Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Askofu Mkuu Ruwa'ichi ataka waamini kufundishwa kuhusu mafuta matakatifu

Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mhashamu Jude Thaddaeus Ruwa`ichi (mwenye Bakora ya Kiaskofu), wakati akiingia katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Yosefu, kuelekea Adhimisho la Sadaka ya Misa Takatifu ya kuweka wakfu Krisma Takatifu na kubariki Mafuta ya Wagonjwa na Wakatekumeni leo Jumanne Aprili 15, 2025.

Muktasari:

  • Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Jude Thaddeus Ruwa'ichi amesema mapadri washiriki kuwafunza waamini ili wasirubuniwe kuhusu mafuta matakatifu.

Dar es Salaam. Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Jude Thaddeus Ruwa'ichi amesema waumini wanapaswa kufundishwa katekesi ili kuwa na uelewa sahihi kuhusu mafuta matakatifu ili wasirubuniwe.

Amesema hayo leo Aprili 15, 2025 katika misa ya kuweka wakfu krisma ya wokovu na kubariki mafuta matakatifu ya wagonjwa na wakatekumeni katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Yosefu, Dar es Salaam.

Askofu Ruwa'ichi amesema ili waamini waelewe matumizi ya mafuta hayo wanahitaji kufundishwa katekesi, kazi ambayo ameeleza hapaswi kuachiwa katekista pekee bali mapdri washiriki kufundisha.

Amesema mafuta matakatifu yanabarikiwa siku ya Alhamisi Kuu na anayepaswa kupaka wagonjwa ni padri na askofu na si watu wengine.

"Hao wanaokuambia njoo nikupake mafuta upone wanakurubuni hawana mamlaka wala madaraka ya kukupaka mafuta ya wagonjwa,” amesema.

Amesema mafuta yaliyowekwa wakfu yatatumika ndani ya kanisa kwa mpangilio sahihi na stahiki na si kwenda kupakana uraiani.

Mafuta yaliyobarikiwa ni ya wagonjwa ambayo hutumika katika sakramenti ya mpako wa wagonjwa ambayo hutolewa kwa wagonjwa walio katika hatari kubwa, kwa kuwapaka usoni na mikononi.

Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mhashamu Jude Thaddaeus Ruwa`ichi (mwenye Bakora ya Kiaskofu), Askofu Mkuu Angelo Accattino - Balozi wa Baba Mtakatifu nchini Tanzania (katikati), Askofu Stephano Musomba wa Jimbo Jipya Katoliki Bagamoyo na Askofu Msaidizi, Henry Mchamungu wakiandamana kuingia katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Yosefu, kuelekea Adhimisho la Sadaka ya Misa Takatifu ya kuweka wakfu Krisma Takatifu na kubariki Mafuta ya Wagonjwa na Wakatekumeni leo Jumanne Aprili 15, 2025.

Mengine ni ya wakatekumeni ambayo ni ishara ya nguvu ya Kristo Yesu kwa waamini wanaojiandaa kupokea sakramenti ya ubatizo ili waweze kupata uwezo wa kupambana na vishawishi pamoja na dhambi.

Pia, yamewekwa wakfu mafuta ya krisma ya wokovu yanayotumika kuwapaka waamini wanapopokea sakramenti za ubatizo, kipaimara na wanapowekwa wakfu mapadre na maaskofu.

Hutumika pia kutabaruku kanisa kwa kupaka altare na kuta kuonyesha kwamba jengo (yaani kanisa) limetengwa kwa ajili ya maadhimisho ya mambo matakatifu ya Mungu.

Misa hiyo pia ililenga kumshukuru Mungu kwa Jimbo la Bagamoyo na kuwaaga mapadri ambao parokia zao zimeangukia Bagamoyo.

Papa Francis Machi 7, 2025 aliunda Jimbo Katoliki la Bagamoyo, nchini Tanzania, akimteua Askofu Stephano Musomba kuwa wa kwanza kuliongoza.

Kabla ya uteuzi huo, Musomba alikuwa Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, uteuzi uliofanywa na Papa Francis Julai 7, 2021 na aliwekwa wakfu kuwa askofu Septemba 21, 2021.

Jimbo jipya la Bagamoyo limeundwa kwa kuligawa Jimbo Kuu la Dar es Salaam na Jimbo la Morogoro. Kanisa Kuu la Jimbo Katoliki la Bagamoyo ni Kanisa la Moyo Safi wa Bikira Maria, lililoko mjini Bagamoyo.

Kwa mujibu wa taarifa ya mtandao wa Vatican News, Jimbo Katoliki la Bagamoyo linakuwa na parokia 22, mapadri wa Jimbo wanane, mapadri watawa 37 na watawa wanane.

Askofu Mkuu Ruwa'ichi Machi 7, alitaja parokia zilizomegwa kutoka jimbo hilo kwenda Bagamoyo kuwa ni Bahari Beach, ⁠Boko, ⁠Bunju,⁠ Kinondo, ⁠Madale, Mbopo, ⁠Mbweni Mpiji, Mbweni  Teta, ⁠Mbweni, ⁠Mivumoni, ⁠Muungano, Nyakasangwe, ⁠Tegeta Kibaoni, ⁠Tegeta, Ununio, ⁠Wazo na ⁠Mbweni JKT (Parokia Teule).

Alisema mapadri waliopo kwenye parokia hizo na waumini wake watakuwa Jimbo la Bagamoyo chini ya uongozi mpya wa jimbo hilo na si kwake tena.