Serikali yahitimisha hoja zake kesi ya Mkataba wa Bandari

Muktasari:
- Serikali imefunga utetezi wake katika kesi ya mkataba baada ya kujibu hoja zote za wadai. Sasa imebakia zamu ya upande wa madai kurejea tena kujibu hoja za Serikali na kuaiachia Mahakama jukumu la uamuzi
Mbeya. Serikali imehitimisha hoja zake katika kesi ya makubaliano ya ushirikiano wa kiuchumi na kijamii, kati ya Serikali ya Tanzania na Dubai (IGA), huku ikidai kuwa wadai katika kesi hiyo wameshindwa kufikia viwango vinavyotakiwa katika Mashauri ya Kikatiba kuthibitisha madai ya ukiukwaji wa Katiba.
Jopo la mawakili wa Serikali linaloongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Mark Mlwambo limehitimisha jukumu lake hilo leo Alhamis Julai 27, 2023, la kujibu hoja za upande wa madai katika kesi hiyo, ambalo walilianza jana baada ya mawakili wa upande wa wadai kuhitimisha hoja zao.
Jana Julai 26, 2023 mawakili hao wa upande wa madai, Mpale Mpoki, Boniface Mwabukusi, Philipo Mwakilima na Livino Ngalimitumba walichambua Ibara zote za mkataba huo wanazozipinga na kuonesha kile wanachodai masharti mabovu yasiyo na maslahi kwa Taifa na jinsi unavyokiuka Sheria na Katiba ya Nchi.
Katika hoja zao walitoa ufafanuzi wa madai yao ili kuishawishi mahakama kuwa mkataba huo ni batili kwa kuwa na ibara hizi zina masharti yanayokiuka Sheria za Ulinzi wa Raslimali na Maliasili za Nchi, Katiba na kwamba unaondoa ukuu wa Nchi na kuiweka chini ya Dubai na vile vile kuathiri Maliasili za Taifa na kuhatairisha usalama wa Taifa.
Pia walifafanua madai yao ya mchakato wa kuridhiwa na Bunge ulivyoikuka Sheria kwa kutowapa wananchi kwanza nafasi ya kutoa maoni yao kabla ya kuridhiwa kama Sheria zinavyoelekeza
Vilevile walifafanua madai yao kuwa ni batili kutokana kwa madai kwamba Dubai haina mamlaka kuingia mkataba wa Kimataifa kama huu kwa mujibu wa Ibara ya 123 ya Katiba ya Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) na kwamba jukumu hilo linapaswa kufanywa na Serikali ya Umoja huo.
Baada ya wadai kumaliza hoja zao Serikali ilianza kujibu hoja hizo lakini ilifsnikiwa kujibu hoja mbili tu kati ya Sita zinazobishaniwa ambazo ndizo Mahakama utajikita katika katika kutoa uamuzi wake na hivyo imemalizia leo hoja nne zilizosalia.
Katika kujibu hoja hizo mawakili hao wa Serikali, Wakili Mkuu wa Serikali Edson Mweyungee na mawakili wa Serikali Stanley Kalokola na Edwin Webiro kwa nyakati tofauti wamechambua Ibara mbalimbali za mkataba huo zinazolalamikiwa wakilinganisha na bifungu vya Sheria za Nchi na Ibara. za Katiba ya Nchi zinazodaiwa kulikuwa na Mkataba huo.
Hata hivyo baada ya kufanya uchambuzi huo wamehitimisha kwa kudai kuwa hakuna kifungu chochote cha Sheria wala Ibara ya Katiba iliyokiukwa.
Katika ujumla wake wamedai kuwa mkataba huo unaolalamikiwa ni mkataba wa Kimataifa hivyo utekelezaji wake hauongozwi na Sheria za Nchi bali Sheria za Kimataifa kama Mkataba wa Kimataifa wa Vienna unavyoeleza kuhusu utekelezaji wa Mikataba ya Kimataifa, ambao Tanzania imeusaini na kuwa mwanachama.
Akihitimisha hoja hizo Wakili Mlwambo ameiomba Mahakama Kuu Mbeya inayosikilizwa kesi hiyo kulitupilia mbali na kuiomba iwaamuri wadai wailioe Serikali gharama.
"Katika kuhitimisha Waheshimiwa majaji tumeweza kuonesha standard (kiwango) ambacho inatakiwa tunapoongelea mashauri ya kikatiba. Tumejibu hoja kwa hoja na baada ya kumaliza hoja zetu tunaomba mahakama iweze kutoa amri kwamba. Bunge lilitekeleza wajibu wake wa kisheria na hakuna mahali popote lilikosea.",amedai Wakili Mlwambo na kuongeza:
"Pia tunaomba Mahakama iweze kutamka kwamba mkataba wa IGA uliokjwa unajadiliwa humu ni wa Kimataifa na Serikali ya Tanzania ilikuwa na haki kuingia na kutumia Sheria za Kimataifa. Na mwisho tunaiomba Mahakama iamue kwamba shauri hili halina mashiko na ilitupilie mbali na Serikali ilipwe gharama."
Baada ya Serikali kuhitimisha sasa mawakili wa wadai nao watarejea kwa ajili ya kujibu hoja zilizoibuliwa na mawakili wa Serikali wakati walijibu hoja zao kuhusiana na maelezo waliyoyatoa katika kufafanua hoja Sita zilizokubaliwa na pande zote kuwa ndizo zinazobishaniwa na kamba ndizo zinapaswa kuamuriwa na Mahakama.
Baada ya mawakili hao wa wadai kumaliza kujibu hoja hizo ambayo ni majibu ya ziada kuhusiana na hoja zilizotolewa na Serikali, kesi hiyo itakuwa imefikia mwisho katika hatua ya usikilizwaji na sasa mpira utabaki kwa mahakama yaani hatua ya uamuzi.
Hivyo Mahakama inaweza ikapanga na kuzitaja tarehe ya uamuzi leo hii au ikawataarifu wadaiwa (pande husika za kesi) baadaye itakapokuwa imekamilisha kuandika uamuzi huo.
Kesi hiyo imefunguliwa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya na mawakili wanne kutoka mikoa tofauti ambao ni; Alphonce Lusako, Emmanuel Chengula, Raphael Ngonde na Frank Nyalus dhidi ya Serikali.
Wadaiwa ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), ambaye ni mshauri wa Serikali kwa masuala ya kisheria, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi na Katibu wa Bunge la Tanzania, ambaye ni mtendaji mkuu na mratibu wa shughuli za Bunge.
Katika kesi hiyo ya Kikatiba namba 5 ya mwaka 2023 wanapinga makubaliano hayo yanayohusha uwekezaji katika Bandari za Tanzania zilizoko katika mwambao wa bahari na katika maziwa, kuwa ni batili kwa kuwa yana Ibara zinazokiuka Sheria na Katiba ya Nchi.
Pia, wanadai kuwa mchakato wa kuridhia Bungeni ni batili kwa kuwa haukufuata utaratibu wa kisheria na bila kuwapa nafasi ya kutosha wananchi kutoa maoni yao kama sheria za Nchi zinavyoelekeza.
Kesi hiyo inasikilizwa na jopo la majaji watatu, Dunstan Ndunguru( Kiongozi wa jopo), Mustafa Ismail na Abdi Kagomba