Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Chadema yatoa masharti haya  kushiriki mdahalo na Makonda

Mkurugenzi wa Mawasiliano, Itifaki na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema

Muktasari:

  • Masharti hayo yametolewa kujibu kile kilichoelezwa jana Jumapili, Januari 14, 2024 na Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Paul Makonda akiwa Unguja Visiwani Zanzibar, akitaka kufanyike mdahalo wa wazi kati yake  na viongozi wa Chadema ili Watanzania wachague ikiwa wataendelea na maandamano au kuchagua maridhiano.

Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimetoa masharti matano kwa Chama cha Mapinduzi (CCM) ili kiridhie kushiriki mdahalo.

Miongoni mwa masharti hayo, Serikali iondoe kwanza miswada mitatu mibovu bungeni inayohusu sheria za uchaguzi, Serikali ianzishe mara moja mchakato wa marekebisho ya Katiba ya Mwaka 1977 na Serikali iwasilishe bungeni muswada wa Sheria ya kukwamua mchakato wa Katiba mpya ukiwa na jibu la  lini nchi itapata Katiba mpya.

Masharti hayo yametolewa kujibu kile kilichoelezwa jana Jumapili, Januari 14, 2024 na Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Paul Makonda akiwa Unguja Visiwani Zanzibar, akitaka kufanyike mdahalo wa wazi kati yake  na viongozi wa Chadema ili Watanzania wachague ikiwa wataendelea na maandamano au kuchagua maridhiano.

Katika kujenga msingi wa hoja yake ya mdahalo ambayo amekuwa akiirudia mara kwa mara, Makonda alisema  kila unapoanzishwa mchakato wa kuleta maendeleo ya pamoja,  Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amekuwa wa kwanza kuvuruga huku akikumbushia namna walivyoingia kwenye mchakato wa kubadilisha baadhi ya vifungu vya sheria lakini Mbowe na wenzake walikataa.

“Alikimbia Bunge la Katiba na kuanzisha vuguvugu huko mtaani kila alichosema Mbowe,   Rais Samia Suluhu Hassan aliridhia na wakati mwingine alikubali kukizana na wana-CCM wenzake ili kujenga mustakabali wa Taifa moja lisilobaguana na vyama,  lakini matokeo yake Mbowe anatangaza kuachana na mchakato huu wenye dhamira njema na kukimbilia mtaani kuhamasisha maandamano,” alisema Makonda. 


Chadema na mdahalo

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa umma na Chadema, kupitia kwa Mkurugenzi wa Mawasiliano, Itifaki na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema amesema chama chao kipo tayari kushiriki na hakijawahi kukimbia midahalo.

“Mdahalo unaweza kufanyika katika masuala yafuatayo ambayo tumeweka msimamo wetu wazi ili yatekelezwe na Serikali. Kwanza, iondoe miswada mitatu mibovu bungeni, ili kuwezesha wadau mbalimbali tukae kwenye mdahalo wa kujadili maudhui ya miswada ya sheria za uchaguzi, Tume ya Uchaguzi na sheria zinazohusu masuala ya Vyama vya Siasa,” amesema

Masharti mengine yaliyobainishwa na Mrema ni Serikali iwasilishe bungeni muswada wa sheria ya kusimamia Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na uchaguzi huo usimamiwe na Tume ya Uchaguzi badala ya Tamisemi.

 Halikadhalika chama hicho kimeeleza baada ya kukamilisha hayo, wadau wataweza kukaa kwenye mdahalo ili kuishauri Serikali jinsi ya kuweza kupunguza ukali wa gharama za maisha na kuonyesha kodi na tozo zipi zipunguzwe,anasa gani ziondolewe na mkakati mzima wa kupunguza ukali wa gharama. 

“Miswada hii iliyopelekwa bungeni, Serikali  imepuuza maoni ya wananchi, viongozi wa dini, wadau na vyama vya siasa, ripoti za waangalizi wa uchaguzi wa kimataifa na ndani, taarifa ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya mwaka 2020 pamoja na amri za Mahakama ya Afrika na Afrika Mashariki kuhusu maeneo mahususi ya kuboresha mifumo ya chaguzi na sheria ya vyama,” amesema.