Dk Biteko aitaka Tafiri kuwa daraja la wavuvi

Muktasari:
- Naibu Waziri Mkuu, Dk Dotto Biteko ameitaka Tafiri kuhakikisha inakuwa daraja la maisha la wavuvi.
Dar es Salaam. Naibu Waziri Mkuu, Dk Doto Biteko ameitaka Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (Tafiri), isione fahari kuona wavuvi wanaendelea kuwa masikini.
Ametaka fahari ya taasisi hiyo, itokane na kuwaona wavuvi wanakuwa na maisha bora yatakayojengwa na shughuli zao.
Dk Biteko ametoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam leo Alhamisi Oktoba 26, 2023 alipohutubia sherehe za kufunga maadhimisho ya miaka 40 ya Tafiri.
Katika hotuba yake hiyo, ametaka utendaji wa taasisi hiyo uwafanye wavuvi waione ndiyo kimbilio lao.
"Waziri (Mifugo na Uvuvi- Abdallah Ulega) bado una kazi ya kufanya wewe na watu wako (Tafiri), mnapaswa kuhakikisha mnakuwa kimbilio la wavuvi, oneni fahari kuwaona wavuvi wanakuwa matajiri na sio masikini," amesema.
Naibu Waziri Mkuu huyo, amesema wakati Tafiri inasherehekea miaka 40 ya kuanzishwa kwake, ni vyema ijikite katika mtazamo wa iliyoyafanya kuwaunufaisha wavuvi.
Kuhusu biashara ya samaki, amesema mwaka jana mauzo yalikuwa Dola za Marekani 168 milioni na mwaka huu hadi sasa yamefikia Dola za Marekani 249 milioni.
Licha ya sehemu kubwa ya Tanzania kuzungukwa na bahari, Dk Biteko amesema asilimia 85 ya mazao yote ya samaki yanatokana na mito, maziwa na mabwawa (maji baridi).
Amesema hatua hiyo inaonyesha umuhimu wa kuongezwa uwekezaji katika sekta ya uvuvi wa maji chumvi.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amesema sekta ya uvuvi kwa sasa imetoa ajira za moja kwa moja 2,000, huku wale waliojiajiri kwenye uchakataji ni zaidi ya milioni 4.5.
Alisema mchango wa sekta hiyo katika pato la taifa ni asilimia 1.7 na mwaka 2030 wanatarajia kufikia mchango wa asilimia 10.
Kuhusu uzalishaji wa samaki, amesema kwa sasa ni tani 500,000 na mwaka 2025/26 wanatarajia kuzalisha tani 600,000.
Ameeleza awali kulikuwa na vikwazo katika ufugaji wa samani kwenye vizimba, lakini sasa amesema vimerahisishwa kutokana na Tafiri kutambua maeneo yote ya ufugaji.
Katika hafla hiyo, ilizinduliwa programu tumizi inayowezesha wavuvi kutambua sakati walipo.
Kutokana na hilo, Ulega amesema kwa sasa watakwenda kuvua katika maeneo ambayo watakuwa na uhakika wa uwepo wa samaki wa kutosha.
Mwenyekiti wa Bodi ya Tafiri, Yahaya Mgawe ameiomba Serikali iinunulie taasisi hiyo boti kwa ajili ya shughuli za utafiti.
Ombi hilo, linatokana na kile alichofafanua, boti iliyokuwa ikitumika awali imeharibika na hata ikitengenezwa haitapewa leseni ya ubora.
Hata hivyo, amesema Sh6 bilioni ndicho kiwango cha fedha kinachohitajika kwa ajili ya kununua boti hiyo.
Katika hatua nyingine, Mgawe amesema kazi ya taasisi hiyo ni kuhakikisha takwimu na habari zinazohusu rasilimali za uvuvi, kijamii, kiuchumi na kimazingira, zinapatikana ili zitumike kufanya maamuzi ya utunzi wa sera kwa ufanisi.
"Serikali inapotaka kuona biashara inaendaje inatuuliza sisi sio kazi rahisi hiyo, ukiona samaki wanapatikana, viribatumbo vinapungua ujue TAFIRI tunafanya kazi," amesema.
Historia ya Tafiri
Akitia historia ya taasisi hiyo, Mkurugenzi wa kwanza wa Tafiri, Profesa Bwathon Philip amesema mzizi wa kuanzishwa kwa taasisi hiyo ni kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) mwaka 1977.
Ameeleza kabla ya kuvunjika kwa jumuiya hiyo shughuli zote za utafiti wa uvuvi wa maji baridi Afrika Mashariki zilikuwa zikifanywa nchini Uganda.
"Baada ya kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki mwaka 1977 Tanzania haikuwa na taasisi ya utafiti," amesema.
Hatua hiyo, amesema iliisababisha Tanzania kukusanya vikundi vyake mbalimbali vilivyokuwa vikifanya utafiti ikiwemo Mwanza, Kyela na Kigoma kuunda taasisi moja ya utafiti.
Baada ya hatua hiyo, amesema mwaka 1979 taasisi ya utafiti ilianzishwa lakini baadaye mwaka 1980 ndipo TAFIRI ilianzishwa baada ya vikao na Wizara.
Baada ya kuzaliwa, amesema ilikuwa ndani ya wizara na mwaka 1983 uzoefu wake ulimfanya apewe nafasi ya kuiongoza taasisi hiyo.
"Majukumu yalikuwa mengi na watafiti walikuwa wachache, wale waliokuwa Tafiri walikuwa sita na wengine waliobaki walikuwa watu wa uvuvi," amesema.
Mkurugenzi wa Misheni wa Shirika la Maendeleo la Marekani (USAID) nchini Tanzania, Craig Hart amesema shirika hilo limeongeza fedha za miradi wa Heshimu Bahari kutoka Dola za Marekani 13 milioni hadi Dola za Marekani 25 milioni.
"Uamuzi huu umetokana na mazungumzo ya ubalozi wa Marekani na Wizara ya uchumi wa Buluu ya Zanzibar, yaliyofanyika mwanzoni mwa mwaka huu," amesema.
Amesema nyongeza hiyo ya fedha itaongeza maeneo ya mradi huo kuhakikisha ushirikishwaji wa wanawake katika shughuli za uvuvi na utunzaji wa rasilimali za bahari.