Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

DJ afungwa maisha Simanjiro kwa kubaka

Muktasari:

  • Mchezesha muziki huyo Athuman Juma (Big dad) mkazi wa Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara, amehukumiwa kifungo cha maisha jela baada ya kukutwa na hatia ya kumbaka mtoto ambaye ni msichana mwenye umri wa miaka 14.

Simanjiro. Mchezesha muziki (DJ) na mkazi wa kitongoji cha Jitegemee katika mji mdogo wa Orkesumet, wilayani Simanjiro mkoani Manyara, Athuman Juma maarufu kama Big Dad, amehukumiwa kifungo cha maisha jela baada ya kupatikana na hatia ya kumbaka msichana mwenye umri wa miaka 14.

Mahakama ya Wilaya ya Simanjiro imetoa hukumu ya kifungo cha maisha jela kwa mshtakiwa huyo Juma, baada ya kupatikana na hatia ya kumbaka msichana wa miaka 14.

Awali, waendesha mashtaka wa Serikali, Mary Lucas na Johnson Ndibalema, waliieleza mahakama kuwa Athuman Juma alitenda kosa hilo Desemba 24, 2024, katika maeneo ya Jitegemee, mji mdogo wa Orkesumet, wilayani Simanjiro.

Lucas ameieleza mahakama kuwa mshtakiwa alimfuata mlalamikaji nyumbani kwao, ambapo alikuwa akiishi na dada yake baada ya kuhitimu elimu ya msingi ya darasa la saba.

Amesema kuwa siku ya tukio, dada wa mlalamikaji aliondoka nyumbani akiwa na rafiki yake, na kumuacha mdogo wake peke yake, hali iliyotumiwa na mshtakiwa kumuingilia na kumbaka.

Hakimu Charles Uiso akisoma hukumu ya kesi hiyo namba 696/2025 leo Juni 25, 2025 ameeleza kuwa mahakama imeridhishwa na ushahidi uliowasilishwa mahakamani hapo na mashahidi watano na kielelezo kimoja cha fomu namba tatu ya polisi iliyojazwa na daktari.

Hakimu Uiso ameeleza kwamba ushahidi huo umemuunganisha mshtakiwa kutenda kosa hilo na kuhukumiwa kifungo hicho cha maisha jela.

Kabla ya kuhukumiwa adhabu hiyo mshakiwa huyo ambaye alikuwa nje kwa dhamana ya watu wawili kwa bondi ya Sh2 milioni aliruka dhamana kwa kutoroka na kutohudhuria mahakamani hata hivyo alikamatwa.

Hata hivyo, mwendesha mashtaka Ndibalema ameiomba mahakama hiyo kumpa adhabu kali mshakiwa huyo ili iwe funzo kwa jamii kutojihusisha na ubakaji.

Ndibalema amesema japokuwa mshakiwa huyo hana kumbukumbu za kufanya makosa kama hayo, ila apewe adhabu kali kutokana na kosa hilo.

Kutokana na ushahidi uliowasilishwa na upande wa mashtaka, Hakimu Uiso alimhukumu mshtakiwa huyo kifungo cha maisha jela kwa kosa la kubaka, akieleza kuwa adhabu hiyo ni ya kisheria na inalenga kutoa fundisho kwa wengine.