Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Dawa mpya ya uzazi wa mpango kwa wanaume yazua mjadala


Muktasari:

  • Njia hiyo mbadala ya uzazi wa mpango iliyo katika mfano wa mafuta (jeli) itapakwa kwenye mabega na kusababisha mbegu kutokuwa na nguvu za kutosha kumpa mwanamke ujauzito.

Dar es Salaam. Watafiti wamefanikiwa kugundua njia ya uzazi wa mpango kwa wanaume, kupitia dawa maalumu itakayotumia homoni mbili za kiume ambazo ni nestorone na testosterone kuzuia uzalishaji wa mbegu katika manii za mwanaume.

Dawa hiyo iliyo katika mfano wa mafuta (jeli) itakuwa ikipakwa na wanaume kwenye mabega yao, mara moja kwa siku na matokeo yake itazuia uzalishaji wa mbegu za kiume.

Hata hivyo, wataalamu wa afya nchini, wameichambua dawa hiyo na kuainisha faida na hasara zake, huku wakisema utafiti zaidi unahitajika ili kuondoa wasiwasi kwa watumiaji.

Kiongozi wa utafiti huo, Diana Blithe kutoka Taasisi za Kitaifa za Afya na Baraza la idadi ya watu nchini Marekani, amesema matokeo hayo yameleta mbinu sawa na njia za kudhibiti uzazi kwa wanawake.

Shirika la habari la CNN limeripoti kuwa geli hiyo itawasaidia wanaume kukaa kwenye hali nzuri ya kiafya, lakini mbegu zao hazitokuwa na nguvu za kutosha kumpa mwanamke ujauzito.

Watafiti hao wamesema ikiwa mwanamke atasahau kidonge cha uzazi wa mpango kwa siku moja au mbili, anaweza kuepuka mimba zisizotarajiwa pale ambapo mwenza wake atapaka hiyo dawa mabegani.

Utafiti umeonyesha pia kuwa mbegu za kiume zitaweza kuongezeka nguvu kwenye muda wa wiki nane  hadi 10 baada ya mwanaume kusitisha matumizi ya dawa hiyo.


Maoni ya wataalamu

Daktari bingwa wa fiziolojia ya homoni na mazoezi kutoka Chuo Kikuu cha Afya Kishiriki cha Sayansi Muhimbili (Muhas), Fredrick Mashili amesema dawa hiyo inasitisha uzalishaji wa mbegu lakini inaingilia homoni ya kiume kwa kiasi fulani.

“Lakini kwa mtazamo wa kiafrika nahisi italeta changamoto kidogo. Imetajwa kuzuia kutengeneza mbegu, kwa kuifikiria haraka kitu chochote kinachoingilia homoni ya kiume ya testosterone inaweza kuingilia pia nguvu za kiume.

“Homoni ya kiume hata kama mtu hataki mtoto, bado atataka kufanya tendo la ndoa. Uhakika kwamba hii dawa haiingiliani na uwezo wa kufanya tendo la ndoa yaani nguvu za kiume, kwa jinsi inavyofanya kazi ni ngumu kidogo,” amesema Dk Mashili.

Hata hivyo amesema kuna njia za uzazi wa mpango kwa wanaume ikiwemo kufunga mirija  na nyinginezo lakini bado wengi hawatumii.

“Kwa mila zetu sisi hata kwenye masuala ya uzazi au ugumba, wanaume wanakataa kwenda hospitali ni suala linalochukua muda kulikubali,” amesema Dk Mashili.

Maoni hayo yametolewa pia na Daktari bingwa wa magonjwa ya mfumo wa mkojo kutoka Hospitali ya Mloganzila, Deogratius Mahenda anayesema huo ni miongoni mwa tafiti zilizofuatiliwa muda mrefu duniani lakini bado unaacha maswali mengi.

Dk Mahenda amesema ili mwanaume aweze kumpa mbegu mwenza wake, kiasi cha mbegu kinatakiwa kiwe cha kutosha kati ya milioni 15 mpaka 20 kwa mshindo mmoja na wengi wanatoa mbegu milioni 15 mpaka milioni 200.

Amesema taarifa hiyo haijaonyesha hicho kiwango cha mbegu kilipungua kwa kiasi gani, mbegu lazima ziwe na ubora pamoja na wingi inatazamwa kama maumbile yake yalikuwa sawasawa na wingi halikadhalika.

“Kichwa cha mbegu kinatakiwa kiwe kimechongoka, kiwiliwili kiwe na mkia kupenyeza na kuingia kwenye yai, hizi habari hazijasema kama kuna athari zozote kwenye ubora wa mbegu,” amesema.

“Haijaelezwa wakitumia kinababa wanapata changamoto gani, kama wenza wanapanga kutokuwa na mtoto inaweza kufaa? Tafiti inahitajika zaidi. Bado ule ubora wa mbegu utarudi sawasawa au utengenezaji pekee, hatujaambiwa kama kutakuwa na madhara ni ya muda mfupi, anapoacha dawa inaendelea?”

Dk Mahenda amesema lazima kuwe na homoni zilizolingana na je, inaenda kupunguza hizo homoni, bado tafiti hiyo ina maswali mengi.


Wasemavyo wanaume

Matthew Treviño (35) kutoka Sacramento, California alishiriki katika utafiti huo. Alipakaa  jeli kidogo kwenye kila bega asubuhi na kusema kuwa imekuwa kawaida kama kuoga na kupiga mswaki.

Kando na kuongezeka uzito kidogo, hakuwa na malalamiko, alisema hamu yake ya ngono imeongezeka, "Nimepata tu kuongezeka kwa hamu.”

Hata hivyo baadhi ya wanaume wa Kitanzania walikuwa na maoni tofauti.

“Hapa ndio mimba zitakataliwa vizuri. Anakudunga mimba anakuruka si yake, alitumia uzazi wa mpango kuna faida na hasara ya hiki kitu, japokuwa lazima dunia ikubali mabadiliko,” amesema Salum Othman mkazi wa Tegeta Dar es Salaam.

Onesmo John mkazi wa Morogoro amesema, “Hapa kuna mtego mkubwa kwa wanaume, sababu hizi dawa zinakwenda kubadili mfumo mzima wa homoni za mwanaume sasa je, unategemea nini kitafuata hapa.”