Diwani, wenzake 13 mbaroni tuhuma za mauaji

Kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mutafungwa akizungumza na waandishi wa habari mkoani Mwanza. Picha na Mgongo Kaitira
Muktasari:
- Mauaji ya mwanamke huyo yalitokea Novemba 5 mwaka huu katika Kitongoji cha Ikoni 'B' wilayani Sengerema mkoani Mwanza baada ya kundi la watu wenye hasira kali likiongozwa na diwani huyo kuvamia na kumshushia kipigo wakimtuhumu kuiba mihogo katika shamba lililokuwa linamilikiwa na mmewe, Ndebete Mzee 'Miharalo'.
Mwanza. Jeshi la Polisi mkoani Mwanza linawashikilia watu 14 akiwamo Diwani wa Kata ya Buzilasoga wilayani Sengerema mkoani Mwanza, David Shilinde kwa tuhuma za kumuua kisha kumchoma moto Mkazi wa Kitongoji cha Ikoni 'B' wilayani humo, Getruda Dotto.
Mauaji ya mwanamke huyo yalitokea Novemba 5 mwaka huu katika Kitongoji cha Ikoni 'B' baada ya kundi la watu wenye hasira kali likiongozwa na diwani huyo kuvamia na kumshushia kipigo wakimtuhumu kuiba mihogo katika shamba lililokuwa linamilikiwa na mmewe, Ndebete Mzee 'Miharalo'.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mutafungwa amewaeleza waandishi wa habari mkoani hapa leo Jumanne Novemba 8, 2022, kuwa uchunguzi wa mauaji hayo umebaini kuwa yamesababishwa na mgogoro wa shamba lenye ukubwa wa nusu eka.
Amewataja watuhumiwa wengine wanaoshikiliwa kwa tuhuma za Mauaji ya mwanamke huyo kuwa ni Mwenyekiti wa Kitongoji cha Ikoni 'B', Emmanuel Makala (48), Kamanda wa kikosi cha Sungusungu, William Nego (54) na Afisa Mtendaji kijiji cha Ikoni 'B', Tiruloza Alphonce (59).
Wengine ni Ndilili Wali (60), Fikiri Wali (48), Zakaria Meshack (48), Zakaria Antony (48), Msafiri Jonas (38), Faustine Masweda (49), Anthony Method (24), Yusuph Simon (26), Peter Lucas (29), James Mazengo (30).
"Huyu Diwani na wenzake walikuwa wakimtuhumu Getruda Dotto kwa kosa la wizi wa mihogo kutoka kwenye shamba la Scholastica John ambalo awali lilikuwa linamilikiwa na mme wa Getruda Dotto, Ndebete Mzee 'Mihalalo'," amesema
Kamanda Mutafungwa amesema; "Sasa mama huyo alienda kuchimba mihogo kwenye shamba hilo akiamini kwamba ni shamba la mme wake kumbe lilishauzwa kwa Scholastica John ndipo wakamfanyia unyama huu,"
Kamanda huyo amesema watu hao baada ya kumpiga na kumuua mama huyo walichukua mwili wake na kuuteketeza kwa moto kisha kubomoa nyumba aliyokuwa akiishi na watoto wake wawili.
Mutafungwa amesema msako wa kuwakamata wahusika waliotoroka unaendelea kisha watafikishwa mahakamani kwa hatua za kisheria.
"Pamoja na mwanamke huyo kujitetea kuwa shamba alilochimba mihogo ni mali ya mmewe, Ndebete Mzee 'Mihalalo' walishirikiana kumshambulia, tutawakamata wote waliohusika kwa sababu tukio hili lilifanyika mchana kweupe watu wakishuhudia," amesema