Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

BoT yawatangazia kiama wanaotoza asilimia 10 ya mikopo

Ofisa wa Benki Kuu akimuhudumia mwananchi aliyetembelea banda hilo katika maonyesho ya Sabasaba. Picha na Aurea Simtowe

Muktasari:

  • Wakati mikopo kausha damu ikiendelea kupigwa vita kila kona, Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imewataka wakopeshaji kutoza riba ya asilimia 3.5 kwa mwezi na si asilimia 10.

Dar es Salaam. Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imezitaka taasisi ndogo za fedha nchini kutoza riba ya asilimia 3.5 kwa mwezi kwa mikopo na watakaokiuka kuchukuliwa hatua ikiwemo kufutiwa leseni.

Maagizo hayo yamekuja baada ya kuwepo kwa matukio mengi ya taasisi hizo kutoza viwango vya hadi asilimia 10 kwa mwezi kwa kila mkopo jambo ambalo lilikuwa likiwaumiza wakopaji.

Pia, BoT kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na Jeshi la Polisi wamejipanga kuanza kuwachukulia hatua wanaodhalilisha watu waliowakopesha.

Hayo yamesemwa na Ofisa Mkuu Mwandamizi wa Benki Idara ya Usimamizi wa Mabenki kutoka BoT, Deogratias Mnyamani alipokuwa akizungumza na Mwananchi Digital, leo Jumapili, Julai 7, 2024 katika viwanja vya maonyesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba).

Mnyamani amesema BoT imekuja na kampeni iliyopewa jina la ‘Amka, usiumizwe na mikopo, chukua mikopo kwa maendeleo’ ikiwa imelenga kukomesha utozaji riba kubwa.

Amesema maagizo hayo yametolewa kwa watoa huduma ndogo za fedha pekee na si watoa huduma wengine nchini.

“Watakaokiuka maagizo haya, watapewa onyo, watanyang’anywa leseni na biashara zao zitafungwa,” amesema Mnyamani.

Hiyo ikiwa na maana kuwa, mtu anapokopa Sh1 milioni hatakiwi kulipa Sh1.1 milioni kwa mwezi na badala yake anatakiwa kulipa Sh1,035,000 pekee.

Mnyamani amesema kwa sasa wamekuwa wakitoa elimu kwa watoa huduma kuhusu riba na ukusanyaji wa mikopo hivyo watakaokiuka maagizo hayo watachukuliwa hatua.

Kanuni za huduma ndogo za fedha (Watoa huduma ndogo za fedha wasiopokea amana) ya mwaka 2019 ndiyo inayowapa mamlaka ya kufuta leseni kwa watu wanaokiuka vigezo hivyo.

Mnyamani amesema kumekuwa na matatizo mengi yanayosababishwa na riba kubwa ikiwemo kuchukua mali za wakopaji jambo ambalo linatweza utu wao.

Amesema, ili kukomesha ukopeshaji huo wa riba kubwa utafiti umebaini kuwa changamoto kubwa ni uelewa mdogo wa watu wanaokopa na wanaokopeshwa.

Amefafanua kutokana na hali hiyo wamejikita kutoa elimu kwa umma, sekta binafsi, wajasiriamali na watumishi wakiwemo walimu.

“Tunatoa elimu kwa wananchi kutokopa kwenye taasisi hizi ambazo hazina leseni ya BoT, bila kujua masharti ya mkopo na kuhakikisha wanapewa mkataba wa mkopo,” amesema Mnyamani.

Katika hatua nyingine, BoT imesema wameingia katika ushirikiano na TCRA na polisi kuwachukulia hatua za kisheria watoa huduma wanaowadhalilisha wakopaji kwa kuvunja utu wa mtu.

Hiyo ni baada ya kuwapo kwa baadhi ya wakopaji wanaowatangaza watu waliowakopesha hasa baada ya kuchelewa kulipa mikopo yao jambo linalowadhalilisha.

Baadhi ya wakopeshaji wamekuwa wakituma jumbe fupi za maandishi kwa watu wa karibu na waliowakopesha wakiwataka wawakumbushe kulipa madeni yao.

Akizungumzia hilo Laizer Msangi mkazi wa Mbagala ameitaka BoT kuwekwa wazi kwa njia ambazo watu wanaweza kuzitumia katika kuripoti watu wanaokiuka masharti na vigezo.

“Watu wanaumia mitaani, wanakopeshwa kwa riba kubwa na wengine wanatangazwa jambo ambalo linaaibisha, kwani tunapokopeshana tunakuwa wawili ila umma unakuja kujua ikiwa unadaiwa,” amesema Msangi.