Baba: Niliambiwa nichague kiungo cha mwanangu nikazike
Mtoto aliyekuwa ametekwa, Paulina Paulo akiwa na Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Paul Chacha.
Muktasari:
- Baada ya kutekwa akiwa shule, Paulina alishikiliwa kwa siku 11 huku watekaji wakidai Sh20 milioni na kutishia kumuua, familia iliishi katika hofu kubwa, lakini juhudi za Jeshi la Polisi zimefanikisha kuokolewa akiwa salama.
Tabora. "Nilipoambiwa nichague kiungo chochote cha mwili wa mwanangu nikazike, nilihisi dunia imesimama. Sikujua kama bado ningemuona akiwa hai."
Hayo ni maneno ya Paulo Salum, baba mzazi wa Paulina Paulo, mwanafunzi wa darasa la kwanza katika Shule ya Msingi Bulunde oliyopo Igunga mkoani Tabora, akisimulia siku 11 ngumu alizopitia baada ya mwanawe kutekwa akiwa shuleni na kushikiliwa huku watekaji wakitaka mamilioni ya shilingi ili wamuachie.
Kwa sauti ya huzuni na hisia nzito, Paulo amesema tukio hilo lilianza Juni 1, 2026, wakati akiwa katika shughuli zake za kawaida bila kufahamu kwamba binti yake alikuwa ameondolewa shuleni kwa kutumia mbinu za udanganyifu.
Amesema mwanamke mmoja ambaye ni mke wa mjomba wa familia hiyo, alienda shuleni kwa Paulina na kujitambulisha kwa walimu kuwa ametumwa na wazazi wa mtoto huyo kwenda kumpiga picha kwa ajili ya kufunguliwa akaunti ya benki.
Kwa kuwa alikuwa mtu anayefahamika na familia pamoja na mtoto mwenyewe, hakukuwa na mashaka yoyote. Walimu waliridhika na maelezo hayo na Paulina akaondoka naye bila hofu yoyote.
Baada ya kutoka shuleni, mwanamke huyo alimvalisha sweta mtoto huyo na kumpandisha kwenye pikipiki, kisha kutokomea naye kusikojulikana.
Paulo Salum baba mzazi wa mtoto Paulina aliyetekwa Igunga, Tabora.
"Siku hiyo hiyo baadaye tulipokea simu. Alitwambia kwamba amemchukua mtoto wetu. Hapo ndipo tulianza kupata wasiwasi mkubwa," anasimulia Paulo.
Muda mfupi baadaye, familia ilipokea ujumbe mfupi wa simu uliokuwa na madai ya fedha. Watekaji walitaka walipwe Sh20 milioni ili kumuachia mtoto akiwa hai.
Lakini, kilichoumiza zaidi familia hiyo si kiwango cha fedha walichotakiwa kulipa, bali vitisho walivyokuwa wakipewa.
"Walituambia kuwa tusipotoa fedha watamchinja mtoto. Neno hilo lilituchanganya sana. Kama mzazi unaposikia mtu anasema atamuua mwanao, unakosa kabisa utulivu," amesema Paulo.
Amesema mara moja waliwasilisha taarifa Polisi huku wakijaribu kuendelea kuwasiliana na mtekaji kupata matumaini ya kumuokoa mtoto huyo.
Katika mazungumzo mbalimbali kwa simu, Paulo alijaribu kumwomba mtekaji asimdhuru mtoto wake. Hata hivyo, kiwango cha fedha kiliendelea kuongezeka huku simu zikizimwa mara kwa mara.
"Alikuwa anapiga simu kudai fedha, baada ya hapo anazima simu hata kwa siku mbili. Tulikuwa tunaishi katika hofu kubwa sana bila kujua mtoto yuko katika hali gani," amesema.
Kutokana na presha na hofu ya kumpoteza mtoto, Paulo amesema familia ililazimika kutuma Sh5 milioni kama sehemu ya fedha zilizokuwa zinadaiwa.
Hata hivyo, mtekaji hakuridhika na kiasi hicho.
"Alisema hataweza kumwachia mtoto mpaka fedha zote zikamilike. Tulijua bado safari ilikuwa ndefu."
Siku zilivyozidi kwenda, mateso ya kisaikolojia kwa familia yaliongezeka. Paulo anasema kuna wakati alipigiwa simu na kuambiwa jambo ambalo halitafutika akilini mwake maisha yote.
"Baada ya siku mbili nilipigiwa simu na kuambiwa nichague kiungo chochote cha mwili wa mwanangu ili nikazike na nisiendelee kuwasumbua. Hapo nilihisi nguvu zote zimeniisha."
Amesema ushauri waliokuwa wakipewa na Polisi ndio uliowasaidia kuendelea kuwa na matumaini.
"Polisi walikuwa wananiambia nisiumie sana, kwamba mtoto anatafutwa kwa umakini mkubwa na atapatikana. Ilikuwa vigumu kuamini wakati huo kwa sababu nilikuwa silali nikimfikiria mwanangu," amesema.
Wakati familia ikiendelea kuishi katika maumivu na sintofahamu, vyombo vya ulinzi na usalama vilikuwa vinaendelea kufanya uchunguzi wa kina na kufuatilia kila nyendo za watuhumiwa.
Hatimaye juhudi hizo zilizaa matunda na mtoto huyo akapatikana akiwa hai na salama, jambo lililoondoa simanzi iliyokuwa imeigubika familia hiyo kwa siku kadhaa.
"Ninamshukuru Mungu na Jeshi la Polisi. Mwanangu amepatikana salama bila majeraha yoyote. Hii ni neema kubwa sana kwetu," anasema Paulo.
Tukio hilo limeibua hisia kali kwa wakazi wa Igunga na maeneo mengine ya Mkoa wa Tabora.
Mkazi wa Tabora, Salum Sizya amesema jamii imeishi katika hofu kubwa tangu kutoweka kwa mtoto huyo na ameomba hatua kali za kisheria zichukuliwe dhidi ya wahusika.
"Tulikuwa tunaishi kwa mashaka makubwa. Hatukutarajia kuona tukio kama hili likitokea katika jamii yetu. Sheria ichukue mkondo wake ili iwe fundisho kwa wengine," amesema.
Naye Asia Juma, mkazi wa Igunga, amesema tukio hilo limeonyesha umuhimu wa jamii kuendelea kulinda na kulea watoto kwa pamoja badala ya kuwageuza kuwa chanzo cha uhalifu.
"Haya si maadili ya jamii yetu. Tunatakiwa kushirikiana katika malezi ya watoto, si kuwateka na kuwafanyia vitendo vya kikatili," amesema.
Mwanamke anaedaiwa kumteka mtoto Paulina akielekea kupanda gari ya polisi
Mtuhumiwa alivyokamatwa
Mkuu wa Mkoa Paul Chacha amesema mwanamke anayehusishwa na tukio la utekaji wa mtoto huyo amekamatwa na Jeshi la Polisi mjini Tabora baada ya operesheni maalumu ya kufuatilia mawasiliano na mienendo yake katika maeneo mbalimbali aliyokuwa akihamia na mtoto huyo.
Amesema uchunguzi uliofanywa na vyombo vya usalama umebaini kuwa mtuhumiwa huyo alisafiri katika maeneo tofauti ikiwemo Kahama na vijiji mbalimbali kabla ya kurejea Tabora, ambako yeye pamoja na wenzake walinaswa kupitia kazi ya intelijensia.
"Baadaye taarifa za kiintelijensia zilionyesha walikuwa wamerejea Tabora, ndipo timu yetu ilipofanikiwa kumkamata yeye pamoja na wenzake," amesema Chacha.
Kwa mujibu wa Chacha, uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa mtuhumiwa alishawishiwa kushiriki utekaji huo na mume wake kwa lengo la kujipatia fedha, baada ya familia yao kukabiliwa na changamoto za kiuchumi.
Amesema watuhumiwa hao walidaiwa kupanga kumteka mtoto huyo na kuomba fedha za fidia kutoka kwa wazazi wake, wakiamini njia hiyo ingewapatia kipato cha haraka cha kukidhi mahitaji yao.
RC Chacha amesema mkoa huo una mfumo madhubuti wa kiintelijensia ambao hauwezi kuruhusu wananchi kuishi kwa hofu kutokana na vitendo vya uhalifu.
"Hatutamruhusu mtu yeyote kuwasumbua wananchi kwa namna yoyote ile. Kila mmoja anapaswa kuishi kwa amani na utulivu," amesema.
Mkuu huyo wa mkoa ameonya kuwa yeyote anayejihusisha au anayefikiria kujihusisha na vitendo vya utekaji, unyang'anyi au uhalifu mwingine atakabiliwa na mkono wa sheria bila huruma.