Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

DC Mpogolo: Bajaji za wenye ulemavu kuwa na utambulisho

Dar es Salaam. Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo amesema wanatarajia kuweka alama na namba maalumu kwenye bajaji zinazobeba abiria zinazomilikiwa na watu wenye ulemavu kwa lengo la kuzitambua zinazofika katikati ya Jiji.

Pia amewataka kufuata sheria za usalama barabarani wanapokuwa wanaendesha vyombo vya moto na kuacha tabia ya kuzozana na askari wa barabarani, wavunjapo sheria hizo.

Mpogolo amesema hayo alipokuwa kwenye Mkutano Mkuu wa Umoja wa Walemavu Waendesha Bajaji Dar es Salaam (Uwawabada), amesema kwa vyombo ambavyo vinaingia katikati ya jiji, vitawekewa alama na namba za utambuzi.

Amesema uamuzi huo unatokana na kikao cha Kamati ya Usalama Barabarani, ambapo walikubaliana juu ya jambo hilo, hata hivyo, suala hilo bado linasubir baraka za vikao vingine, kisha liundiwe sheria ndogo na hatimaye liweze kufanyika.

“...tunakuwekea alama na namba ili yeyote atakayekuwepo katikati ya jiji hana namba mtamjua huyu si mwenzenu...niwaombe mnapokuwa mnajadili na kuazimia, wekeni na uataratibu wa nini kifanyike kwa atakaye kwenda kinyume na maazimio yenu,” amesema.

Mpogolo amesema Serikali inawajibu wa kuwalinda, hata hivyo ameonya wale watakao chukua bajaji za watu wenye ulemavu na kuendesha na wasio na ulemavu kuwa sheria itachuku mkondo wake.

“Mnatakiwa kutafakari suala hilo, kwani kuna baadhi mnawapatia vyombo vyenu ndugu zenu wasio na ulemavu, kisha mnawapa na baadhi ya viungo vyenu bandia ili waonekane ni walemavu, jambo hili siyo jema na linarudisha nyuma maenedeleo,” amesema.

Mpogolo amesema baada ya zoezi la kuwekewa alama na namba hizo, Serikali itachukua hatua kali za kisheria kwa mtu yoyote atakaye kwenda kinyume na makubaliano yatakayopitishwa katika mkutano wao mkuu.

Pia aliwataka kufuata sheria ya upakiaji na kujua wanatakiwa kubeba abiria wangapi katika kila bajaji na hivyo kupunguza changamoto zinazowakabili barabarani.

Alieleza Serikali iko pamoja na watu wa makundi maalum ndiyo maana imetoa asilimia 2 katika kila halmashauri kwa ajili ya kundi hilo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Walemavu Tanzania (Chawata), Hamad Komboza amesema mazingira ya ofisi nyingi za Serikali siyo rafiki kwa watu wenye ulemavu hivyo yanatakiwa kuboreshwa.

Komboza amesema watu wenye ulemavu wanaoendesha bajaji, katikati ya mji wana changamoto ya maegesho kutokana na kuchanganyika na watu wa kawaida hali inayowasababisha kukosa abiria kwa sababu hawawezi kupambana kutafuta wateja na watu wa kawaida.

Kwa upande wa Katibu wa Uwawabada, Hamis Mjanameli ameiomba Serikali kuwatengea maegesho yao maalum katika vituo vya kupakia abiria.

“Unakuta kuna abiria anakuja kituoni anayemuwahi abiria huyo ni mtu wa kawaida, mwenye ulemavu  inakuwa ni vigumu kwake kuweza kupambana kutokana na mazingira yanayomzunguka,” amesema Mjanameli.