Atupwa jela miaka 20 kwa kosa la shambulio la aibu kwa mtoto

Muktasari:
- Hukumu hiyo imesomwa jana Aprili 14, 2025, mbele ya Makimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Kyela, Andrew Njau baada ya kumtia hatiani mshtakiwa.
Mbeya. Mkazi wa Kijiji cha Busale, Wilaya ya Kyela mkoani Mbeya, Emmanuel Uswege (30) amehukumiwa kifungo cha miaka 20 jela kwa kosa la kufanya shambulio la aibu kwa mtoto wa miaka mitano.
Hukumu hiyo imesomwa jana Aprili 14, 2025, mbele ya Makimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Kyela, Andrew Njau baada ya kumtia hatiani mshtakiwa.
Imeelezwa mahakamani hapo na mwendesha mashataka mkaguzi wa msaidizi wa Polisi, Bihemo Mayengela kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo Januari 16, 2025 katika Kijiji cha Busale.
Mayengela amesema siku ya tukio, mshtakiwa alikutwa akiwa na watoto wawili ambapo mmoja kati yao alikuwa akimfanyia shambulio la aibu.
Mahakama imemtia hatiani baada ya ushahidi kutolewa, huku mwendesha mashtaka akiomba adhabu kali itolewa ili iwe fundisho kwa watu wengine na kukomesha vitendo vya ukatili wa kijinsia na unyanyasaji dhidi ya watoto.
Amesema mshtakiwa ametiwa hatiani kwa mujibu wa kifungu cha sheria 138(C), kifungu kidogo cha 1(a) na cha 2(b) vya Sheria ya Kanuni ya Adhabu sura ya 16 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2022.
Kufuatia maelezo na ushahidi uliotolewa na pande zote, Hakimu Njau alimhukumu mshtakiwa kutumikia miaka 20 jela baada ya kukutwa na hatia.
Hata hivyo, mshtakiwa alipopewa nafasi ya kujitetea, aliiomba Mahakama kumpunguzia adhabu, ombi ambalo lilitupiliwa mbali.
Wakati huohuo, Mahakama ya Wilaya ya Chunya imemhukumu kifungo cha maisha jela, Said Kandonga (60) kwa kosa la kumbaka mtoto wa miaka tisa (jina limehifadhiwa).
Hukumu hiyo imesomwa na Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, James Mhanuzi, Aprili Mosi, 2025 baada ya kuridhishwa na ushahidi ukiotolewa.
Awali, mwendesha mashataka wa Serikali, Wakili Mwajabu Tengeneza alieleza mahakamani hapo kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo Septemba 16, 2024.
Amesema upande wa Jamhuri umemtia hatiani mshtakiwa baada ya kuridhika na ushahidi uliotolewa pasipo shaka.
Amesema siku ya tukio, mshtakiwa aligundua nyumbani kwa mwathirika, wazazi wake walikuwa hawapo, ndipo alimkamata na kumbaka ambapo baadaye wazazi wake walimkuta akiendelea na tendo hilo.