Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Bima yapunguza mzigo wa matibabu dawa, vipimo kilio

Muktasari:

  • Imeelezwa kuwa, licha ya wananchi kupata unafuu wa gharama za matibabu, bado wanakumbana na changamoto zinazochelewesha huduma wanazostahili kupata kupitia bima hiyo.



Dar/Mikoani. Wakati Serikali ikiendelea na utekelezaji wa Mpango wa Bima ya Afya kwa Wote, baadhi ya wananchi walioanza kunufaika na mpango huo wamesema bado wanakabiliwa na changamoto za upungufu wa dawa, baadhi ya vipimo kutokupatikana, foleni ndefu na hitilafu za mifumo ya kidijitali katika vituo vya kutolea huduma za afya.

Hata hivyo, ufuatiliaji wa Mwananchi mikoa ya Dar es Salaam, Mbeya, Kilimanjaro, Simiyu, Mara, Geita na Manyara unaonesha utekelezaji wa mpango huo umeanza kupunguza mzigo wa gharama za matibabu kwa kaya maskini na makundi maalumu.

Licha ya wananchi kupata unafuu wa gharama za matibabu, bado wanakumbana na changamoto zinazochelewesha au kupunguza ubora wa huduma wanazostahili kupata kupitia bima hiyo.

Alipoulizwa suala hilo juzi Jumapili Julai 26, 2026 Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dk Grace Magembe amesema Serikali inaendelea kuimarisha mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), upatikanaji wa dawa, vifaa tiba na rasilimali watu ili kuboresha utoaji wa huduma na kufanikisha malengo ya Bima ya Afya kwa Wote.

“Serikali inaendelea kuimarisha mifumo ya Tehama ili mifumo mbalimbali iweze kuwasiliana na kubadilishana taarifa, hatua ambayo itarahisisha upatikanaji wa huduma kwa wanufaika, kuboresha uamuzi unaotegemea takwimu na kuimarisha uendelevu wa kifedha wa skimu za bima ya afya,” amesema Dk Magembe.

Mkoani Kilimanjaro, baadhi ya wananchi kutoka Mwika, Uru Kusini na Mwanga wamesema bima hiyo imewawezesha kufika hospitalini bila hofu ya gharama, lakini wakati mwingine hukumbana na changamoto ya kukosa baadhi ya dawa na huduma.

Mkazi wa Mwika, Yasinta Molleli, amesema kabla ya kupata bima ilikuwa vigumu kwenda hospitalini kutokana na ukosefu wa fedha, lakini bado kuna nyakati baadhi ya huduma hukosekana.

“Tunashukuru kupata bima kwa sababu kabla ilikuwa changamoto kwenda hospitali bila fedha, lakini kuna wakati ukienda kituo cha afya unaambiwa baadhi ya dawa au huduma hazipo,” amesema.

Katika Mkoa wa Simiyu, wananchi kutoka wilaya za Maswa, Bariadi, Meatu, Itilima na Busega wamesema mafanikio ya mpango huo hayatapimwa tu kwa idadi ya waliosajiliwa, bali pia kwa ubora wa huduma zinazotolewa.

Mkazi wa Maswa, Ana Ngeleja amesema thamani ya bima inaonekana pale mgonjwa anapopata huduma zote bila usumbufu.

“Bima ni jambo zuri, lakini ukifika hospitali ukaambiwa dawa zimeisha au mfumo haufanyi kazi, wananchi wanakata tamaa,” amesema.

Mbali na changamoto hizo, watumishi wa afya wamesema matumizi ya mifumo ya kidijitali yamerahisisha utambuzi wa wanufaika na kuongeza uwazi, ingawa wakati mwingine hitilafu za mtandao husababisha ucheleweshaji wa huduma.

Mkazi wa Mbagala, Wilaya ya Temeke, Dar es Salaam, Rehema Mushi amesema kuanza kunufaika na Bima ya Afya kwa Wote kumemwepusha na mzigo wa kutafuta fedha kila mtoto anapougua.

"Mambo yako vizuri. Changamoto iliyobaki ni kwamba wakati mwingine baadhi ya dawa zinaisha na tunaelekezwa kununua nje," amesema.

Mkazi wa Sinza, Wilaya ya Ubungo, Mohamed Suleiman ambaye hupata matibabu ya shinikizo la damu, amesema bima imemrahisishia kufuatilia huduma za afya bila kubeba fedha taslimu kila anapoenda hospitalini.

"Ukiwa na bima unaondokewa na hofu ya gharama za matibabu, lakini tungependa dawa zote muhimu zipatikane hospitalini," amesema.

Hata hivyo, pamoja na changamoto hizo, utekelezaji wa mpango huo unaendelea kuonesha mafanikio katika maeneo mbalimbali nchini.

Mkoani Mbeya, usajili wa kaya zisizo na uwezo umefikia asilimia 75 katika awamu ya kwanza ya majaribio ya utekelezaji wa mpango huo.

Takwimu zinaonesha kuwa kati ya kaya 7,921 zilizolengwa kusajiliwa, kaya 5,933 tayari zimesajiliwa na kuanza kupata huduma za matibabu katika vituo vya afya vya umma.

Meneja wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), ambao ndiyo watekelezaji wa mpango huo Mkoa wa Mbeya, Dk Eliud Kilimba amesema wanufaika waliosajiliwa wanapata huduma pamoja na wategemezi wao, huku wakisubiri maelekezo ya Serikali kuhusu kuanza kwa awamu inayofuata itakayohusisha makundi mengine ya wananchi.

Katika Mkoa wa Mara, wanufaika wa awamu ya kwanza, hasa wale waliotokana na kaya za Tasaf, wanasema huduma zimeanza kuwafikia na kuondoa hofu ya kushindwa kumudu gharama za matibabu.

Yustina Majura, mkazi wa Musoma, amesema alipata huduma katika Kituo cha Afya Nyasho bila kulipa fedha yoyote, huku Merina Kasaje akisema alijutia kutokujiandikisha mapema baada ya kuona wenzake wakinufaika.

Meneja wa NHIF Mkoa wa Mara, Kuhungwa Msambichaka amesema zaidi ya wananchi 27,000 walisajiliwa katika awamu ya kwanza na idadi ya wanaopata huduma inaendelea kuongezeka.

Kwa upande wa Geita, wananchi wameiomba Serikali kuongeza usimamizi wa utoaji wa huduma katika vituo vya afya ili kuhakikisha dawa na huduma muhimu zinapatikana kwa wakati.

Mtaalamu wa masuala ya afya kutoka Simiyu, Boniphace Mabonesho amesema mafanikio ya Bima ya Afya kwa Wote yatategemea zaidi uwezo wa Serikali kuimarisha upatikanaji wa dawa, vifaa tiba, mifumo ya Tehama na elimu kwa wananchi.

Meneja Uhusiano kwa Umma wa NHIF, James Mlowe amesema uandikishaji wa kaya maskini unaendelea katika mikoa mbalimbali nchini na taarifa za maendeleo zinawasilishwa kila siku.

Amesema fedha za kugharamia mpango huo ni za Serikali, hivyo tarehe rasmi ya kuanza kutumika itatangazwa na waziri mwenye dhamana baada ya taratibu zote kukamilika.

"Wananchi wanauliza kila siku kuhusu lini mpango utaanza kutumika. Kwa sasa tunaendelea na uandikishaji wa kaya maskini na tunapokea taarifa kutoka mikoani. Tamko rasmi la kuanza kutumika litatolewa na waziri," amesema Mlowe.


Ufafanuzi wa serikali

Kwa mujiu wa Serikali, utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote unaendelea kwa awamu, huku kaya 276,004 zisizo na uwezo zikiwa tayari zimesajiliwa na kuanza kunufaika na huduma za matibabu kupitia mpango huo, wakati maandalizi ya kusajili mamia ya maelfu ya kaya nyingine yakiendelea.

Dk Magembe ambaye ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, amesema baada ya kuanza kwa mwaka wa fedha 2026/27, Serikali inaendelea kukamilisha ugawaji wa kadi za bima kwa kaya zilizosajiliwa katika awamu ya kwanza, ambazo zinajumuisha wananchi 1,206,319.

"Dhamira ya Serikali ni kuhakikisha kaya zote zisizo na uwezo zilizotambuliwa zinapata kadi zao na kuanza kupata huduma. Hadi Juni 2026, kaya 180,008 sawa na asilimia 65 zilikuwa tayari zimechukua kadi za uanachama, huku zoezi la kusambaza kadi zilizobaki likiendelea kupitia ofisi za NHIF kwa kushirikiana na viongozi wa mikoa na wilaya," amesema Dk Magembe.

Amesema Serikali imegharimia Sh51.59 bilioni bima ya afya kwa kaya hizo, huku pia ikiwapatia bima wazee na watoto wanaoishi katika makazi yanayosimamiwa na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu.

Dk Magembe amesema Julai hadi Septemba mwaka huu, Serikali inajiandaa kusajili kaya nyingine 655,689 zisizo na uwezo zilizopo kwenye kanzidata ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf).

Akizungumzia kifurushi kipya cha bima ya afya cha Sh150,000, amesema wananchi tayari wameanza kunufaika nacho, lakini utekelezaji wake unafanyika kwa awamu, ukianza na kaya zisizo na uwezo ili kutoa nafasi ya elimu na uhamasishaji kabla ya usajili wa wananchi wa sekta binafsi na sekta isiyo rasmi kuanza.

"Serikali imekamilisha maandalizi muhimu ikiwamo miongozo ya usajili wa wanachama, utoaji wa huduma, haki na wajibu wa wadau pamoja na mkakati wa mawasiliano. Pia, mifumo ya Tehama imeimarishwa ili wananchi waweze kujisajili kidigitali na vituo vya kutolea huduma kuwasilisha madai moja kwa moja bila kutumia karatasi," amesema.

Amesema maboresho hayo yamepunguza muda wa kulipa madai ya vituo vya afya kutoka siku 60 hadi chini ya siku 45, hatua inayolenga kuongeza ufanisi na kudhibiti udanganyifu.

Kuhusu matarajio ya kuanza kwa awamu ya pili ya usajili, Dk Magembe amesema hakuna mkwamo wa kifedha wala kiutendaji, bali Serikali inatekeleza mpango wake kwa hatua ili kuhakikisha wananchi wanapata elimu ya kutosha kuhusu umuhimu wa kuwa na bima ya afya kabla ya kuugua.

"Hatutaki wananchi waingie kwenye mfumo bila uelewa. Tathmini ya awamu ya kwanza itakapokamilika, Serikali itatoa tangazo rasmi kuhusu kuanza kwa hatua inayofuata ili wananchi wengi waweze kushiriki," amesema Dk Magembe.



Imeandikwa na Herieth Makwetta (Dar) Joseph Lyimo (Manyara) Godfrey Chubwa (Geita) Beldina Nyakeke (Musoma) Samwel Mwanga (Simiyu) Yese Tunuka (Kilimanjaro) na Hawa Mathias (Mbeya)