Askofu Niwemugizi, Bagonza wasema chanjo ni salama

Muktasari:
- Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Rulenge-Ngara, Severine Niwemugizi pamoja na Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Karagwe, Dk Benson Bagonza leo Agosti 6, 2021 wameungana na wakazi wa wilaya hizo kupata chanjo ya Covid-19.
Mwanza. Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Rulenge-Ngara, Severine Niwemugizi pamoja na Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Karagwe, Dk Benson Bagonza leo Agosti 6, 2021 wameungana na wakazi wa wilaya hizo kupata chanjo ya Covid-19.
Viongozi hao wa kiroho wamefichua kuwa chanjo hiyo ni salama baada ya kuhakikishiwa na watalaamu wa afya wa ndani na nje ya Tanzania. Pia, wamesema kuwa kinachofanyika kwa sasa ni vita ya kibiashara ya kampuni kubwa.

Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Rulenge-Ngara, Severine Niwemugizi
Wakati Askofu Niwemugizi akipata chanjo katika kituo cha hospitali ya Wilaya Ngara -Nyamiaga, Dk Bagonza amechanjwa katika Hospitali teule ya Wilaya ya Karagwe, Nyakahanga.
Kupitia ukurasa wake wa Facebook, Dk Bagonza amesema amechanjwa akiwa wa kwanza katika hospitali hiyo huku akitaja sababu zilizomfanya achanjwe kuwa ni kuridhika na maelezo aliyopewa na madaktari wa ndani ya nchi na nje ya nchi wakiwemo kutoka Marekani, Ulaya na Canada wakati akifanya utafiti kuhusu chanjo hiyo.
“Vita ya kibiashara kwa kampuni kubwa ni ya muda wote kwa bidhaa zote. Wanaokuuzia vazi la kuzuia risasi, kesho wanatengeneza risasi ya kupenya tishirt waliyokuuzia jana,” ameandika na kuongeza:
“Chanjo ya Jensen inazuia kupata corona kwa asilimia 66. Ikitokea ukapata corona, chanjo hii inazuia kwa asilimia 86 usiingie katika ugonjwa mkali. Na chanjo hii inazuia kifo cha corona kwa asilimia 100.”
Amesema: “Mimi nimeridhika. Una hiari ya kuamua unavyopenda.”
Katika ukurasa wake huo, Dk Bagonza amesema amewahi kuugua corona kwenye wimbi la kwanza, kuzika wengi na kuifanya ratiba yake kujaa kwa wiki nzima mbele kwa ajili ya kuzika.
“Nimechagua kufa kesho siyo leo,”ameandika Dk Bagonza.
Akizungumza kwa njia ya simu na Mwananchi, Askofu Niwemugizi amesema ameamua kuchanja kama wataalamu wa afya walivyoelekeza ili hata akipata virusi vya corona asiangaike sawa na watakavyoangaika ambao hawatochanja.
Soma zaidi hapa: Wataka Serikali itoe takwimu za corona
“Mungu ametupa akili ya kutunza uhai wetu, nami natumia wataalamu wa afya kulinda uhai wangu, ” amesema Askofu Niwemugizi.