Baadhi ya waongoza watalii nchini wanavyopiga mabilioni ya fedha Serikali
Muktasari:
- Uhalifu wa mtandaoni unazidi kuongezeka katika mfumo wa malipo wa Serikali. Sasa waongoza watalii wasio waaminifu wanatumia kadi za ulaghai kufanya malipo, jambo ambalo linaikosesha Serikali mapato.
Dar es Salaam. Uhalifu wa mtandaoni unazidi kuongezeka katika mfumo wa malipo wa Serikali na sasa waongoza watalii wasio waaminifu wanatumia kadi za ulaghai kufanya malipo, jambo ambalo linaikosea Serikali mapato.
Vyanzo vya habari hii vimelidokeza gazeti dada la The Citizen kuwa upigaji huo umekuwa ukifichwa kwa muda mrefu kwa sababu taasisi za Serikali zilizolengwa zimeamua kunyamaza kimya ili kulinda hadhi yake.
Hata hivyo, tukio la hivi karibuni lililoukumba Mfumo wa Malipo ya Serikali (GePG) ni la waongoza watalii wasio waaminifu, kudai kufanya miamala yenye thamani ya zaidi ya Dola 1 milioni za Marekani (zaidi ya Sh2.7) kupitia kadi za ulaghai.
Kufuatia tukio hilo, Wizara ya Fedha imeandika barua kwa Chama cha Waongoza Watalii Tanzania (Tato), ikilalamikia baadhi ya waongoza watalii wa Kitanzania wanaofanya miamala ya fedha kwa kutumia kadi za ulaghai.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk Natu Mwamba katika barua yake kwa Tato yenye kumbukumbu MG.233/261/01'A', iliyotolewa Septemba 4, 2024 ikiwa imeambatanishwa na majina ya waongoza watalii wanaotajwa kujihusisha na suala hilo, ameeleza waongoza watalii hao wasio waaminifu waliotajwa kwenye orodha hiyo ya aibu, wamefanya miamala ya zaidi ya Dola 1 milioni za Marekani bila kubainisha kipindi kilichohusika.
Dk Mwamba amesema wasiwasi wake ni udanganyifu huo unaenda kuvuruga jitihada za kukuza utalii na kurahisisha malipo ya Serikali.
Hivyo, ameonya kama hali hiyo haitadhibitiwa, inaweza kuharibu sifa ya sekta ya utalii na kuathiri uchumi wa Tanzania.
Matumizi ya kadi za ulaghai yanaweza pia kusababisha taasisi za kifedha za kimataifa kufikiria upya ushirikiano wao na benki za Tanzania, hali inayoweza kupunguza uwekezaji na kuathiri ukuaji wa uchumi.
“Na kazi kama inafanywa kilaghai inaweza kuzifanya benki za kigeni kuacha kufanya miamala ya fedha hapa nchini, hali ambayo itaathiri huduma za visa na utalii,” amesema Dk Mwamba.
Hata hivyo ameonya kama hali hiyo haitadhibitiwa, itawafanya watalii wenye nia ya kuja Tanzania kuhamia maeneo mengine.
Hivyo, Dk Mwamba ameiomba Tato kuwaonya wanachama wake kuacha kutumia kadi za ulaghai na kurejesha fedha zilizopatikana kinyume cha sheria kwa benki zilizoibiwa.
Anasisitiza umuhimu wa juhudi hizi katika kuunga mkono mipango ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kukuza utalii.
Kauli ya Tato
Katika kujibu, Tato imelaani shughuli za ulaghai zinazodaiwa kufanywa na baadhi ya waongoza watalii wakitumia mfumo wa malipo ya Serikali.
Tato imesema iko tayari kushirikiana na Serikali na Wizara ya Fedha kuwabaini watu hao na kuboresha uadilifu na uwazi wa uendeshaji wa sekta ya utalii.
Mkurugenzi Mtendaji wa Tato, Elirehema Maturo ameishukuru Serikali kwa hatua ya haraka ya kukabiliana na suala hilo.
"Tunashukuru pia kwa kuelezwa kuhusu waongoza watalii waliotumia kadi za ulaghai kufanya malipo ya Serikali," amesema Maturo.
Mwenyekiti wa Tato, Wilbard Chambulo amelaani vikali matendo ya ulaghai ndani ya sekta ya utalii nchini akisema vinaonesha ukosefu wa uzalendo na ni kinyume cha sheria, kanuni na taratibu zinazodhibiti sekta hiyo. Chambulo amesema tabia hizo zinachafua taswira ya sekta ya utalii, ambayo ni muhimu kwa uchumi wa nchi.
"Orodha ya Aibu" iliyotolewa na Serikali inaonyesha kuwa ni kampuni mbili pekee kati ya wanachama hai 323 wa Tato, zilihusishwa katika kashfa hiyo.
Kama hatua ya haraka ya kushughulikia suala hilo, Tato iliwasiliana na kampuni hizo Septemba 5, 2024 na kuwaagiza kufika katika matawi ya benki ili kurekebisha hali hiyo.