Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Bosi adaiwa kuua 'house girl' wa miaka 14 kwa kichapo

Muktasari:

  • Jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro, linamsaka mkazi wa Kijiji cha Uswaa, wilayani Hai (jina linahifadhiwa kwa sababu za kiuchunguzi), akidaiwa kuhusika kifo cha msichana wake wa kazi 'house girl' ambaye ni mwenyeji wa Mkoa wa Kigoma.
no

Moshi. Jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro, linamsaka mkazi wa Kijiji cha Uswaa, wilayani Hai (jina linahifadhiwa kwa sababu za kiuchunguzi), akidaiwa kuhusika kifo cha msichana wake wa kazi 'house girl' ambaye ni mwenyeji wa Mkoa wa Kigoma.

Mtoto Zuwena Bihumo, (14) ambaye ndiye alikuwa akifanyia kazi kama mtumishi wa ndani kwa mama huyo, anadaiwa kuwa Oktoba 23, 2023; alifariki dunia baada ya kupigwa viboko na bosi wake, ambavyo vinadaiwa kumsababishia majeraha mbalimbali mwilini, ambayo ndiyo kiini cha kifo chake.

Hayo yamebainishwa leo Oktoba 26, 2023 na jeshi hilo, huku likisema kuwa baada ya kifo hicho, mwanamke huyo anadaiwa kutoroka na kwamba juhudi za kumatafuta zinaendelea, japo mumewe yuko mikononi mwa Polisi.

Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Simon Maigwa amesema: "Tunamshikilia mtuhumiwa mmoja mwanaume (Jina limehifadhiwa kwa sababu za kiuchunguzi) kwa kudaiwa kusababisha kifo cha binti aitwaye Zuwena Bitaliho Bihumo, (14) mfanyakazi wa ndani mwenyeji wa Kigoma."

"Mtuhumiwa huyo na mke wake walikuwa wakimfanyia ukatili binti huyo kwa kumchapa na kitu kinachodhaniwa ni fimbo maeneo mbalimbali ya mwili wake na kupelekea majeraha makubwa yaliyosababisha kifo chake," ameongeza Kamanda Maigwa.

Kamanda huyo amesema baada ya kutenda unyama huo, ‘waajiri’ hao walimfikisha marehemu Hospitali ya Wilaya ya Hai kama mgonjwa huku wakitambua kuwa alishafariki muda mrefu.

Wakati huo huo, Kamanda Maigwa amesema katika kipindi cha mwezi Agosti hadi Oktoba mwaka huu, Jeshi hilo, limefikisha mahakamani kesi 50, ambapo watuhumiwa 50 walipatikana na hatia na kupewa adhabu mbalimbali.

Maigwa amesema watuhumiwa hao walipewa adhabu za kutumikia vifungo tofauti tofauti na wengine kulipa faini huku magari 17 na pikipiki 22 zikitaifishwa kuwa mali ya Serikali baada ya kuthibitishwa na mahakama kuwa zilikuwa zikitumika kwenye uhalifu.

Aidha kamanda Maigwa amesema, jeshi hilo limeendesha operesheni maalum Wilaya ya Moshi na kufanikiwa kukamata watuhumiwa 84 na pikipiki 77 kwa makosa mbalimbali yakiwemo ya usalama barabarani.

Ametoa rai kwa wananchi na wazazi wanaoendelea kutenda ukatili dhidi ya watoto kuacha kwa kuwa  Polisi mkoani humo, haitasita kuwachukulia hatua kali za kisheria.