Bodaboda aliyegonga ‘mwendokasi’ afariki

Muonekano wa basi la mwendokasi lililopata ajali baada ya kugongana na bodaboda katika makutano ya mataa ya Lumumba na Barabara ya Morogoro. Picha na Hadija Jumanne.
Muktasari:
- Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji wa mkoa wa Ilala, Kamishna Msaidizi Mwandamizi, Christina Sunga, amethibitisha kutokea kwa ajali iliyohusisha basi la mwendokasi na bodaboda ambaye alifariki dunia.
Dar es Salaam. Mkazi wa Kiwalani jijini hapa, Yusuph Abeid, amefariki dunia leo, Septemba 12, 2023 baada ya kuligonga basi la mwendokasi.
Kwa mujibu wa mashuhuda ajali hiyo imehusisha basi la mwendokasi lilokuwa likitokea Kimara kwenda Kivukoni na bodaboda ambaye alikuwa akitokea barabara ya Fire katika makutano ya mataa ya Lumumba na Barabara ya Morogoro.
Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji wa mkoa wa Ilala, Kamishna Msaidizi Mwandamizi, Christina Sunga, amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo iliyosababisha kifo cha mtu mmoja na majeruhiwa mmoja.
Akizungumza na Mwananchi Digital, Kamanda Sunga amesema katika ajali hiyo majeruhi ni moja ana alipelekwa Hospitali ya Mnazi Mmoja kwa ajili ya matibabu.
"Aliyefariki ni dereva wa bodaboda ambaye mwili wake umehifadhiwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili," amesema Kamanda Sunga.
Amesema tayari basi hilo limeshatolewa eneo la ajali na kupelekwa katika yadi za kampuni hiyo kwa ajili hatua nyingine.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila wakati akizungumza na waandishi wa habari amesema taarifa kamili kuhusu ajali hiyo itatolewa na Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro, huku akisema atakuja na ajenda maalumu kuhusu watu kukatisha kwenye barabara za mwendokasi.