Bwege: Bila upinzani kuungana CCM haing’oki

Mbunge wa zamani wa Kilwa Kusini mkoani Lindi, Selemani Bungara maarufu ‘Bwege’
Muktasari:
- Kwa takriban miaka 30 baada ya kurejea kwa mfumo wa vyama vingi bado CCM kimeendelea kunyakua ushindi na vyama vya upinzani kudhoofika
Lindi. Tangu kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992 na kushuhudia uchaguzi mkuu wa kwanza uliovihusisha vyama hivyo mwaka 1995, upinzani umeshindwa kutimiza dhamira yao ya kukiondoa Chama cha Mapinduzi (CCM), madarakani.
Hata hivyo kumekuwa na panda shuka kwa wapinzani, uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 ndio unaoweza kupigiwa mfano wa mafanikio bora baada ya kujinyakulia viti vingi vya ubunge, udiwani na kura nyingi za urais.
Aliyekuwa mgombea wa urais wa Chadema, Edward Lowassa ambaye alikuwa akiungwa mkono na vyama vinne vya upinzani (CUF, NCCR-Mageuzi, NLD na Chadema) alipata kura 6,072,848 ikiwa ni asilimia 39.97 ya kura zote na Magufuli alipata kura 8,882,935 ikiwa ni asilimia 58.46.
Jina Selemani Bungara maarufu ‘Bwege’, mbunge wa zamani wa Kilwa Kusini mkoani Lindi si geni katika medani za siasa kutokana staili yake ya ufanyaji shughuli za kisiasa na namna alivyokuwa akiwasilisha hoja zake ndani ya ukumbi wa Bunge enzi hizo akiwa mwakilishi wa wananchi wa jimbo hilo.
Bwege anasema pamoja na changamoto ya Katiba, lakini ili kuiondoa CCM vyama vya upinzani vinapaswa kuungana na kuwa na lengo moja. anasema hata ikiwepo Katiba Mpya nzuri lakini kama wapinzani hawajaungana CCM haiwezi kutoka madarakani.
“Kwa jinsi ilivyo ACT inasema Chadema. Chadema nao wanaishambulia ACT au wanaisema CUF, sasa wenyewe kwa wenyewe wanagombana. Ninachoomba viongozi wakuu wa vyama upinzani makini akiwemo Mbowe (Freeman), Zitto (Kabwe), wakea chini na kutengeneza muungano,” anasema Bwege.
Bwege, aliyekuwa mbunge wa CUF kwa miaka 10 kuanzia mwaka 2010/2020 kabla ya mwaka juzi kuhamia ACT-Wazalendo, ana staili ya pekee ya kufanya siasa hasa anapozungumza na wananchi au kuchangia mijadala bungeni.
Staili yake maarufu ni ile ya kuzungumza kwa mzaha ukiwa ndio mfumo wake wa kufikisha ujumbe kuhusu ajenda zinazohusu Taifa au chama chake. Kutokana staili hiyo Bwege alijizolea umaarufu na amekuwa akifikisha ujumbe kwa urahisi huku akiwaacha hoi watu kwa vicheko wanaomsikiliza au kufuatilia hotuba zake.
Lakini, tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu uliopita ulioipa CCM viti vingi vya udiwani na ubunge, Bwege amekuwa kimya kwa sababu mbalimbali, ikiwemo kujipa muda wa kutafakari kilichotokea katika mchakato huo uliosababisha kushindwa kutetea nafasi yake.
Hivi karibuni Mwananchi lilifanya mahojiano na Bwege nyumbani kwake, Kilwa mkoani Lindi. Mahojiano hayo yalilenga masuala mbalimbali ya kitaifa, ikiwemo mwenendo wa hali ya kisiasa unaoendelea hivi sasa nchini baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kushika madaraka tangu Mei 19, 2021.
Kwa mujibu wa Bwege, mwenendo wa kisiasa ni mzuri na maridhiano yanayoendelea yanaashiria mwanga mzuri mbele ya safari.
Anasema mwenendo wa sasa unaweza ukapita hali zote zilizopita nyuma kuanzia utawala wa Awamu ya Nne wa Rais mstaafu Jakaya Kikwete.
“Kama anachokisema na kukisimamia Rais Samia na kinachosimamiwa na Watanzania kitafanyika kwa ufanisi, basi hali ya demokrasia itakuwa nzuri kuliko miaka yote kwa maoni yangu. Kwa ufupi mwelekeo ni mzuri,” anasema Bwege.
Ukimya wake
Bwege anasema amekuwa kimya kwa sababu mbalimbali, ikiwemo kujiuguza kutokana na maradhi yanayomsumbua muda mrefu na pia alikuwa akipumzika masuala ya siasa ili atafakari kilichotokea katika uchaguzi uliopita kabla ya kusonga mbele.
“Kwa namna siasa ilipofikia miaka sita iliyopita, ilikuwa ni lazima ufikirie na kujipanga utaanzia wapi. Jambo kubwa kama lile likitokea lazima ukae kwa kutulia, lakini sikukata tamaa. Katika maisha yangu sikati tamaa katika kupambania haki na demokrasia na uhuru,” anasema mwanasiasa huyo.
“Niliamua kuwa kimya ili kuangalia mazingira yakoje, ila nashukuru Mungu hali ya sasa sio mbaya inaridhisha. Sasa unafungua tawi na kufanya mkutano wa ndani bila kusumbuliwa na polisi. Tunaomba kwa Mungu tupate mikutano ya hadhara kabisa.”
Bwege anasema endapo Rais Samia atakubali kuwepo kwa Tume Huru ya Uchaguzi, Katiba mpya na utawala wa sheria atakuwa kiongozi wa mfano wa Tanzania, Afrika na duniani kuweka rekodi na historia ya kuimarisha demokrasia.
“Namuomba Rais Samia athubutu na awe jasiri kwa sababu haya anayoyafanya kuna baadhi ya watu ndani ya CCM hawayapendi. Sasa kama hajathubutu na kuwa jasiri ataishia njiani. Kikubwa asimamie haki asisikilize maneno ya watu wengine, naamini Mungu atamuongoza,” anasema Bwege.
Makongamano ACT
Bwege anasema ACT-Wazalendo ni chama kinachokua kwa kasi na kina maono ya mbali kwa sababu kinakosoa na kutoa njia mbadala na mwongozo wa nini kifanyike ili kurekebisha jambo fulani.
“Kwa siasa za Tanzania ACT ndio chama kiongozi cha siasa kutokana na aina za siasa tunazozifanya. Upinzani sio kupinga kila kitu, unapinga mabaya na unaelekeza mazuri. Likiwa zuri pongeza, baya kosoa na kutoa njia mbadala,” anasema.
Kwa nyakati tofauti chama hicho kimekuwa kikifanya makongamano kuhusu Tume Huru ya Uchaguzi kuelekea kupata Katiba Mpya katika maeneo ya mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza na Ruvuma na lengo ni kuhakikisha mchakato wa Tume Huru ya Uchaguzi kuelekea Katiba Mpya unafanikiwa.
Kuhusu Tanzania kufikisha miaka 30 ya mfumo wa vyama vingi, Bwege anasema Taifa halijapiga hatua, badala yake limerudi nyuma katika kipindi cha miaka sita iliyopita. Hata hivyo, hivi sasa kuna mwanga mkubwa kwa vyama vya siasa kufanya shughuli zao.
Jambo asilolisahau
Yapo mambo mengi ambayo mbunge huyo wa zamani huyakumbuka kama matukio yaliyomsisimua, lakini lipo moja ambalo kamwe hawezi kulisahau maishani mwake.
“Mwaka 1994 nilikamatwa na kufungwa jela kwa miezi sita bila sababu. Sitasahau kwa sababu zilifanyika fitina kwa kesi ya uongo niliyopewa, lakini nilipambana na bahati nzuri nilishinda kesi ile. Hili sitalisahau katika harakati za siasa,” anasema Bwege.
“Lakini jambo ninalolifurahia katika maisha ya siasa ni pamoja na wananchi wa Kilwa kunielewa na wao kujitambua ni watu wa aina gani katika kusimamia haki za msingi za Watanzania. Kazi hii nimeifanya na watu wa Kilwa wameelimika na kujitambua.”
Sirudi CUF
Bwege anasema licha ya kudumu kwa muda mrefu ndani ya CUF, hawezi kurejea tena baada ya kuhama mwaka 2020 kwani kabla ya kuondoka aliweka wazi kwamba hawezi kufanya kazi na Profesa Ibrahim Lipumba, ambaye ni mwenyekiti wa chama hicho.
“Sasa kabla sijahama nilitamka maneno, leo nipo ACT-Wazalendo ndio nitarudi? Siwezi kurudi CUF hata iweje. Narudi kufanya nini au kwa lipi? Sikatai nilikuwa nakipenda, lakini mwenendo wake haukuwa mzuri, ikiwemo kumfukuza Maalim Seif Sharrif Hamad (sasa marehemu, aliyekuwa katibu mkuu wa CUF wakati huo),” anasema.
“Nipo hapa ACT, nikiona kinakwenda kinyume na haki za wananchi nitaondoka, kwa sababu napenda na kusimamia haki za wananchi.”
Uchaguzi wa 2020
Bwege anadai kuwa uchaguzi wa mwaka 2020 haukuwa huru wala haki kwa sababu kuna wagombea wa upinzani, akiwemo yeye waliporwa ushindi. Hata hivyo, Bwege anadai dalili za kuharibika kwa uchaguzi huo zilianza kuonekana mapema katika uchaguzi wa Serikali za mitaa 2019.
“Mchakato wa uchaguzi mkuu ulianza vizuri, lakini mwisho kilichojitokeza Watanzania mashahidi. Ndio maana watu wengi walivunjika moyo kisiasa kwa kilichojitokeza,” anasema Bwege.