Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Askofu Laizer asimikwa kuwa msaidizi wa Askofu KKAM

Mchungaji Jeremia Laizer (kulia)

Muktasari:

Mchungaji Laizer aliyekuwa Mkuu wa Jimbo la Magharibi amesimikwa rasmi leo Juni 30, 2025 katika Kanisa la KKAM Dayosisi ya Arusha Jimbo la Magharibi katika Parokia ya Mto wa Mbu.

Arusha. Kanisa la Kilutheri Afrika Mashariki (KKAM) limemsimika na kumuingiza kazini Mchungaji Jeremia Laizer, kuwa msaidizi wa Askofu Mkuu Dayosisi ya Arusha.

Mchungaji Laizer aliyekuwa Mkuu wa Jimbo la Magharibi amesimikwa leo Juni 30, 2025 katika Kanisa la KKAM Dayosisi ya Arusha Jimbo la Magharibi katika Parokia ya Mto wa Mbu.

Akimsimika Mchungaji Laizer, Askofu Mkuu wa Kanisa la KKAM Dayosisi ya Arusha, Dk Philemon Mollel 'Monaban' amesema kuwa kuapishwa kwa kiongozi huyo kunaongeza jeshi la utumishi wa Mungu katika kuliombea Taifa libaki na amani hasa kipindi hiki cha Uchaguzi Mkuu.

“Kuwa na viongozi wengi wa dini kunaongeza nguvu ya kutumikia Taifa letu la Tanzania, hasa katika maombi ya kuhakikisha vurugu zinazoendelea katika nchi zingine zisisambae katika Taifa letu bali tubaki na amani, utulivu na tuboreshe zaidi ushirikiano,” amesema.

Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Monduli, Salum Kali amewataka viongozi hao kutumia muda mwingi kuliombea Taifa kupata viongozi wenye mapenzi mema na wananchi hasa moyo wa kuwatumikia na sio kujitumikia wenyewe.

“Matukio ya uchaguzi katika nchi nyingi imekuwa chanzo cha machafuko, hivyo nitumie nafasi hii kuwaomba viongozi wa dini muongeze juhudi katika maombi ya amani, upendo na mshikamano katika nyakati hizi ambazo nchi yetu imeanza mchakato wa Uchaguzi Mkuu”.

“Lakini pia msiache kuomba kwa ajili ya watia nia wetu, ili Mungu akaguse mioyo yao na kuona dhamira yao ili atupatie viongozi wenye wito, waadilifu na wenye mapenzi mema ya kutumikia na kutatua kero za wananchi sio wa kuja kujitumikia wenyewe,” amesema Kali.

Awali akihubiri katika ibada hiyo, Askofu Mkuu wa kanisa la KKAM Tanzania, Oscar John Ulotu amewataka Wakristo nchini kujiepusha na matukio ya ukatili ambayo yamekuwa yakishamiri nchini.

Akizungumza baada ya kusimikwa, Askofu Laizer amesema kuwa hatua hiyo inazidisha moyo wake wa kufanya kazi ya kumtumikia Mungu na kuomba viongozi wengine kuwa na ushirikiano.

“Naombeni msaada wenu kwani peke yangu sitaweza, na muwe mnaniombea niimudu kazi hii ya kumtumikia Mungu katika kutekeleza majukumu yote yaliyo ndani yangu, msigeuke chanzo cha majuto, malalamiko wala manung’uniko yangu,” amesema.