi lililoandaliwa na Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Sayansi za afya na Tiba Shirikishi (Cuhas) leo Novemba 13, 2024 jijini Mwanza lililohusisha zaidi ya watafiti na wanasayansi 450 watakaojadili juu ya masuala ya afya ya binadamu, wanyama na mazingira. Picha na Saada Amir

Muktasari:

  • Serikali itaendelea kuwawezesha, kuwapa ufadhili na kuwatambua watafiti wanaofanya vizuri na kuchapisha majarida ndani na nje ya nchi.

Mwanza. Serikali imesema itaendelea kuwafadhili wanafunzi wanaosoma masomo ya sayansi pamoja na kuwatambua watafiti wanaofanya tafiti zinazoisaidia kuweka mipango mikakati ya kukabiliana na magonjwa mbalimbali nchini.

Akifungua kongamano la kimataifa la kisayansi lililoandaliwa na Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Sayansi za Afya na Tiba Shirikishi (Cuhas) lenye ujumbe wa Afya Moja na Usalama wa kidunia, leo Jumatano Novemba 13, 2024 jijini Mwanza, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko amesema ufadhili huo utawawezesha kusoma na nchi kupata wataalamu wengi katika sekta ya afya.

“Serikali itaendelea kuwawezesha, kuwapa ufadhili na kuwatambua watafiti wanaofanya vizuri na kuchapisha majarida ndani na nje ya nchi, endeleeni kufanya utafiti ili kupambana na aina yoyote ya maradhi,”amesema Dk Biteko.

Katika kongamano hilo linalowakutanisha zaidi ya watafiti na wanasayansi 450 kwa siku mbili kutoka Tanzania, Marekani, China, Ujerumani, Uingereza, Kenya, Zamba na Ghana, watajadili masuala mbalimbali ya afya ya binadamu, wanyama, mimea na mazingira.

Hivyo, Dk Biteko amesema machapisho zaidi ya 150 ya tafiti yaliyochapishwa na Cuhas yameisaidia Serikali kuweka mikakati mbalimbali ukiwamo wa kitaifa wa kukabiliana na usugu wa vimelea.

Ameongeza kuwa katika kuhakikisha nchi na Watanzania wanakuwa salama dhidi ya magonjwa yakiwamo ya mlipuko, Serikali kwa kushirikiana na wanasayansi imeandaa mpango mkakati wa Taifa wa afya moja wa 2022/27 unaozingatia utaalamu kati ya sekta ya afya ya binadamu, mifugo, wanyamapori na mazingira ili kupunguza milipuko ya magonjwa ambukizi (zuonotiki), usugu wa vimelea vya magonjwa dhidi ya dawa na matishio mengine ya afya.

Katika hatua nyingine, Dk Biteko amempongeza mwana sayansi bora wa afya kitaifa kwa mwaka 2024 ambaye ni mtafiti na profesa wa vimelea vya magonjwa Cuhas, Stephene Mshana aliyefanya tafiti zaidi ya 270 na kunukuliwa kimataifa.

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Omari Kipanga amesema kupitia mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) wenye thamani ya zaidi ya Sh972 bilioni unaenda kusomesha wataalamu 1,000 katika sekta ya afya.

Amesema mpango mwingine wa kuinua masuala ya sayansi na afya nchini, Serikali ina mkakati wa kujenga shule katika kila mkoa zitakazofundisha masuala ya sayansi kwa watoto wa kike ili kuibua wanasayansi wa kutosha na kuhudumia nchi na dunia kwa ujumla.

 “Suala la kuendeleza wana sayansi lipo, tuna mradi wetu mkubwa sana wa mageuzi ya kielimu kwa nyanja ya kiuchumi wenye thamani ya zaidi ya Sh972 bilioni, mradi huo pamoja na mambo mengine unaenda kutuhakikishia kuwa utasomesha wataalamu zaidi ya 1,000 katika sekta ya afya pamoja na sekta zingine lakini msisitizo mkubwa umewekwa kwenye sekta ya afya,” amesema.

Awali akitoa taarifa ya kongamano hilo, Makamu Mkuu wa Cuhas, Profesa Erasmus Kamugisha ameiomba Serikali kupitia Bodi ya Mikopo (HESLB) kuwakopesha wanafunzi wanaosoma sayansi ili kumudu gharama za masomo hayo alizosema ni kubwa.

 “Kwa awamu ya kwanza wanafunzi wetu wamepata kiwango fulani ambacho kitawapunguzia makali ya ada, kwa hiyo tunategemea pia awamu nyingine wataendelea kupata mikopo ili iwasaidie kulipa ada yao na chakula,” amesema Profesa Kamugisha

 “Wanafunzi wanaosoma sayansi katika vyuo vya afya, ada yao ni kubwa kuliko vyuo vingine kwa hiyo wasipopata mikopo inakuwa vigumu kumudu gharama za ada zinazotozwa vyuo vya sayansi, mikopo inawasaidia kupooza hayo makali ya ugumu wa kulipa hizo ada kwenye taasisi zetu.”

Mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya kongamano hilo, Profesa Mariam Mirambo amesema kongamano hilo litasaidia wanafunzi pamoja na wanasayansi wa ndani kupata fursa ya kujadiliana masuala mbalimbali ya kiutafiti pamoja na kupata uzoefu wa nini washiriki wanafanya kutoka kwenye nchi za nje.