Chalamila aagiza Takukuru kuchunguza majina yaliyopitishwa Kariakoo

Mkuu wa Mkoa, Albert Chalamila akizungumza na watumishi na uongozi wa Shirika la Masoko Kariakoo katika Ofisi ya Shirika la Masoko Magogoni.
Dar es Salaam. Mvutano baina ya wafanyabiashara wa Soko la Kariakoo na uongozi wa soko hilo, umechukua sura mpya baada ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila kufikisha suala hilo kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).
Takukuru wamepewa jukumu la kuchunguza majina 891 yaliyopitishwa na Shirika la Masoko Kariakoo ya watu wanaotakiwa kurejea katika soko hilo kati ya 1891 waliokuwapo awali kabla ya kuteketea Julai 2021.
Sambamba na hilo, ametaka kuondolewa mara moja kwenye mfumo majina hayo mpaka pale vyombo vya uchunguzi vitakapoyapitia upya na kujiridhisha vigezo vilivyotumiwa kuwapata.
Chalamila ametangaza uamuzi huo leo Ijumaa, Julai 12, 2024 katika mkutano wake na viongozi wa shirika hilo, ikiwa ni saa chache kupita tangu alipofanya kikao na wafanyabiashara zaidi ya 800 wanaodai kukatwa majina yao kwenye orodha hiyo.
Soko hilo liliungua Julai mwaka 2021 na kuteketeza karibu mali zote za wafanyabiashara ambapo Serikali iliamua kulikarabati kwa kutenga Sh28 bilioni na kuwahamishia kwa muda katika masomo ya Kisutu na Machinga Complex.
Tayari soko hilo ujenzi wake umekamilika kwa asilimia 93 na mwezi ujao linatarajiwa kuzinduliwa na Rais Samia Suluhu Hassan.
Chalamila alitangaza uamuzi huo baada ya awali kuwaeleza wafanyabiashara hao kuwa kuwa ambao wamekatwa wataanza kuhakikiwa kuanzia Jumatatu ijayo.
Chalamila alikutana nao baada ya jana Alhamisi kuandamana kutoka viwanja vya Mnazi Mmoja kwenda Ofisi za CCM Lumumba kuwasilisha kilio chao kwa chama tawala. Hata hivyo, amewaeleza walikosea kufanya hivyo.
Baada ya kumalia kuzungumza nao ofisini kwake, alikwenda kukutana na viongozi wa shirika hilo akiwa na Katibu Tawala wa Mkoa, Dk Toba Nguvila na uongozi wa Takukuru Dar es Salaam, huku Chalamila akionekana mwenye hasira wakati akizungumza.
Amesema wamegundua malalamiko ya wafanyabiashara yana ukweli ndani yake, ikiwemo uhakiki huo kuhusishwa na vitendo vya rushwa.
Kutokana na hilo alisema anaipa kazi Takukuru na vyombo vingine vya uchunguzi kupitia majina hayo kujiridhisha na baada ya hapo mkeka mwingine wa majina ya watakaotakiwa kurejea, utaunganishwa na walioachwa katika orodha ya mwanzo.
“Naagiza majina hayo yaondolewe mara moja na kama itadhihirika majina hayo ni halali kuwepo yatabaki mpaka pale yatakapounganishwa na mengine, ambayo bado hayajahakikiwa sawasawa na baadaye majina hayo yatawasilishwa kwenye ngazi husika,” amesema.
Ameongeza:“Hii ni baada pia ya ofisi ya Rais kujiridhidha, ofisi ya Waziri wa Tamisemi na ofisi ya Takukuru kujiridhisha ndio yataruhusiwa kuwekwa tena mtandaoni.’’
Aidha, kwa ajili ya kuwapata wafanyabiashara wengine watakaoingia sokoni hapo ukiacha wale waliokuwepo awali, Chalamila ametaka kuwepo kwa uwazi kuhusu utaratibu huo ikiwemo kutangazwa na kufahamika kabla ya Watanzania kuomba.
Jingine amesema alilolibaini katika malalamiko ya wafanyabiashara ambayo mengi yamejikita kwenye rushwa, kumemfanya ajiulize maswali mengi kuhusu umadhubuti wa bodi ya shirika,mtendaji wake na umadhubuti wa wakuu wa idara na wale wote wanaofanya uamuzi katika shirika hilo.
“Kwa mantiki hiyo, natoa wiki mbili bodi ijitazame, ijihakiki na mtendaji wa Karikaoo pamoja na wakuu wa idara zote ili malalamiko yote haya yanayohusu rushwa yaweze kutatuliwa na katika hili namkabidhi Mkuu wa Takukuru Dar es Salaam kuichimba ofisi hiyo na kunipa taarifa kabla ya Agosti,” amesema.
Kuhusu uhakiki unaoenda kufanyika, amesema wanaenda kuwashirikisha kwa karibu viongozi wa wafanyabaishara, ili kutoonewa kwa upande wowote.
Pia kwa upande wa watumishi wa shirika, ametaka kupitiwa upya kwa nyaraka za umri wao wa kukaa katika shirika hilo, ufanisi wao ili ikiwezekana kuhamishwa kwa atakayebainika kuhusika kufanya vitendo vya udanganyifua na taarifa yake aipate ndani ya wiki moja.
Wakitoa maoni yao kwa nyakati tofauti kuhusu uamuzi huo, wafanyabiashara hao wamesema kushirikishwa kwa viongozi wao ndio walichokuwa wanakitaka tangu mwanzo lakini kwa bahati mbaya walipuuzwa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa soko dogo, Minja Msuya, amesema ushirikiano huo ungefanywa tangu mwanzo changamoto zilizotokea zisingekuwapo.
Kuhusu ni muda gani wanaweza kumaliza kuhakikiana, Msuya, amesema haitachukua hata siku tatu kwa kuwa wanajuana wote na kueleza muda wa kufunguliwa soko mwezi ujao wanaamini hautaathiriwa na shughuli hiyo ya uhakiki.
Naye Naye Rukia Milambo, amesema awali waliogopa kwa kuwa Mkuu wa Mkoa alianza na mikwara na hakutegemea wangefikia pazuri kiasi hicho.