Prime
Bandari ilivyounganisha wanaharakati na Chadema, kudhihirisha umoja ndani ya CCM

Muktasari:
- Januari 3, 2023 Rais Samia Suluhu Hassan alipoondoa marufuku ya mikutano ya hadhara ya kisiasa, mapokeo yalikuwa ya shukurani. Ni haki yao ambayo ilikuwa imenyimwa, ikarejeshwa. Si utumwa kumshukuru aliyerejesha, bali ni tendo la kiungwana.
Januari 3, 2023 Rais Samia Suluhu Hassan alipoondoa marufuku ya mikutano ya hadhara ya kisiasa, mapokeo yalikuwa ya shukurani. Ni haki yao ambayo ilikuwa imenyimwa, ikarejeshwa. Si utumwa kumshukuru aliyerejesha, bali ni tendo la kiungwana.
Vyama vikuu vya upinzani Tanzania, Chadema na ACT-Wazalendo, vilitangaza uzinduzi wa mikutano yao. Chadema Januari 21, 2023 katika Uwanja wa Furahisha, Mwanza. ACT Februari 19, 2023, Zakhem, Mbagala, Dar es Salaam.
Uzinduzi wa mikutano hiyo ya Chadema na ACT, unaweza kuuweka kwenye sentensi moja ya maneno mawili, “Asante Samia". Kwa sehemu kubwa wazungumzaji wa upinzani katika mikutano hiyo, walijitahidi kuwa waungwana na kuonyesha shukurani zao kwa Rais Samia.
Japokuwa, Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Tanzania Bara, Tundu Lissu alionekana kuwa na hoja za moto kwa Serikali, lakini zipo nyakati naye alikiri na kutambua uungwana wa Rais Samia. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema wana-Chadema watake au wasitake, angemshukuru Rais Samia.
Miezi sita imepita tangu mkutano wa Furahisha na mitano tangu ule wa Zakhem. Agenda ya mkataba wa bandari baina ya Tanzania na Dubai imefungua siasa kwa namna ya kipekee. Hoja za Chadema si zile za "Asante Samia", bali wanarusha mawe kwelikweli.
CCM nao wakaamka, wakajibu mapigo. Mchuano wa hoja kwenye mikutano ya CCM na Chadema kuhusu bandari, umetoa picha kuwa kila upande upo huru kutumia msuli na silaha zake dhidi ya mwingine. Hakuna aliyeshikwa mkono!
Kuna mtu aliandika "Rais Samia ameruhusu mikutano atakoma". Ni mtazamo wake. Ukitazama mchuano wa mikutano kuhusu bandari, baina ya CCM na Chadema, unaona kuna faida nyingi kwa Rais Samia. Muhimu zaidi, kwa Watanzania.
Faida za Rais Samia
Katika wazungumzaji kuhusu bandari, Lissu amesemwa kwa kutokuwa na maneno ya staha dhidi ya Rais Samia. Mbowe anashutumiwa kwa kuanzisha hoja za mgawanyiko wa Uzanzibari na Utanganyika.
Aina ya uzungumzaji wa Lissu na Mbowe ni faida kwa Rais Samia. Amejionea na amejua aina ya wanasiasa ambao yupo nao ulingoni na hoja zao. Anapotaka kukabiliana nao, ni msuli kiasi gani wa kuutumia na silaha zipi za kuingia nazo ‘vitani’.
Uwanja wa ‘vita’ kwa wanasiasa ni majukwaa ya kisiasa. Silaha za kivita kwenye siasa ni hoja. Umahiri wa kujenga hoja ndiyo msuli katikati ya mapigano ya kisiasa. Mikutano ya CCM na Chadema, inaweza kumpa picha Rais Samia, uwezo wa jeshi lake dhidi ya wapinzani.
Chadema wanazunguka na mikutano yenye utambulisho wa “Oparesheni +255 Katiba Mpya, Okoa Bandari Zetu”. CCM waliingia kazini baada ya tamko la Halmashauri Kuu CCM (NEC), lililotaka wananchi waelimishwe zaidi kuhusu uwekezaji wa bandari na faida zake kwa Taifa.
CCM walizunguka na aina mbili ya misafara, mmoja uliongozwa na Makamu Mwenyekiti Tanzania Bara, Abdulrahman Kinana, wa pili chini ya Katibu Mkuu, Daniel Chongolo. Chadema mikutano inaongozwa na Mbowe na mingine na Lissu.
Msafara wa Kinana, akiwa Kondoa, Dodoma, alisema Rais Samia ni mtulivu, hakurupuki kujibu mashambulizi. Bila shaka, kwa utulivu wake, ameona nguvu za pande mbili na sasa anajua nafasi yake kama mwenyekiti wa CCM na upepo ulivyo kisiasa.
Hoja kwa hoja
Kesi ya kupinga Mkataba wa Bandari, ilifunguliwa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya. Pamoja na hatua hiyo kuchukuliwa, bado siasa hazikusimama. Maneno ya tambo hadi lugha kali zilitoka kila upande. Suala la bandari lilifanya siasa za nchi ziwe na ukumbusho wa miaka minane nyuma.
Wakati huo ungewaona Chadema chini ya Mbowe, wapo mitaani na Operesheni Sangara, halafu CCM na Kinana (katibu mkuu wakati huo), akiongoza timu yake kukipeleka chama kwa wananchi, huku akiwashughulikia mawaziri kwa kuwaita mizigo.
Katika bandari, unawaona CCM wakimtumia Profesa Kitila Mkumbo kutoa elimu kuhusu mkataba, kisha Albert Msando, yeye kazi yake kupangua hoja za kisheria na kuchambua mkataba huo kueleza faida zake.
Upande wa Chadema, Lissu kazi yake ni kutumia lugha kali kujaribu kutafuta kuungwa mkono hadi na wale ambao miaka mitatu iliyopita asingeiva nao. Mathalan, amewaangukia mpaka wafuasi wa Rais wa tano, Dk John Magufuli, aliposema kuwa atakwenda Chato kumwombea.
Veterani Stephen Wasira, mtu mahiri katika siasa, yeye kazi yake ikawa kushusha vigongo na kusuta. Anachukua hoja za upande wa pili na kuzigeuza. Mfano, suala la Lissu kumtumia Magufuli, Wasira anasema "watu wanasahau hata jana walizungumza nini, miaka yote huyu ndiye alikuwa anamtukana Magufuli, leo anamwona mzuri."
Chongolo, anasimama kutafsiri msimamo wa CCM na msukumo wake kama chama kwa Serikali, kuhusu uwekezaji wenye tija bandarini. Kinana, kiutu-uzima, hotuba zake kwa sehemu kubwa zinajikita kumsafisha Rais Samia na kumlinda dhidi ya mishale iliyoelekezwa kwake.
Mbunge wa Ukonga, Jerry Silaa, yeye kazi yake ni kama Msando, lakini hakuwa akitumia lugha za kejeli. Alijikita zaidi kuelimisha. Mjumbe wa Halmashauri Kuu CCM (Nec), Richard Kasesela, yeye alikuwa anarusha makombora ya kisiasa.
Kwa kifupi, bandari imewezesha kufungua anga la kisiasa. Na kwa vile umebaki mwaka mmoja kufanyika kwa uchaguzi wa Serikali za Mitaa, vilevile miwili kabla ya Uchaguzi Mkuu 2025, suala la bandari limebebwa kama mtaji mkubwa kuelekea misimu ya uchaguzi.
Uwekezaji mkubwa ambao Chadema wanauweka katika ajenda ya bandari, unaweza kupatia kama utasema kwamba wameona ndiyo mtaji wa kujenga imani kubwa kwa wananchi. Hii ni baada ya kupita miaka sita pasipo kuwa na fursa ya kufanya siasa kwa uhuru unaopaswa ama hoja zenye mashiko na sasa wameupata sasa turufu ya kukimbia nayo.
Ni kama Chadema wanasema "hatutaki kurudia makosa". Kwamba baada ya kifungo cha kisiasa cha miaka sita, wanaona mazingira ya sasa ni fursa ya dhahabu ya kutwaa dola.
Wanajaribu kutumia kila kadi ili kujenga uungwaji mkono. Wanacheza karata ya hayati Magufuli, wanacheza bao la Utanganyika.
Pengine Wasira amelielewa hilo na aliwatangulia mbele aliposema, hoja ya bandari inabebwa zaidi na wanaoutaka Urais kwenye Uchaguzi Mkuu 2025. Kisha akasema, Chadema wanamvizia Rais Samia mithili ya fisi kwa mkono wa binadamu akidhani unavyoyumba utadondoka.
CCM inavyotumia silaha zake
Chadema wamefanikiwa kuchokoza mjadala na kuendelea kukazia maudhui waliyoanza nayo. Mafanikio ya Chadema yapo pia walipoweza kuunganisha nguvu na wanaharakati mbalimbali wenye kupinga mkataba. Imewezekana hadi kuchangia jukwaa na katibu mkuu wao wa zamani, Dk Willibrod Slaa, ambaye walishapitia vipindi vya uadui. Imewashtua wengi kwa Dk Slaa kukaa jukwaa moja na Chadema.
Pamoja na kuwafikia wananchi na kuzungumza nao, mafanikio makubwa ya CCM ni jinsi walivyoweza kusimama pamoja. Wamedhihirisha ni wamoja kama chama. Inawezekana ndani kwa ndani kuna misuguano, ila walipotoka nje, CCM imeonekana ni moja. Huu ndio umuhimu wa kula chumvi nyingi na kuwa mkubwa.
Hata wale waliokuwa wakidhaniwa kwamba hawatajitokeza kuutetea mkataba, Kinana na Nazir Karamagi wakidaiwa kuwa na masilahi wamepanda jukwaani na kuupigania.
Kinana ametoka na kuwataka Watanzania kumwamini Rais Samia kuhusu suala la bandari, vivyo hivyo Karamagi, mwenyekiti wa CCM Kagera na mmiliki mwenza wa kampuni ya Ticts ambayo kwa miaka 20 ilikuwa ikiendesha Bandari ya Dar es Salaam.
Karamagi alikuwa kitovu cha mashambulizi, lakini amesimama jukwaani na kutetea mkataba wa bandari baina ya Tanzania na Dubai. Alisema kuwa kwa hali iliyofikia, Bandari ya Dar es Salaam inahitaji kampuni yenye uwezo mkubwa zaidi ya Ticts.
Kinana na Karamagi wamezika maneno mengi yaliyosemwa kabla.
Aliyekuwa Spika wa Bunge, Job Ndugai, naye alipanda jukwaani. Kwa sehemu kubwa CCM walitumia kila silaha na walidhihirisha umoja wao katika kuitetea Serikali yao.
Kuhusu mafanikio ya mikutano si rahisi kuyapima, kwani inategemea na mapokeo. Mahudhurio yamekuwa mazuri kwa mikutano na kwa sababu hii ni dunia ya Tehama, vipande vya video vimekuwa vikisambaa na ujumbe kufika mbali.
Hii ni maana kwamba, kazi ambayo Chongolo na timu yake walitumwa kuifanya na NEC wameitimiza kwa mafanikio kufikisha ujumbe kuhusu uzuri na mafanikio kwa Tanzania kuingia kwenye uwekezaji huo. Chongolo na timu yake wamezunguka kwenye Kanda zote nchini wakifanya mikutano bandika bandua bila kupumzika huku Chadema nao wakiendelea kupasua anga kuupinga.