Bilioni 18 kupeleka umeme kwa wachimbaji wadogo Kanda ya Ziwa

Muktasari:
Serikali kupitia Shirika la Umeme nchini (Tanesco) imetoa zaidi ya Sh18 bilioni kupeleka nishati ya umeme maeneo ya wachimbaji wadogo katika Mikoa ya Kanda ya Ziwa lengo likiwa ni kuwapunguzia gharama kubwa za matumizi ya mafuta wanayotumia sasa.
Geita. Serikali kupitia Shirika la Umeme nchini (Tanesco) imetoa zaidi ya Sh18 bilioni kupeleka nishati ya umeme maeneo ya wachimbaji wadogo katika Mikoa ya Kanda ya Ziwa lengo likiwa ni kuwapunguzia gharama kubwa za matumizi ya mafuta wanayotumia sasa.
Akizungumza Septemba 22, 2023 katika Kongamano la wadau lililofanyika katika maonyesho ya sita ya kimataifa ya teknolojia ya madini yanayoendelea mjini Geita, Meneja wa Shirika la umeme (Tanesco) Mkoa wa Geita, Grace Ntungi amesema kwa mkoa huo mradi huo utapeleka umeme katika maeneo 35.
Amesema mradi huo ambao ni maalum kwa ajili ya maeneo ya mikoa ya Kanda ya Ziwa unatekelezwa kwa miezi 18 chini ya mkandasi OK Electrical and Electronics Services na tayari utekelezaji wake umeanza kuanzia Januari mwaka huu.
Amesema ukosefu wa umeme kwenye maeneo ya wachimbaji wadogo imekuwa kilio cha muda mrefu kwani hulazimika kutumia nishati ya mafuta ambayo ni gharama kubwa hivyo kuwafanya washindwe kunufaika na uchimbaji madini.
Akizungumzia mradi wa Peri-Urban unaolenga kupeleka umeme kwenye maeneo ya vijiji vilivyopo kwenye miji, Ntungi amesema mradi huo unaofadhiliwa na Wakala wa Nishati vijijini (REA) kwa gharama ya Sh8.1 bilioni utapeleka umeme kwenye vijiji 42 vilivyopo ndani ya Mkoa wa Geita na utakamilika Desemba 2024.
Naibu Waziri Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe akizungumza kwenye kongamano hilo lilizokutanisha taasisi mbalimbali za sekta ya madini amezitaka taasisi zilizoko kwenye mnyororo wa thamani wa madini kuwalea wachimbaji wadogo ili wanufaike na rasilimali hiyo badala ya kusubiri wakosee ili wawapige faini ama kuwapa adhabu.
“Tusifikie kuwapa adhabu na faini maana hii inawakatisha tamaa lengeni kuwasaidia ili wasikosee sio kwamba wanakosea kwa kukusuida wengi hawana elimu na hawapati taarifa sahihi tuwasaidie kuona rasilimali wanazotumia wanatumia kwenye eneo sahihi,”amesema Kigahe
Kigahe ametaka taasisi za Serikali kupunguza urasimu wanaoufanya kwa kuweka vikwazo visivyo vya lazima na kusema licha ya wachimbaji wadogo kuwa na mchango mkubwa kwenye mapato serikalini lakini uelewa mdogo wa sheria na kanuni hukwamisha jitihada zao.