Bunge la EALA kujadili bajeti ya Mwaka wa fedha 2026/2027
Spika wa Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki (Eala), Joseph Ntakirutimana akizungumza katika kikao cha bunge hilo hivi karibuni.
Muktasari:
- Mkutano huu wa tatu, kikao cha nne cha Bunge la tano la kikanda, unatajwa kuwa na umuhimu mkubwa kiuchumi na kisheria kwa nchi wanachama, kwasababu utatoa mwelekeo wa kibajeti na kifedha kwa mwaka ujao wa fedha
Arusha. Bunge la Afrika Mashariki (EALA) linatarajiwa kuendelea na vikao vyake kesho, Alhamisi Juni 18, 2026, katika Makao Makuu ya Jumuia ya Afrika Mashariki (EAC) jijini Arusha, ambapo ajenda kuu itakuwa mjadala wa Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2026/2027.
Mkutano huo wa tatu wa kikao cha nne cha Bunge la Tano la Kikanda, unatajwa kuwa na umuhimu mkubwa kiuchumi na kisheria kwa nchi wanachama wa EAC, kwa kuwa utatoa mwelekeo wa sera za bajeti na matumizi ya fedha kwa mwaka ujao wa fedha. Vikao hivyo vinatarajiwa kuendelea hadi Juni 25, 2026.
Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa leo, Juni 17, 2026, moja ya matukio muhimu yanayotarajiwa katika kikao hicho ni kuanza rasmi kwa majukumu ya wabunge wapya kutoka Jamhuri ya Shirikisho ya Somalia, ambayo ni mwanachama mpya zaidi wa Jumuia ya Afrika Mashariki.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa, mbali na Somalia, wabunge wapya waliochaguliwa hivi karibuni kuiwakilisha Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika EALA pia watapatiwa semina elekezi ya kuwajengea uwezo kuhusu majukumu yao. Semina hiyo imepangwa kufanyika Jumamosi, Juni 20, 2026.
“Hatua hii itasaidia kujaza nafasi zilizokuwa wazi na kuleta nguvu mpya katika kuendeleza ajenda ya mtangamano wa kikanda,” imeeleza taarifa hiyo.
Kwa upande wa shughuli za kisheria na kibunge, EALA linatarajiwa kujadili ajenda mbalimbali muhimu zinazohusu usimamizi wa fedha na utendaji wa taasisi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Miongoni mwa ajenda hizo ni uwasilishaji wa Hotuba ya Bajeti ya EAC kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027, ambapo wabunge watajadili ripoti ya Kamati ya Masuala ya Jumla kuhusu makadirio ya bajeti hiyo pamoja na bajeti ya ziada.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, James Ole Millya akizungumza kwenye kikao cha Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki (Eala) hivi karibuni.
Aidha, Bunge litasoma kwa mara ya pili na ya tatu miswada miwili muhimu ambayo ni Mswada wa Ziada wa EAC wa mwaka 2026 na Mswada wa Matumizi ya Fedha wa EAC wa mwaka 2026.
Katika hatua nyingine, Kamati ya Hesabu ya Bunge hilo itawasilisha ripoti ya ukaguzi wa hesabu za EAC kwa mwaka wa fedha ulioishia Juni 30, 2023. Ripoti hiyo iliwasilishwa Desemba 3, 2025 na imekuwa ikisubiri mjadala wa wabunge.
Pia kutakuwa na mjadala kuhusu maendeleo na utendaji wa Vituo vya Mpaka vya Pamoja (OSBP), ukilenga kutathmini mchango wake katika kurahisisha biashara ya mipakani na kuimarisha mtiririko wa bidhaa na huduma ndani ya ukanda wa Afrika Mashariki.
EALA limeeleza kuwa kikao hicho kinafanyika katika kipindi ambacho nchi wanachama zinaendelea kusisitiza umuhimu wa kuondoa vikwazo vya biashara, kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na kuongeza kasi ya utekelezaji wa malengo ya mtangamano wa kikanda.
Wabunge wanatarajiwa kukamilisha shughuli zote zilizopangwa ifikapo Juni 26, 2026.