Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

CAG: Tanzania haijapewa ardhi Uturuki, Kuwait

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere akizungumza na waandishi wa habari leo Aprili 16,2025 Dodoma. Picha na Hamis Mniha

Muktasari:

  • CAG amesema hilo ni kinyume cha utaratibu wa utoaji huduma kwa uwiano sawa (reciprocity) kidiplomasia kunahusu makubaliano baina ya nchi mbili kupeana huduma kwa uwiano usawa, kwani tayari nchi hizo zimepewa maeneo Dodoma.

Dar es salaam. Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2023/2024 imebainisha kuwa Tanzania haijapewa ardhi, Uturuki na Kuwait licha ya kutoa maeneo Dodoma.

Ripoti hiyo iliyowekwa wazi jana imeeleza kuwa Serikali ya Tanzania iliipatia Jamhuri ya Uturuki ekari tano za ardhi katika eneo la Mtumba-Dodoma lililotengwa kwa ajili ya majengo ya balozi mbalimbali, lakini Ubalozi wa Tanzania haujapatiwa ardhi nchini Uturuki licha ya barua za kukumbusha zilizotumwa tangu Machi na Novemba 2024.

“Vilevile, licha ya nchi ya Kuwait kupatiwa ardhi na Serikali ya Tanzania Kiwanja Namba 61, Kitalu A, Eneo la Ihumwa, Dodoma, nilibaini kuwa Ubalozi wa Tanzania nchini humo haujapatiwa ardhi licha ya barua ya kukumbusha iliyotumwa Januari 10, 2023.

CAG amesema Ibara ya 2 ya mkataba wa Vienna wa uhusiano wa kidiplomasia wa mwaka 1961 inahitaji kuwapo kwa makubaliano baina ya nchi mbili na utoaji huduma kwa uwiano sawa (reciprocity).

Amesema kutoshughulikiwa kwa suala hili kunazorotesha utoaji wa huduma kwa uwiano usawa, uhusiano wa kidiplomasia na kunaongeza gharama za uendeshaji kwa balozi za Tanzania kwa kuendelea kukodi majengo ya ofisi na makazi.

“Ushirikiano imara wa kidiplomasia ni muhimu katika kuhakikisha masilahi ya Tanzania yanazingatiwa,” amesema.

Amependekeza kuwa Serikali, kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, iendelee kuwasiliana na mamlaka za nchi husika ikiwamo kufanya mazungumzo ya kidiplomasia ili kuharakisha utoaji wa ardhi kwa Ubalozi wa Tanzania huko Ankara na Kuwait.

Kadhalika amependekeza Serikali, ifuatilie kufutwa kwa masharti ya viza kwa Watanzania wanaoingia Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.