Bawacha,TEC watoa ya moyoni sheria za uchaguzi

Mwenyekiti wa Bawacha, Suzan Lyimo
Muktasari:
- Bawacha wameungana na Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC) kutaka sifa za mgombea zitumike zilizomo kwenye Katiba ya Jamhuri badala ya kuwa na sifa za ziada, kama vile kukosea kujaza fomu au muhuri kugongwa kwenye sura ya picha.
Dodoma. Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha) limetoa maoni yake likitaka matokeo ya urais katika majimbo ya uchaguzi, yatangazwe kwenye gazeti la Serikali ndani ya mwezi mmoja baada ya Uchaguzi Mkuu.
Pia, Bawacha wameungana na Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC) kutaka sifa za mgombea zitumike zilizomo kwenye Katiba ya Jamhuri badala ya kuwa na sifa za ziada, kama vile kukosea kujaza fomu au muhuri kugongwa kwenye sura ya picha.
Akitoa maoni ya Bawacha mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria kwenye ukumbi wa Bunge wa Pius Msekwa leo Januari 8, Makamu Mwenyekiti wake Susan Lyimo amesema hadi sasa matokeo ya urais ya majimbo hayajatangazwa kwenye gazeti la Serikali.
“Niko tayari kusahihishwa hapa, matokeo ya urais kwenye majimbo hadi sasa hayajawekwa kwenye gazeti la Serikali.
“Sisi Bawacha tunapendekeza matokeo ya kura za urais kwa ngazi ya majimbo zitangazwe kwenye gazeti la Serikali ndani ya mwezi mmoja,” amesema.
Lyimo pia amezungumzia suala la wakurugenzi wa halmashauri kusimamia uchaguzi kwamba siyo sahihi kwa kuwa ni watumishi wa umma na wamekuwa wakisimamia masilahi ya aliowateua.
“Mfano, Rais Magufi (John) ambaye amefariki dunia aliwahi kutamka kwa kuwaeleza wakurugenzi kwamba hawezi kuwalipa mshahara halafu waje kumtangaza mgombea wa upinzani kuwa ameshinda,” amesema Lyimo.
Pia, amesema wakurugenzi wako chini ya Waziri wa Tawala za Mikoa na serikali za mitaa (Tamisemi) na ndio wanawajibika huko na si kwenye Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec).
Amesema sheria inaelekeza mgombea akienguliwa na mkurugenzi, akate rufaa kwa mkurugenzi wa uchaguzi wa Nec, lakini aliongeza kuna waliokata rufaa na mkurugenzi wa Nec akawarejesha, lakini mkurugenzi wa halmashauri aliyekuwa msimamizi wa uchaguzi akakataa.
Hoja hiyo imezungumziwa na TEC wakishauri jukumu la usimamizi wa uchaguzi lifanywe na watumishi wa NEC.
Katibu wa TEC, Dk Charles Kitima amesema maaskofu wanapenda kuona hoja za watu juu ya kuwa na tume huru ya uchaguzi, zinafanyiwa kazi.
“Nchi za wenzetu nyingi zimeanza kurekebisha tume za uchaguzi zikawa huru na kwamba ngazi za chini kule kwa wenzetu matatizo ni karibu yamekwisha, huko juu kwenye urais ndio bado changamoto zipo, utazikuta hata Marekani.
“Lakini huku chini kutokana na Tume kuwa huru…Afrika Kusini tume ina wafanyakazi karibu 1,000, Kenya ina wafanyakazi karibu 900, Tanzania tuna uwezo wa kuajiri pia watumishi wa tume.” alisema.
Kwa upande wake, mwenyekiti wa Ngome ya Vijana ya ACT-Wazalendo, Abdul Nondo naye alitoa maoni kuhusu suala la wakurugenzi wa halmashauri akisema baadhi ya wakurugenzi ni wanasiasa na wamekuwa wakijonyesha hivyo.
Amesema kwa hoja hiyo wakurugenzi hawana sifa ya kuwa watu wasio na upande kwenye kusimamia uchaguzi huku akinukuu kifungu cha Katiba ya Jamhuri ibara 74 (14) kinachokatazwa watumishi wa umma kujihusisha na siasa.
Nondo amesema kwa wakurugenzi hawa kufanya kazi za kisiasa ni kujihusisha na siasa, hoja iliyopingwa na Mbunge wa Jimbo la Ziwani Kisiwani Pemba, Ahmed Juma Ngwali ambaye ni mjumbe wa kamati hiyo, akinukuu ibara ya 20 (1) ya Katiba ya Jamhuri inayotoa uhuru kwa kila raia wa Tanzania kushiriki siasa.
Naye Mkurugenzi wa utetezi na maboresho wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), Fulgence Massawe amesema kifungu kinachoelezea uteketezaji wa nyaraka za uchaguzi baada ya miezi sita kirekebishwe.
Kwa mujibu wa Masswe, kesi nyingi za uchaguzi huwa zinachukua muda mrefu mahakamani, hivyo kuteketeza nyaraka kutasababisha wahusika wa kesi za uchaguzi kukosa nyaraka kwa ajili ya ushahidi.
Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba, Dk Ananilea Nkya amesema kuna haja kuweka kifungu kinachoviwajibisha vyombo vyote vya habari kutoa haki sawa kwa wagombea.
Imeandikwa na Noor Shija