Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Bunge laibana Serikali magari ya zimamoto

Muktasari:

  • Wabunge wataka Serikali ibebe jukumu kununua magari ya zimamoto.

Dodoma. Bunge limeazimia Serikali ipeleke bungeni muswada wa sheria kuweka utaratibu wa halmashauri kutenga fedha katika bajeti zake kwa ajili ya kununua magari ya zimamoto, matengenezo ya magari hayo na vifaa vya zimamoto na uokoaji.

Baada ya hoja kujadiliwa, Spika Dk Tulia Ackson alilihoji Bunge ambalo liliipitisha kwa asilimia 100.

Azimio hilo linatokana na hoja binafsi iliyowasilishwa bungeni Juni 6, 2024 na mbunge wa Moshi Mjini, Priscus Tarimo aliyelitaka Bunge kuazimia kuwa, Serikali ipeleke bungeni muswada wa sheria kuweka utaratibu kuziwezesha halmashauri za miji na wilaya, kuingia makubaliano na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kununua magari na vifaa vya uokoaji.

“Serikali ilete bungeni muswada wa sheria utakaoweka utaratibu wa utekelezaji wa Sera ya Huduma kwa Jamii (CSR) kuwezesha miradi mikubwa ya kimkakati kuweka huduma za zimamoto na uokoaji,” amesema Tarimo.

Pia ametaka Bunge kuazimia Serikali kupeleleka muswada wa sheria utakaoweka utaratibu wa kuwezesha vituo vya kuchota maji kwa magari ya zimamoto katika miradi yote ya maji na kuingia makubaliano ya ushirikiano kati ya mamlaka za maji nchini na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, katika uwekaji na ukarabati wa vituo hivyo.

Mbali na hayo ametaka Bunge kuazimia Serikali kuweka utaratibu wa kuwezesha upatikanaji wa ajira kwa jeshi hilo ili kuajiri askari wengi kila mwaka kukidhi shughuli za uokoaji na kupambana na majanga.


Michango ya wabunge

Mbunge wa Korogwe Mjini, Dk Alfred Kimea amesema haoni kwamba ni busara kuziongezea halmashauri jukumu hilo.

“Kama kuna halmashauri zina uwezo wa kununua magari haya basi zifanye hivyo, kama kuna watu binafsi wana uwezo wa kufanya hivyo wafanye kazi hiyo kuliko kuiongezea halmashauri jukumu hilo zito,” amesema akitaka Serikali kuliongezea uwezo jeshi hilo wa kupambana na matukio ya moto.

Hoja hiyo iliungwa mkono na mbuge wa Viti Maalumu, Felista Njau aliyesema isiwe lazima kwa kila halmashauri kutenga bajeti za ununuzi wa magari na vifaa kwa sababu zipo ambazo ziko hoi.

Ametaka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kushirikiana ili kukitokea janga la moto magari yaweze kufika.

Constastine Kanyasu (Geita Mjini) ametaka Serikali kuendelea na jukumu hilo akisema zipo halmashauri makusanyo yake ni Sh2 bilioni na gari moja la zimamoto linagharimu Sh1 bilioni.

Kilumbe Ng’enda (Kigoma Mjini), amesema haungi mkono halmashauri kulazimishwa kununua magari hayo kwa kuwa hata ya taka hakuna, akieleza maeneo mengi ya kuchotea maji yamejengewa majengo badala ya kuachwa wazi.

Mbunge wa Nkasi Kusini, Vincent Mbogo ametaka Jeshi hilo kuanzisha kitengo cha zimamoto jamii kwa sababu askari wa jeshi hilo ni wachache.

Mbogo ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, amesema jeshi hilo awali lilikuwa halipatiwi fedha lakini sasa limeanza kupewa.

Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Aida Khenan amesema, “Hakuna haki bila wajibu, ili zimamoto walaumiwe ni lazima askari wawepo, viwepo na vitendea kazi lakini Serikali iwape fedha,” amasema.


Majibu ya Serikali

Naibu Waziri wa Fedha, Hamad Chande alimpa taarifa mbunge huyo kuwa Serikali imeshapeleka Dola za Marekani milioni 100 Mei mwaka huu kwa ajili ya ununuzi wa magari, helikopta na boti vyote vya  Jeshi hilo.

Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Jumanne Sagini amesema zaidi ya watumishi 800 wameajiriwa katika kipindi cha miaka mitatu ya Rais Samia Suluhu Hassan.

Amesema mwaka huu zimamoto wamepewa fedha za kununua magari yatakayopelekwa kwenye taasisi zote za Serikali 150 ikiwemo mikoa na halmashauri zote nchini.

Akimpa taarifa Sagini, mbunge wa Handeni Mjini, Reuben Kwagilwa amesema zilitengwa Sh3 bilioni mwaka 2023/24 kwa ajili ya kununua magari matano ya zimamoto lakini hayajanunuliwa.

Oktoba 2, 2023 Waziri wa Mambo ya Ndani alikaririwa na vyombo vya habari akisema Serikali inakwenda kufanya uwekezaji mkubwa katika Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kwa kununua magari ya zimamoto yasiyopungua 150, boti maalumu za uokozi zisizopungua 25, gari za wagonjwa zisizopungua 20, na helikopta, lengo likiwa kuokoa mali na maisha ya Watanzania yanapotokea majanga

Aprili 26, 2023 wakati wa uzinduzi wa majengo ya zimamoto katika vituo vya Nzuguni na Buigiri jijini Dodoma, Kamishina Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, John Masunga alisema wanakabiliwa na uhaba wa vitendea kazi, ikiwemo magari kuwa chakavu.

Pia alisema magari ya ngazi kwa ajili ya kuzima moto kwenye majengo marefu yanatakiwa tisa lakini Tanzania ina moja la aina hiyo ambalo lipo Dar es Salaam.

Alizungumzia pia maeneo ya kujazia maji akisema vinahitajika vituo 285,000 nchi nzima lakini viko 2,348 na kati ya hivyo vinavyofanya kazi ni 1,628.