Prime
CAG: Vituo vingi vya mabasi vina uhaba wa vyoo, Taboa yaunga mkono

Muktasari:
- Changamoto zingine zinazovikabili vituo vya mabasi ni ukosefu wa sehemu za abiria kujikinga jua na mvua, barabara zisizo na vibamba (pavements), uhaba wa vyoo na ukosefu wa walinzi.
Dar es Salaam. Ukaguzi wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), umebaini vituo vingi vya mabasi nchini vinakabiliwa na changamoto za miundombinu ikiwamo uhaba wa vyoo, hali inayosababisha mazingira ya maeneo hayo kutokuwa rafiki kwa watumiaji.
Changamoto zingine ni ukosefu wa sehemu za abiria kujikinga jua na mvua, barabara zisizo na vibamba (pavements) na ukosefu wa walinzi.
CAG, Charles Kichere amebainisha hayo katika ripoti Kuu ya Mwaka wa Ukaguzi wa Tamisemi ya Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa mwaka fedha 2023/24 aliyoiwasilisha bungeni Aprili 16, 2025.
Kichere amesema hatua hiyo inasababisha uwekezaji uliofanywa na Serikali katika vituo vya mabasi kuwa katika hatari ya kutoendeshwa kwa ufanisi na upotevu wa mapato.
“Mchanganyiko wa changamoto hizo unaonesha haja ya usimamizi thabiti, mifumo madhubuti ya uendeshaji, na uchukuaji wa hatua stahiki ili kuhakikisha matumizi sahihi ya uwekezaji wa fedha umma katika vituo vya mabasi,” amesema Kichere.
Amesema ukaguzi wa uendeshaji wa vituo vya mabasi ulibaini kwa kiasi kikubwa kutokutumika ipasavyo na upungufu katika uendeshaji wa vituo, jambo linalosababisha upotevu wa mapato na utoaji wa huduma hafifu.
“Ukaguzi umebaini vituo vya mabasi katika halmashauri nne havifanyi kazi ipasavyo, huku idadi ndogo ya mabasi ikivitumia kutokana na ukosefu wa mifumo madhubuti ya ufuatiliaji,” amesema.
Kichere amesema uwekezaji wa fedha za umma katika vituo vya mabasi unapaswa kusimamiwa ipasavyo, kuendeshwa na kufanya kazi kikamilifu ili kuboresha utoaji wa huduma, kuongeza makusanyo ya mapato, na kuhakikisha thamani ya fedha inapatikana.
Kutokana na hali hiyo, CAG amependekeza Tamisemi kusimamia utekelezaji wa miongozo ya uendeshaji ili kuhakikisha vituo vya mabasi vinatumika kikamilifu kwa kuweka mifumo ya ufuatiliaji wa mabasi yanayoingia na kutoka vituoni, kuboresha miundombinu ya sehemu za abiria kukaa na barabara za vituo hivyo.
“Mamlaka za serikali za mitaa husika zinapaswa kuimarisha usalama ili kulinda mapato na kuzuia uharibifu wa miundombinu na wizi. Naishauri Serikali, kupitia Tamisemi na mamlaka nyingine husika za usafiri na afya kuwezesha na kusimamia uwekaji wa mazingira rafiki katika vituo vya mabasi.
Kwa mujibu wa CAG, hatua hiyo haitaboresha tu utoaji wa huduma bali pia itaimarisha ukusanyaji.
Taboa yaungana na CAG
Kutokana na ripoti hiyo, Mwananchi limezungumza na Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa), ambacho kimesema kilichoelezwa CAG ndiyo hali halisi iliyopo katika vituo vya mabasi vilivyopo katika maeneo mbalimbali nchini.
“CAG hajakosea yupo sahihi, ndio hali iliyopo kwenye vituo vya mabasi, kinachookana watendaji wapo ‘busy’ kukusanya ushuru au tozo badala ya kutatua changamoto hizo,” amesema Priscus John ambaye ni Katibu Mkuu wa Taboa.
John ameiambia Mwananchi kumekuwa na changamoto ya ubovu wa barabara zilizopo katika stendi hali inayosababisha mabasi kuharibika.
“Mfano stendi ya Magufuli ukifika fremu mbele zinatoa huduma ya maduka ya vifaa vya magari au baa, nilitegemea ziwe ofisi za abiria ili kupata tiketi lakini huduma hiyo inatolewa ghorofa ya nne,” amesema.
“Hali hii inasababisha kuwepo kwa mazingira ya ulanguzi wa tiketi na uwepo wa wapiga debe, halafu wanasema wamiliki wanawaweka wapiga debe,” amesema John.
Kutokana na hilo, John amesema ndio maana wamiliki wengi wameamua kuingia gharama ya kukodi fremu ili kuweka stendi binafsi kuepusha adha ya abiria wao kusumbuliwa na wapiga debe.
Amesema changamoto zilizoainishwa na CAG ndizo sababu baadhi ya mabasi kutoingia kwenye vituo, huku akisema ana wasiwasi kuhusu risiti za huduma zinazotolewa ikiwemo ya maliwato kama zina muunganiko na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
“Sasa kwa mazingira haya yaliyoelezwa kwenye ripoti ya CAG, lazima mabasi yasite kuingia vituoni. Serikali iboreshe mazingira, ukitaka maziwa kwa ng’ombe wako lazima umrishe vizuri,”amesema John.
Abaini miradi kutekelezwa miaka mitatu hadi 25
Katika ukaguzi huo, CAG amebaini miradi yenye thamani ya Sh14.30 bilioni ilitekelezwa na mamlaka za serikali za mitaa 13 kwa vipindi kati ya miaka mitatu hadi miaka 25 ikiwa katika hatua mbalimbali za ukamilishaji.
“Utelekezaji wa miradi hii umetokana na ukosefu wa bajeti za kutosha na kutoweka kipaumbele cha kukamilisha miradi ya awali, hasa iliyoanzishwa kupitia michango ya jamii,” amesema.
“Kutelekeza miradi ya maendeleo baada ya uwekezaji mkubwa wa fedha husababisha upotevu wa rasilimali na kushindwa kufikia malengo yaliyokusudiwa,”amesema Kichere.
CAG amependekeza Tamisemi kuhakikisha mamlaka ya serikali za mitaa zinatenga upya bajeti ya miradi iliyoachwa kwa muda mrefu ili kuhakikisha inakamilika na kufanikisha malengo yake.
Pia, amezishauri mamlaka za serikali za mitaa kuweka kipaumbele katika upangaji wa fedha na matumizi kwa kuzingatia miradi michache inayoweza kukamilika.