Augustine Mrema alivyoacha alama Wizara Mambo ya Ndani

Aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha TLP, Augustine Mrema wakati wa uhai wake akiwa na mkewe, Doreen Kimbi walipohudhuria mkutano mkuu maalumu wa CCM, jijini Dodoma. Picha na maktaba
Muktasari:
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwa bado kwenye mfumo wa chama kimoja, alitokea mtu. Asili yake Kijiji cha Kiraracha, kilichopo Wilaya ya Moshi Vijijini, Kilimanjaro.
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwa bado kwenye mfumo wa chama kimoja, alitokea mtu. Asili yake Kijiji cha Kiraracha, kilichopo Wilaya ya Moshi Vijijini, Kilimanjaro.
Jinsi alivyofanya kazi zake na namna jina lake lilivyosambaa, ikajengeka taswira kwenye vichwa vya wengi kuwa mtu huyo kutoka Kiraracha ni shujaa mwenye nguvu zisizomithilika, yaani superhero.
Nani angeweza kufika kazini asubuhi na kuchukua kiti cha mkuu wa idara kabla mwenye ofisi hajaingia kazini? Mwingine yupi aliyetoa maagizo ya siku saba na nchi ikatetemeka, tena akiwa waziri tu?
Mtu huyo kutoka Kiraracha, akatambulika zaidi kwa jina la Mzee wa Kiraracha. Augustino Lyatonga Mrema ndio mhusika. Imempendeza Mungu asubuhi ya Agosti 21, 2022, iwe nukta yake ya kuvuta pumzi ya mwisho.
Ona sasa, ilibaki siku mbili tu, Mrema angetimiza miezi mitano tangu alipoingia kanisani, Parokia ya Uwomboni, Kiraracha, kufunga ndoa na mke aliyemaliza ngwe ya maisha duniani akiwa naye.
Mrema alifunga ndoa na Doreen Kimbi, Machi 24, 2022. Wakati Mrema anaingia kanisani kupokea Sakramenti ya Ndoa na Doreen, ilikuwa imepita miezi sita iliyotimia tangu kufariki dunia kwa mkewe aliyedumu naye kwa miaka mingi, Rose.
Septemba 16, 2021, alifariki dunia Rose. Mwanamke ambaye Mrema alipata kusimulia umbali waliotoka pamoja kwamba walikutana shule. Mzee wa Kiraracha akiwa mwalimu, Rose mwanafunzi. Baada ya shule, walifunga ndoa.
Kokotoa; tangu Septemba 16, 2021 mpaka Agosti 21, 2022, ni miezi 11 na siku tano. Hivyo, zilibaki siku 26 tu Mtema angeadhimisha mwaka mmoja wa kifo cha Rose wake. Mungu hakupanga hiyo siku ifike. Mrema naye ameitikia wito.
Ndivyo maisha ya binadamu yalivyo; kama mmea huchipua na kustawi, kisha huchanua na kupendeza, hufika muda hunyauka na kufa. Mrema amepita hatua zote hizo.
Mrema alichipua kama ofisa wa usalama wa taifa, akastawi katika siasa. Uwaziri wa Mambo ya Ndani ulimfanya achanue na kupendeza kimamlaka. Ndizo nyakati Mrema alitafsiriwa kama superhero.
Kwa nafasi yake ya uwaziri wa Mambo ya Ndani na Naibu Waziri Mkuu, Mrema aliwahi kulalamikiwa kuingilia mpaka mawaziri wengine. Naye alikuwa na jibu moja tu; kwamba hawakuwa wakifanya kazi vizuri ndio maana aliingilia wizara zao.
Alilivaa sakata la mashamba ya mkonge Tanga na kumshughulikia mfanyabiashara mwenye asili ya Asia, Vidyadhar Girdharlal (V.G.) Chavda. Alivamia Namanga palipo na mpaka wa Tanzania na Kenya, kisha akatoa amri ya maduka 300 yaliyokuwepo yapunguzwe na kubaki 10.
Alihoji; Namanga kulikuwa na wakazi 3,000, maduka 300 yote ya nini? Ina maana kila watu 10 wanahudumiwa na duka moja? Mrema alisema wingi wa maduka Namanga kilikuwa kiashiria cha uhalifu. Mrema alivamia Namanga Januari 5, 1991.
Mrema alipoingia Wizara ya Mambo ya Ndani, alikuta nchi inaliwa hovyo kama “shamba la bibi”. Kulikuwa na kampuni ya Kitanzania iliyokuwa inauza nguo nje ya nchi na kubandika ‘lebo’ kuonesha matengenezo yalikuwa yakifanyika nchini. Wakurugenzi wa kampuni hiyo waliwekwa mahabusu Desemba 1990 kwa amri ya Mrema.
Kuna tukio lililomhusu mwanamke mkazi wa Dodoma, Salome Mazengo. Machi 1991, Salome akiwa na wenzake, walipanda lori kama chombo cha usafiri. Polisi walikamata lori hilo na kulazimisha abiria wote watoe rushwa ili waendelee na safari.
Salome aliwakataza abiria wenzake wasitoe rushwa. Kitendo hicho kiliwaudhi polisi, wakamkamata na kumbambikia kesi. Kesi hiyo ilifika kwa Mrema ambaye alifunga safari kutoka Dar es Salaam mpaka Dodoma.
Pamoja na kubambikiwa kesi, Salome alidai alipoteza mzigo wake wa samaki zenye thamani ya Sh70,000 (zingatia ni Sh70,000 ya mwaka 1991). Fedha nyingi mno wakati huo. Mrema alisimamia Serikali ikampa Salome Sh20,000, kisha akaagiza polisi waliohusika wamalizie deni lililokuwa limesalia, Sh50,000.
Mrema alipokalia kiti cha Wizara ya Mambo ya Ndani, aliunguruma kutoka Dar es Salaam, alipotoa maagizo kwa watu wote waliokuwa wanamiliki bunduki kinyume cha sheria wazisalimishe. Kisha, bunduki zilifukuliwa mpaka makaburini.
Mwanzoni mwa miaka ya 1990, Mrema alianzisha jeshi la ulinzi wa jadi, likaitwa Sungusungu. Matukio ya vibaka na ujambazi yalipungua kwa kiasi kikubwa.
Mrema akawa sababu ya vituo vidogo vya polisi kujengwa maeneo mengi nchini Tanzania. Mpaka hapa ni kuonesha kuwa Mrema alitengeneza alama nyingi ndani ya Wizara ya Mambo ya Ndani.
Ni Mrema pekee ambaye alitajwa kutinga Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, wakati huo ukiitwa Uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam. Akakamata dhahabu zilizotajwa kuwa za aliyekuwa First Lady, Sitti Mwinyi.
Ujasiri na uthubutu wa Mrema haujawahi kulinganishwa na yeyote ndani ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Suala la dhahabu alizokamata uwanja wa ndege liliendelea kuwa tukio la heshima kwake na aliendelea kujinadi nalo hadi katika kampeni za Uchaguzi Mkuu 1995.
Alama za Mrema
Katika maisha yake ya kisiasa, Mrema aliacha alama nyingi. Mosi ni kuwa Tanzania imewahi kuwa na manaibu Waziri Mkuu wawili tu tangu taifa lilipoasisiwa.
Wa kwanza ni Salim Ahmed Salim, ambaye alikuwa Naibu Waziri Mkuu mwaka 1985 mpaka 1989, alipoondoka Baraza la Mawaziri, kwenda kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU).
Kabla ya Uchaguzi Mkuu 1985, Salim alikuwa Waziri Mkuu. Ali Hassan Mwinyi alikuwa Rais wa Zanzibar na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Baada ya Mwinyi kushinda urais wa Tanzania mwaka 1985, ikawa vigumu kikatiba Salim kuendelea kuwa Waziri Mkuu.
Mwinyi na Salim wote ni Wazanzibari, hivyo ilitakiwa Waziri Mkuu atoke Bara ili awe pia Makamu wa Rais. Salim akateuliwa kuwa Waziri wa Ulinzi na Naibu Waziri Mkuu. Jaji Joseph Warioba akawa Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Tanzania.
Naibu Waziri Mkuu wa pili na wa mwisho kuwa naye hadi sasa ni Mzee wa Kiraracha, Mrema. Sio kingine kilichosababisha Mwinyi amteue Mrema kuwa Naibu Waziri Mkuu, zaidi ya uchapakazi na wepesi wa kushughulikia kero za wananchi na matatizo mbalimbali.
Palipokuwa na jambo Mrema alikuwepo, bila kujalisha lilihusu wizara yake au la! Hiyo ndio sababu Mwinyi aliona ili kumtahisishia kazi na asionekane anaingia wizara nyingine, ndipo akampa hadhi ya unaibu Waziri Mkuu.
Mwanazuoni Profesa Issa Shivji, amewahi kusema kuwa watu wengi huogopa kukosoa serikali kwa sababu ya kungoja uteuzi. Miaka 27, Mrema alisimama bungeni na kujipambanua kuwa cheo si muhimu kuliko misingi ya uzalendo.
Februari 1995, Mrema akiwa Waziri wa Kazi, Maendeleo ya Vijana na Michezo, alitoa msimamo wenye kukinzana na ule wa Baraza la Mawaziri kuhusu mfanyabiashara Chavda aliyekuwa na kashfa ya kuchofa fedha serikalini Sh916 milioni kwa ajili ya kuendeleza mashamba ya manne ya mkonge lakini hakufanya hivyo.
Mrema alisema, angeteswa na dhamira yake endapo angekubali kusimama na serikali kuhusu suala la Chavda. Msimamo wa Mrema ni kwamba serikali ndio iliyokuwa inamlea Chavda hadi kuisababishia serikali hasara ya mamilioni ya fedha.
Kila mtu alipigwa na butwaa bungeni Mrema alipokuwa anajenga hoja za kuirudi serikali. Maana alijua alichokuwa anafanya kilikuwa kinakwenda kumfukuzisha kazi. Hata hivyo, mwenyewe aliamua kujilipua. Uzalendo kwa nchi yake ulikuwa muhimu kuliko uwaziri.
Kabla ya kuondoka Wizara ya Mambo ya Ndani mwaka 1994, Mrema alikuwa sauti ya wanyonge na faraja ya akina mama walioteswa na ukatili wa kijinsia nyumbani. Kanga za “Asante Mrema”, zilivaliwa na wanawake kila kona ya nchi.
Mrema daraja la mageuzi
Wakati taifa likielekea kufanya Uchaguzi Mkuu wa kwanza kuhusisha vyama vingi vya siasa tangu nchi ilipopata uhuru, vyama vya upinzani vilionekana vinajitafuta kwa kuungaunga ili kushiriki uchaguzi.
Ghafla, Mrema alibadili upepo. Alijiunga na NCCR-Mageuzi, huku akiapa kuwa kama angerejea CCM, basi angeitwa muongo na mnafiki. Kila mtu anaweza akauzungumza uhusika wa Mrema kwa namna yake. Hata hivyo, hili ni hakika kwamba Mrema aliishi kiapo chake. Hakurejea CCM hadi kifo.
Kujiunga kwa Mrema NCCR-Mageuzi kulifanya siasa za upinzani zipate nguvu. Hapa pia naweza kusema kwa kujiamini kuwa kipindi Mrema anaondoka Baraza la Mawaziri, alikuwa waziri maarufu kuliko mwingine yeyote. Hivyo, kuhamia kwake upinzani lilikuwa pigo kubwa kwa CCM.
Ndivyo ilivyokuwa, alipoingia NCCR, ilibidi safu ya uongozi ibadilike. Mrema akawa Mwenyekiti. Mabere Marando ambaye alikuwa Mwenyekiti, akashuka hadi kuwa Katibu Mkuu. Kisha, Mrema akawa mgombea urais.
CCM ilibidi wafanye kazi ya ziada kumdhibiti Mrema. Mgombea Urais wa CCM, Benjamin Mkapa, hakuwa maarufu japo kufikia nusu ya Mrema. Alitegemea zaidi nguvu ya chama na uwezo wake wa kujenga hoja. Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, aliingia ulingoni kumnadi Mkapa kikamilifu.
Ulifanyika mdahalo wa wagombea urais wote mwaka 1995. Ulifanyika Hoteli ya Kilimanjaro, siku hizi inaitwa Hyatt Regency, The Kilimanjaro. Kila ilipofika zamu ya Mrema, alikuwa hasikiki vizuri. Zamu za wagombea wengine; Mkapa, Profesa Ibrahim Lipumba (Cuf) na John Cheyo (UDP), kipaza sauti kilitoa sauti vema.
Ilidaiwa kuwa kuna mchezo ulifanywa kwenye kipaza sauti kwa makusudi ili Mrema asisikike. Hakika, Mrema hakusikika na kumwacha Mkapa aking’ara vilivyo katika mdahalo akifuatiwa na Lipumba. Kasoro ya sauti ilifanya ushiriki wa Mrema uwe mbovu kuliko wote.
Mrema alishindwa urais, lakini alipata matokeo ambayo rekodi yake ilidumu kwa miaka miaka 20. Mrema alipata asilimia 28 ya kura za urais, akiwa wa pili nyuma ya Mkapa aliyeshinda kwa kuvuna kura asilimia 62.
Mwaka 2015, Edward Lowassa alipogombea urais kupitia Chadema, alipata kura asilimia 40, hivyo kuipiku rekodi ya Mrema. Mgombea urais mwingine wa Chadema, Dk Willibrod Slaa, mwaka 2010, kidogo aifikie rekodi ya Mrema alipopata kura asilimia 27.
Tukirejea mwaka 1995, Mrema alifanikiwa kuiwezesha NCCR-Mageuzi kupata wabunge 17 wa kuchaguliwa kutoka majimbo mbalimbali nchini. Vyama vingine vya upinzani vilivyopata wabunge ni Cuf, Chadema na UDP.
Baada ya Uchaguzi Mkuu 1995, ushindi wa mbunge wa Temeke, Ally Kihiyo, ulipingwa mahakamani, kisha Mahakama ikatengua ubunge wa Kihiyo. Mwaka 1996, Mrema aligombea ubunge katika uchaguzi mdogo akashinda kwa kishindo.
Mwaka 1997, migogoro ilianza kuiandama NCCR-Mageuzi. Vurugu kubwa zilitokea Hoteli ya Raskazone, Tanga, Mei 1997, hali iliyolazimu mlinzi binafsi wa Mrema, marehemu Mohamed Posh, amfiche chini ya meza bosi wake huyo ili kumnusuru na mashambulizi.
Migogoro iliendelea kuisulubu NCCR-Mageuzi mpaka mwaka 1999, Mrema alipojiondoa na kujiunga na TLP. Tangu kupokea kadi ya TLP na kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti, Mrema alidumu na chama hicho pamoja na cheo chake mpaka umauti ulipomchukua.
Mrema alipoondoka NCCR-Mageuzi, alikuwa bado hajamaliza deni la mkopo wa gari. Wananchi kutoka kona mbalimbali za nchi walijitolea kumchangia na kumlipia deni hilo.
Uchaguzi Mkuu 2000, Mrema aligombea tena urais kupitia TLP, akatoka wa tatu nyuma ya Mkapa (CCM) na Lipumba (Cuf). Mwaka 2005, aligombea na kutoka wa nne, nyuma ya Jakaya Kikwete (CCM), Lipumba (Cuf) na Freeman Mbowe (Chadema).
Uchaguzi Mkuu 2010, Mrema aligombea ubunge jimbo la Vunjo na kushinda. Baada ya kuingia bungeni, alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC).
Uchaguzi Mkuu 2015 na 2020, Mrema alifanya majaribio ya kurejea bungeni bila mafanikio. Hata hivyo, kwa muda mrefu Mrema alikuwa akishutumiwa kwa kutokuwa na msimamo thabiti wa upinzani.
Uchaguzi Mkuu 2015, Mrema alimwombea kura mgombea urais wa CCM, Dk John Magufuli licha ya chama chake (TLP), kuwa na mgombea urais, Machmillan Lymo. Baada ya uchaguzi, Mrema alisema aliahidiwa kupewa kazi na Magufuli.
Mwaka 2016, Magufuli alimteua Mrema kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Parole. Januari 2020, Mrema akiteuliwa kuendelea na cheo hicho. Alidumu nacho mpaka umauti ulipomfika.
Pamoja na kushutumiwa kutokuwa na msimamo thabiti wa upinzani, Mrema alikuwa mmoja wa waliolalamikia Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2019 na Uchaguzi Mkuu 2020, kwamba haukuendeshwa kwa haki.
Mrema mpambanaji
Kati ya mwaka 1995 na 2000, Mrema alidhihirika kuwa na msuli mkubwa mno na ilikuwa dhahiri kwamba angegombea ubunge jimbo lolote wakati huo angeweza kushinda kutokana na nguvu kubwa ya ushawishi aliyokuwanayo.
Kukosa urais na kugombea ubunge ni alama kubwa kwamba alikuwa mpambanaji. Hata safari yake ya kuingia bungeni kwa mara ya kwanza ilihusisha mapambano hadi mahakamani.
Mrema alitia nia ya kugombea ubunge Moshi Vijijini kwa mara kwanza mwaka 1985. Hata hivyo, alipingwa na kuondolewa. Mrema alikwenda mahakamani kutetea haki yake ya kuwa mgombea ubunge. Mwaka 1987, Mahakama ilitoa hukumu yenye kuhalalisha Mrema kugombea cheo chochote.
Mwaka 1990, Mrema alishinda ubunge Moshi Vijijini na kudumu na cheo hicho mpaka mwaka 1995 alipovuliwa uanachama wa CCM.
Alipoondoka CCM kuna waliombeza kuwa alikosa sifa ya kuwa na shahada moja ya chuo kikuu ambacho kilikuwa kigezo cha CCM kumpata mgombea urais wake.
Mrema atakumbukwa pia bungeni kwa jinsi alivyokuwa mstari wa mbele kuibua mabomu mazito dhiri ya Serikali.