Deni la Taifa lapaa kwa Sh6.9 trilioni kwa mwaka

Muktasari:
- Inaelezwa kuwa pamoja na deni kukua, fedha zinatumika kuwekeza kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo.
Dar es Salaam. Wataalamu wa uchumi nchini wamesema deni la Taifa litakuwa na afya kwa uchumi wa nchi iwapo fedha zilizokopwa zitatumika katika uwekezaji wenye tija.
Kulingana na Benki Kuu ya Tanzania (BoT), katika taarifa ya mwezi Februari ya mapitio ya uchumi (MER), deni la Taifa limeongezeka kwa Sh6.9 trilioni katika kipindi cha mwisho wa Januari mwaka huu, ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka jana.
Katika kipindi hicho, deni limeongezeka kutoka Dola za Marekani 37.6 bilioni (zaidi ya Sh86.5 trilioni) hadi Dola za Marekani 40.6 bilioni (zaidi ya Sh93.4 trilioni).
“Deni limefikia kiwango hicho hasa kutokana na uwekezaji mkubwa unaofanywa kwenye miradi ya maendeleo,” alisema Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano serikalini katika Wizara ya Fedha na Mipango, Benny Mwaipaja.
Kwa mujibu wa Mwaipaja, Watanzania hawapaswi kuwa na wasiwasi kuhusu deni hilo.
Baadhi ya miradi hiyo ni pamoja na Reli ya Kisasa (SGR), Mradi wa Kufua Umeme wa Julius Nyerere (JHPP), upanuzi wa bandari ya Dar es Salaam na ujenzi wa miundombinu ya mradi wa mabasi yaendayo haraka Dar es Salaam. “Watanzania hawapaswi kuwa na wasiwasi kwa kuwa deni la Taifa limeendelea kuwa himilivu kwa muda mfupi, wa kati na mrefu. Tutaendelea kukopa kwa umakini, tutahakikisha kila tunachokopa, kinatumika katika lengo lililokusudiwa,” alisema Mwaipaja.
Akirejea msimamo wa Serikali, mtaalamu wa uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe, Profesa Aurelia Kamuzora alisema kiwango cha deni kilichopo sasa hakipaswi kuwatia hofu Watanzania, licha ya kuwa deni linaongezeka. “Deni kuwa kubwa sio tatizo, tatizo ni namna gani tunatumia hicho tulichokikopa,” alisema na kuongeza wanahitajika wataalamu watakaoishauri Serikali namna ya kufanya uwekezaji kwa fedha ya mkopo ili kupata faida na marejesho.
Alisema hashangazwi na kiwango cha deni hilo, kwa sababu Tanzania haina mtaji wa kutosha kugharimia miradi mikubwa.
Hoja ya Profesa Kamuzora inaungwa mkono na Dk Abel Kinyondo, mtaalamu wa uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), aliyesema ni sawa kutumia zaidi, lakini iwe kwa uzalishaji wenye tija.
“Deni ni matokeo ya matumizi ya kupitiliza. Ingawa matumizi zaidi kwenye uwekezaji wenye tija sio tatizo kwa sababu unatarajiwa kuwa na matokeo chanya, ndiyo maana nasisitiza kuzingatia nidhamu ya matumizi,” alisema Dk Kinyondo.
Pia, alisema mikopo ya masharti nafuu ndiyo inayopaswa kupewa kipaumbele zaidi, badala ya yenye masharti ya kibiashara. Hata hivyo, alionyesha wasiwasi kwa kusema kuwa Tanzania imefikia uchumi wa kati daraja la chini, kwa siku zijazo kuna hatari ya kukosa vigezo vya kupata mkopo wenye masharti nafuu. Akijibu hoja hiyo, Mwaipaja alisema asilimia 73 ya mikopo ya Tanzania ni ya masharti nafuu na riba yake ni chini ya asilimia moja na ina kipindi kirefu cha kulipa.
Kwa upande wa mtaalamu wa biashara na uchumi, Donath Olomi alisema kwa miradi mikubwa ya miundombinu inayojengwa, si ajabu kuona deni la Taifa likiongezeka. “Haitawezekana kwa Tanzania kutekeleza miradi muhimu ya miundombinu bila kukopa, hatuna fedha zetu wenyewe,” alisema. Hata hivyo, alisema ili kupunguza kukopa, Taifa linapaswa kuishirikisha sekta binafsi katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo kupitia ubia wa Serikali na sekta binafsi (PPP).
Katika hilo, Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akisisitiza kuwa Serikali itaendelea kutafuta mikopo kwa ajili ya kugharimia utekelezaji wa miradi ya miundombinu.