Basi lateketea kwa moto, abiria 50 wanusurika

Basi la kampuni ya Happy Nation ambalo limeteketea kwa moto maeneo ya bonde la Wami mkoani Pwani.
Muktasari:
Abiria zaidi ya 50 waliokuwa wakisafiri na basi la Happy Nation wamenusurika na kifo baada ya basi hilo kuteketea kwa moto mkoani Pwani.
Dar es Salaam. Zaidi ya abiria 50 waliokuwa wakisafiri na basi la kampuni ya Happy Nation wamenusurika kifo baada ya basi hilo kuteketea kwa moto mkoani Pwani.
Tukio hilo limetokea leo Jumatatu Desemba 19, 2022 saa nne asubuhi maeneo ya bonde la Wami wakati basi hilo likitokea Dar es Salaam kuelekea Arusha.
Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Issa Inkya ameliambia Mwananchi kwamba licha ya basi kutekekea kwa moto hakuna madhara kwa binadamu na wote walitoka salama pamoja na mali zao.
“Kwa mujibu wa maelezo ya watu wangu wameniambia chanzo cha basi kuungua ni hitilafu ya waya katika mfumo mzima wa gari, nipo njiani kuelekea huko kwa jinsi lilivyoungua sidhani kama litafaa kwa matumizi,” amesema Inkya.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Pius Lutumo amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo, akisema hata hivyo, haikusababisha madhara yoyote kwa abiria na mali zao.
"Ni kweli leo bahati nzuri waliwahi kuokoa mali za abiria na hakuna madhara yoyote kwenye ajali hiyo," amesema Kamanda Lutumo.