Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Dada aeleza kilichotokea kabla ya mauaji ya Aneth

Muktasari:

  • Aliyekuwa dada wa kazi wa marehemu Aneth Msuya, juzi alianza kutoa ushahidi wake katika kesi ya mauaji ya aliyekuwa mwajiri wake.

Dar es Salaam. Aliyekuwa dada wa kazi wa marehemu Aneth Msuya, juzi alianza kutoa ushahidi wake katika kesi ya mauaji ya aliyekuwa mwajiri wake.

Akiwa shahidi wa 25 wa upande wa mashtaka katika kesi hiyo inayosikilizwa na Jaji Edwin Kakolaki wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Getruda Mfuru (38), mama wa watoto watatu, pamoja na mambo mengine, alielezea sehemu ya matukio yaliyojiri kabla ya mauaji ya mwajiri wake huyo.

Ushahidi wake

Akiongozwa na mwendesha mashtaka, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Paul Kimweri, alisema mwaka 2015 aliamua kutafuta kazi za ndani, akakutana na mama mmoja aitwaye mama Manka ambaye baada ya kumweleza hitaji lake alimweleza kuwa kuna mama mmoja anaishi Cairo Mererani, anaitwa Bibi Msuya anatafuta msichana wa kazi.

Hivyo mama Manka alimuunganisha naye. Baada ya mazungumzo, Bibi Msuya alimtumia Sh10, 000 kupitia M-pesa kwa ajili ya nauli ya kwenda kwake Cairo Mererani.

Hivyo Februari 15, 2015 alisafiri kwenda kwa bibi Msuya huko Mererani, ambako walikubaliana kufanya kazi kwa malipo ya Sh40, 000 kwa mwezi. Mbali na yeye, walikuwepo wafanyakazi wengine watatu wa kike.

Alifanya kazi hapo mpaka Agosti 28, 2015, alipoondoka kurudi nyumbani kwa bibi yake Masama Sonu, kuangalia watoto wake.

Kwa muda alioishi kwa bibi Msuya, alifanikiwa kuwaona watoto wake wanne, Antuja, Bahati, Joyce na Aneth.

Baada ya kurudi, bibi Msuya alimpigia simu akamweleza kuwa mtoto wake Aneth, anahitaji mfanyakazi na yeye Getruda akasema anaweza kwenda, hivyo bibi Msuya akamwambia asubiri amuunganishe na Aneth aliyekuwa akiishi Dar es Salaam.

Alisema Januari 4, 2016; aliondoka na Antuja, dada wa Aneth kwenda Kigamboni Dar es Salaam alikokuwa akiishi marehemu.

Alipofika kwa Aneth, Kigamboni alielezwa majukumu ya kazi na wakakubaliana mshahara wa Sh60, 000 kwa mwezi. Pia Aneth alimuahidi kuwa ikifika mwezi Juni 2016 angemuongezea mshahara.

Hivyo alianza kazi na maisha katika familia ya Aneth iliyokuwa ni ya watu watatu, Aneth mwenyewe, mtoto wake Allan na yeye mwenyewe Getruda.

Kwa muda aliokaa pale hakuwahi kumuona rafiki au mume wa Aneth pale nyumbani isipokuwa Aneth aliishia kumuonesha mumewe kwenye picha tu.

Hata hivyo, alisema Mei 15, 2016 majira ya mchana alitokea geti la nyuma ya nyumba hiyo kwenda dukani kununua karatasi za chooni (toilet paper), njiani alikutana na gari la rangi ya buluu nyeusi.

Kioo cha nyuma cha pili kutoka kwa dereva wa gari hilo, kilishushwa na akamuona mama mmoja aliyevaa suti ya buluu fulana ya ndani nyeusi na shingoni alikuwa amevaa cheni mbili moja kubwa moja nyembamba zenye mwonekano wa dhahabu na hereni za dhahabu.

Alikuwa ni mwenye uso wa mviringo na alikuwa amesuka nywele za kitimutimu na kisha aliomba kuongea naye.

Alipofika kwenye ile gari aligundua kuna mtu mwingine wa kiume, alikuwa upande wa dereva wa hiyo gari.

Yule mama alimuuliza kama anapajua kwa Aneth Msuya naye akajibu kuwa ndio anapajua. Kisha akimuonesha kwa ishara ya kidole nyumba na akamwambia kuwa anaishi naye ni dada yake.

Yule mama alisema ni ndugu yake (Aneth) na kwamba ana siku nyingi hajamuona lakini akamwambia kuwa wataonana keshokutwa, Mei 17, 2016. Siku hiyo Mei 15, Aneth alikuwa kazini.

Alisema pia Mei 18, 2016 majira ya saa 4 asubuhi alipotoka kuchota maji alimkuta huyo mama wamesima nje ya geti akiwa na yule mwanaume aliyekuwa naye kwenye gari Mei 15.

Siku hiyo yule mama alikuwa amevaa suti ya maziwa, viatu vya zambarau, cheni kubwa mbili, na hereni na kichwani alikuwa amesuka kwa mtindo wa ‘weaving.’

Chini alikuwa amevaa sketi fupi ya suti na miguu yake haikuwa nyembamba na juu alikuwa mnene.

Yule mwanaume alikuwa amevaa suti nyeusi, shati jekundu, viatu vyeupe, miwani juu ya paji la uso. Kwa umbo alikuwa mrefu wa kati, mnene wa kati na mweusi.

Yule mama alipomuita ilibidi arudishe ndoo ndani akafunga geti kisha akawafuata, lakini iliporudi aliwakuta wameshaingia kwenye gari ya kifahari aina ya Rangerover yenye rangi ya fedha waliyokuwa nayo.

Alipofika yule mama alimtaka aingie kwenye gari na alipoingia alikuta watu watatu na yeye akawa wa nne. Kulikuwa na mwanaume mwingine ndani ya gari. Alikuwa amevaa fulana nyekundu na suruali ya jinzi ya bluu.

Ndani ya gari alikaa katikati ya yule mama na yule kijana mwingine mwenye fulana ya bluu na yule mama alichukua pochi akafungua upande wa zipu ndogo akatoa simu aina ya Nokia ndogo, akampa.

Alimwambia ashike hiyo simu watakuwa wanawasiliana naye mara na asiwasiliane na mtu mwingine yeyote na kwamba wakijua kuwa anawasiliana na mtu mwingine yeyote watamuwajibisha.

Yule mama aliongea na dereva akisema: "Mali nitafute mimi na mume wangu wengine wanazihangaikia za nini?"

Yule mwanaume alimjibu kwa kuguna, "mmmh,” kisha akasema hao ni wapumbavu tu.

Yeye Getruda alimuuliza yule mama hiyo simu ni ya nini na yule mama akamjibu kuwa watakuwa wanawasiliana mara kwa mara.
Kisha alisema yule mwanaume aliyevaa fulana nyekundu alichukua bastola akamuwekea shingoni upande wa kushoto.

"Nilijisikia vibaya na kuingiwa na hofu kubwa sana," alisema Getruda.

Simu ile aliyopewa ilikuwa na mtandao wa Airtel lakini namba zake hakuzishika kichwani.

Baada ya kumpatia hiyo simu pia walimwambia kuwa wana kazi na Aneth, alipomuuliza yule mama kuwa ni kazi gani hiyo alimjibu kuwa yeye haimhusu.

Kisha yule mama alimuuliza kama anapafahamu nyumbani kwa kina Aneth Msuya, yeye akajibu kuwa hapana. Yule mama akamuuliza kama anamfahamu yeye akajibu hapana kisha akamuuliza yeye anatokea wapi? Akamjibu Machame Hospitali.

Alimjibu hivyo kuwa hapafahamu kwao Aneth kwa sababu tayari walikuwa wameshamtishia kwa bastola shingoni.

Wakati anamuuliza hayo maswali, alivuta kumbukumbu kuwa aliwahi kumuona wapi na akakumbuka kuwa wakati anafanya kazi kwa bibi Msuya, waliwahi kwenda na bibi Msuya akamtambulishwa kuwa ni mke wa marehemu Erasto, aliyekuwa mtoto wake.

Kisha alishuka kwenye gari na kuelekea nyumbani na wale waliokuwa kwenye gari waliondoka kuelekea barabara kuu.

Alipoingia ndani (ya geti) alizima ile simu, akaificha kwenye kochi dogo ambalo lilikiwa nje barazani lililokuwa halitumiki, ili Aneth asisikie akiwasiliana na mtu mwingine yeyote yule.

Kesho yake (Mei 19) Aneth alipoondoka kwenda kazini yeye aliiwasha ile simu.

Hakuweza kumueleza Aneth chochote kuhusu matukio hayo kwa madai kuwa vitisho vile alivyopewa vilimuogopesha.

Mei 23 2016 akiwa nyumbani alipigiwa simu na yule mama katika simu ile aliyopewa, akamwambia kuwa waonane nje.

Alitoka akawakuta mbele ya nyumba lakini yule mama akamuomba wasogee pembeni kidogo. Walikuwa na ile gari ya Rangerover ya rangi ya fedha.

Alipofika alichungulia ndani ya gari yule mama akamwambia aingie ndani ya gari.

Kesi hiyo itaendelea kesho ambapo shahidi huyo ataendelea na sehemu ya pili ya simulizi yake kabla ya kuwekwa katika kikaango cha maswali ya dodoso kutoka kwa mawakili wa utetezi.