Anayedaiwa kusafirisha kobe 116 kuendelea kusota rumande hadi Julai 23
Mshtakiwa, Orga Kryashtop ambaye ni raia wa Ukraine anayekabiliwa na kesi ya kusafirisha kobe 116, akiwa chini ya ulinzi wa askari Magereza katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu. Picha na Hadija Jumanne
Muktasari:
- Orga Kryashtop, ambaye ni raia wa Ukraine, anakabiliwa na mashtaka mawili likiwemo la kusafirisha Kobe 116 wenye thamani ya Sh18.9 milioni, bila kuwa na kibali.
Dar es Salaam. Raia wa Ukraine, Orga Kryashtop, anayekabiliwa na mashtaka mawili ikiwemo la kusafirisha kobe 116, wenye thamana ya Sh18.9 milioni, ataendelea kubaki rumande hadi Julai 23, 2026 kesi yake itakapotajwa.
Hatua hiyo inatokana na upelelezi wa kesi hiyo kutokukamilika.
Wakili wa Serikali Mwandamizi, Thawab Issa ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, leo Jumanne, Juni 23, 2026 wakati kesi hiyo ilipotajwa.
Wakili Issa ametoa taarifa hiyo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Rahim Mushi.
"Jamhuri bado inaendelea na uchuguzi dhidi ya kesi hii, hivyo tunaomba mahakama itupangie tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa na kuangalia iwapo upelelezi umekamilika au laa" alidai wakili Issa
Hakimu Mushi baada ya kusikiliza taarifa hiyo, alikubaliana na ombi la upande wa jamhuri na kuahirisha hadi Julai 23, 2026 kwa kutajwa.
Mshtakiwa amerudishwa rumande baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kuzuia dhamana.
Mshtakiwa, Orga Kryashtop ambaye ni raia wa Ukraine anayekabiliwa na kesi ya kusafirisha kobe 116, akiwa chini ya ulinzi wa askari Magereza katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu. Picha na Hadija Jumanne
DPP aliwasilisha maombi ya kuzuia dhamana mahakamani hapo Julai 12, 2023, baada ya mshtakiwa kuruka dhamana katika kesi nyingine iliyofunguliwa nje ya nchi.
Inadaiwa kuwa mshtakiwa kabla ya kupelekwa katika Mahakama ya Kisutu na kufunguliwa kesi hiyo, alishawahi kufunguliwa kesi nyingine huko nchini Thailand na baada ya kupewa dhamana, aliruka dhamana.
Baada ya kuruka dhamana mshtakiwa alikimbia na askari wa Interpol wakishirikiana na vikosi vingine walifanikiwa kumkamata nchini Bulgaria na kisha kumleta Tanzania ambapo alifunguliwa kesi hiyo.
Hata hivyo, wakati Kryashtop anafunguliwa kesi hiyo upande wa mashtaka hawakuwa wanajua kama mshtakiwa alisharuka dhamana kwenye kesi nyingine, hadi hapo walipopata taarifa kutoka jeshi la Polisi.
Kwa mara ya kwanza, mshtakiwa alifikishwa mahakamani hapo Juni 19, 2023 na kusomea mashtaka yake.
Katika kesi ya msingi, mshtakiwa anadaiwa kati ya Januari Mosi hadi Julai 30, 2022 jijini Dar es Salaam, mshitakiwa alijihusisha na nyara za serikali kwa kununua, kuuza na kusafirisha kobe 116 wenye thamani ya Sh18,935,840 mali ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Shtaka la pili, inadaiwa katika tarehe hizo, katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) uliopo wilaya ya Ilala, Kryshtop alikamatwa akiwa na kobe hao bila kuwa na kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa Wanyama Pori nchini.