Chalamila afunguka binti aliyedhalilishwa na 'waliotumwa na afande’

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila. Picha na Maktaba
Muktasari:
- Watetezi wa haki za binadamu watoa wito kwa Rais Samia Suluhu Hassan kukemea tukio hilo na kuunda tume huru kuchunguza matukio yote yaliyoripotwa kufanywa na watumishi wa vyombo vya ulinzi na usalama.
Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amesema kitendo alichofanyiwa binti anayedaiwa kuwa mkazi wa Yombo, ni kinyume cha sheria na maadili ya Mtanzania.
Amesema binti huyo kwa sasa yupo kwenye mikono salama ndani ya moja ya vituo vya mkoa wake, akipata elimu ya unasihi itakayomsaidia kujikuza katika maisha yake ya kila siku.
Chalamila amesema hayo jana Agosti 8, 2024 akizungumza na Mwananchi ikiwa ni siku nne zimepita tangu Agosti 4, ziliposambaa picha jongefu kwenye mitandao ya kijamii zikiwaonyesha vijana watano wakimbaka na kumlawiti binti huyo, huku wakimtuhumu kwa kile kilichosikika katika video hiyo kuwa ametembea na mume wa mtu wakimtaka kumuomba radhi mtu waliyemwita kwa jina la ‘afande’.
Wakati Chalamila akieleza hayo, watetezi mbalimbali wa haki za binadamu wametaka hatua za haraka zichuliwe dhidi ya waliohusika katika tukio hilo, huku wakitoa wito kwa Rais Samia Suluhu Hassan kuunda tume kuchunguza matukio yote yaliyofanywa na watumishi wa vyombo vya ulinzi na usalama.
Chalamila amesema kitendo alichofanyiwa binti huyo, kinalaaniwa na Serikali kwa nguvu zote, kwani ni kinyume cha sheria za nchi na utamaduni wa Mtanzania.
“Binti yupo mikono salama hajafa, mimi mkuu wa mkoa nafahamu kabisa yupo salama, yupo kwenye moja ya vituo vyetu na lazima binti huyo awe salama apone kisaikolojia, aweze kutulizwa vizuri na kupewa elimu ya unasihi itakayomsaidia kujikuza katika maisha yake ya kila siku,” amesema Chalamila.
Amesema kitendo kilichotokea ni uthibitisho kwamba wapo baadhi ya wazazi wamekuwa na aina ya malezi yanayochangia kutokea matukio hayo.
Kwa mujibu wa Chalamila, waliotenda matukio hayo hawakutoka mbinguni au ardhini bali duniani, na wamezaliwa na baba na mama.
Amesema watoto wasipolelewa vizuri, mwisho wanaweza kufanya vitendo visivyoendana na dira, muonekano na hadhi ya dunia na Taifa.
“Kwa tukio hilo tukiwa wakazi wa Dar es Salaam tunalaani vikali. Natoa wito kwa wazazi wetu kuhakikisha wanawapitisha watoto katika malezi ambayo yatakuwa msaada katika uzalendo, utu na makuzi yanayomuogopa Mungu katika misingi ya utamaduni wa Taifa letu,” amesema.
Kuhusu uchunguzi
Chalamila amewataka Watanzania kuwa watulivu wakati ufuatiliaji wa tukio hilo ukiendelea. Amesema tayari Jeshi la Polisi limeshaweka bayana namna ambavyo linashughulikia jambo hilo.
“Mimi Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam nimemsikia binti anapoulizwa anasema anatokea Yombo na kwa mantiki hiyo Jeshi la Polisi kwanza litathibitisha binti anapotoka na pia kuthibitisha tukio limetokea wapi,” amesema.
Amesema katika video iliyosambaa mtandaoni binti yule alisema ni mkazi wa Dar es Salaam lakini haikusemekana tukio lile lilitokea wapi, hivyo vyombo vya ulinzi vitathibitisha.
Watetezi wa haki
Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) Kanda ya Mashariki na Pwani, Michael Marwa amesema wito wao kwa Rais Samia, ni kutaka akemee tukio hilo na kuunda tume huru kuchunguza matukio yote yaliyoripotwa kufanywa na watumishi wa vyombo vya ulinzi na usalama.
"Maombi haya yamekuwepo kwa miaka mingi lakini hakuna chombo huru cha kushughulikia masuala haya ambayo yanachafua taswira ya nchi," amesema Marwa.
Kutokana na hali hiyo, amelitaka Jeshi la Polisi kuchukua hatua stahiki za kuwakamata watuhumiwa waliombaka na kumlawiti binti huyo, kuwafikisha mahakamani ili wapewe adhabu kwa mujibu wa sheria na iwe funzo kwa wengine wenye tabia za aina hiyo.
Kwa upande wake, mwakilishi wa shirika la msaada wa kisheria la Wochaid Temeke, Fauzia Lema amemuomba Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dk Dorothy Gwajima kumhakikishia mwathirika wa ukatili huo usalama wake na familia.
Pia waziri awaagize wataalamu wa wizara yake kumpa huduma ya unasihi na msaada wa saikolojia jamii na afya ya akili.
"Naiomba jamii kwa ujumla waache kusambaza taarifa za uongo zinazohusu tukio hili na kuwakumbusha kuwa kusambaza taarifa za uongo na zenye kuleta taharuki kwenye jamii, ni kosa kisheria kwa mujibu wa sheria ya makosa ya kimtandao na sheria ya kulinda taarifa binafsi," amesema.
Ilichosema Tamwa
Wakati huohuo, Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (Tamwa) kimevitaka vyombo vya usalama na hasa Jeshi la Polisi kuongeza nguvu ya kukabiliana na ukatili unaoendelea kwa kasi nchini.
“Tamwa, inakemea vitendo vyovyote vya udhalilishaji wa wanawake na watoto, na ndiyo maana ilihamasisha kuundwa kwa Sheria ya Makosa ya Kujamiiana (SOSPA) ya mwaka 1998 ambayo inapinga na kukomesha vitendo vya ubakaji kwa ujumla wake,” imesema taarifa ya chama hicho.
Tamwa imesema vitendo hivyo vya kinyama havikubaliki katika Taifa ambalo limejengwa kwa misingi ya haki, usawa na staha, na itaendelea kupaza sauti dhidi ya ukatili huo hadi mwathirika wa tukio hilo atakapopata haki.
Naye Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Boniface Mwabukusi Agosti 5, 2024 alilitaka Jeshi la Polisi lichukue hatua stahiki za kisheria na kuhakikisha wahalifu wote waliotenda kitendo hicho na waliowezesha wanakamatwa na kufikishwa mahakamani ili haki itendeke.
Pia Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kupitia Mkurugenzi wake, Anna Henga, kilisema kituo hicho kama sehemu ya jamii kimehuzunishwa na ukatili huo na kutaka wahusika wote watano na aliyewatuma kulingana na maelezo, wakamatwe na kufikishwa mbele ya mkono wa sheria.
Hatua zilizochukuliwa
Agosti 4, 2024 Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime alitoa taarifa kwa umma kuzungumzia tukio hilo, akieleza wameanza kulifanyia kazi na kulilaani kwa kuwa halikubaliki na ni kinyume cha sheria, maadili ya Mtanzania na haki za binadamu.
Agosti 5, 2024, Mwananchi lilimtafuta Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni kujua ni nini kinaendelea juu ya watuhumiwa hao, akasema vyombo vinavyohusika vinaendelea kulishughulikia suala hilo kwa mujibu wa sheria.