Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Brela yawafunda maofisa biashara 569

Katibu Tawala Mkoa wa Mara,  Robert Msalika akifunga mafunzo kwa maofisa biashara kutoka halmashauri za mikoa 10 yaliyofanyika mjini Musoma kwa siku tatu. Picha na Beldina Nyakeke

Muktasari:

Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela) imewafunda maofisa biashara 569 kuhusu Sheria ya Biashara na Leseni ya mwaka 1972.

Musoma. Maofisa biashara 569 kati ya 682 waliopo katika mikoa na halmashauri zote nchini wamefundwa na kujengewa uelewa kuhusu sheria ya Biashara na Leseni ya mwaka 1972.

Mafunzo hayo yametolewa na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni Nchini (Brela) kwa awamu tofauti kati ya mwaka 2022 na mwaka huu huku wengine waliosalia nao wakitarajiwa kupata mafunzo hayo.

Akizungumza leo Jumatano Juni 28, 2023 wakati wa kuhitimisha mafunzo hayo kwa maofisa biashara kutoka halmashauri za mikoa kumi yaliyofanyika siku tatu mjini Musoma, Kaimu Mkuu wa Sehemu ya Leseni za Biashara kutoka Brela, Tawi Kilumile amesema lengo ni kuboresha utendaji kazi wa mofisa hao.

"Sheria hii ni ya miaka mingi na imefanyiwa marekebisho mara kadhaa sasa tulibaini kuwa kuna chagamoto wanazokutana nazo hawa maofisa biashara na kupelekea kushindwa kutimiza wajibu wao ipasavyo,"amesema

Amesema mafunzo hayo ni moja ya mikakati ya Brela katika kufanikisha malengo ya Serikali ya kukuza sekta ya biashara ili kupanua wigo wa ukuaji wa uchumi kwa manufaa ya wananchi na Taifa kwa ujumla.

Akifunga mafunzo hayo, Katibu Tawala Mkoa wa Mara, Robert Msalika amewataka maofisa hao kuhakikisha wanapunguza kero wanazokutana nazo wafanyabiashara ili kujenga mazingira wezeshi ya kufanya biashara na uwekezaji nchini.

"Hakuna sababu ya kusubiri hadi wafanyabiashara waanze kugoma, hakikisheni mnakuwa sehemu  ya kuondoa kero za wafanyabiashara na hii itasaidia katika kuboresha na kukuza biashara zao na hatimaye kuongeza pato la mmoja mmoja na Serikali pia," amesema

Amesema ili serikali iweze kutimiza majukumu yake hasa ya kuleta maendeleo kwa wananchi, inahitaji kuwa na pato la uhakika na biashara ni sehemu ya chanzo cha mapato hayo na kwamba endapo wafanyabiashara watakuwa na mazingira mazuri ya biashara Serikali pia itakuwa na wigo mpana wa kukusanya kodi na tozo zilizopo kwa mujibu sheria.

Amewakumbusha kujiepusha na vitendo vya kuomba na kupokea rushwa akidai kuwa, licha ya vitendo hivyo kuwa ni kinyume cha maadili ya utumishi lakini pia ni fedheha kwao.

Msalika amewataka maofisa hao kuwa marafiki na walezi wa wafanyabiashara hatua ambayo itasaidia ukuaji na uendelevu wa biashara nchini.

Akizungumza kwa niaba ya washiriki, Ofisa Biashara kutoka Mkoa wa Geita,  Charles Chacha amesema mafunzo hayo yamekuja muda muafaka hasa katika wakati huu ambao Serikali inaboresha idara ya uwekezaji na biashara.

"Hii sheria ni ya siku nyingi kuna wengine humu walikuwa hata hawajazaliwa wakati sheria inatungwa sasa mafundisho haya yatatusaidia kujenga uelewa wa pamoja na kutimiza wajibu wetu kwa ufanisi na tija,”amesema