Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Aliyeua mke bila kukusudia jela miaka mitano

Muktasari:

  • Paulo John mkazi wa Kijiji cha Msazi, Wilaya ya Kalambo mkoani Rukwa alishtakiwa kwa kosa la kumuua mkewe Helena Elias kwa kumchapa na fimbo sehemu mbalimbali za mwili wake, ikiwemo kichwani, mgongoni na miguuni baada ya mke huyo kumtuhumu kuwa na mahusiano ya kimapenzi na wanawake wengine.

Arusha. Mahakama Kuu Masijala Ndogo ya Sumbawanga imemhukumu adhabu ya kifungo cha miaka mitano jela, Paulo John (40), baada ya kumkuta na hatia ya kumuua mkewe Helena Elias, bila kukusudia.

Hukumu hiyo imetolewa Machi 3, 2025 na Jaji Abubakar Mrisha na nakala yake kupatikana jana kwenye mtandao wa mahakama.

Paulo alikutwa na hatia baada ya kukiri mwenyewe kuua bila kukusudia kinyume na kifungu cha 195 na 198 cha Kanuni ya Adhabu.

Ilidaiwa na upande wa mashtaka kuwa Novemba 4, 2024, katika Kijiji cha Msazi Wilaya ya Kalambo mkoani Rukwa, mshitakiwa alisababisha kifo cha mkewe ambaye alikuwa akiishi naye.

Siku ya tukio ilidaiwa mshtakiwa alifika nyumbani akiwa amechelewa ambapo alikuwa amemletea dawa mkewe aliyekuwa anaumwa, lakini baada ya Helena kupewa dawa hizo, alianza kumtuhumu mumewe kuwa na mahusiano ya kimapenzi na wanawake wengine.

Ilidaiwa wawili hao walirushiana maneno ambayo yalizua mzozo baina yao, ndipo mshitakiwa alichukua fimbo na kumpiga mkewe, kitendo ambacho kilimfanya apige kelele na majirani walipofika walimkuta Helena na majeraha mengi kichwani, mgongoni na miguuni.

Kwa mujibu wa maelezo mashahidi, hata baada ya majirani kumuwahisha Helena katika Zahanati ya Mao kwa ajili ya matibabu, hawakuweza kuokoa maisha yake kwa kuwa alikuwa amekwisha fariki dunia, tukio likaripotiwa mamlaka ya Serikali za Mtaa na kisha mtuhumiwa akakamatwa.

Uchunguzi wa mwili wa marehemu ulifanyika na kubaini kuwa chanzo cha kifo ni kutokwa na damu na majeraha makubwa ya ubongo.

Ilidaiwa baada ya mshtakiwa kuhojiwa alikiri kutenda kosa hilo bila kukusudia na upelelezi ulipokamilika alishtakiwa kwa kosa la kuua bila kukusudia.

Upande wa jamhuri uliongeza kuwa mwili wa marehemu ulikutwa na majeraha mengi ambayo yanaashiria kuwa alipigwa na alishindwa kujitetea na kuwa kitendo alichofanya mtuhumiwa kwa mkewe kilikuwa cha kinyama na hakikubaliki kwa jamii nzima.

Paulo katika utetezi wake aliiomba mahakama kumpunguzia adhabu kwani ni baba wa watoto wanane wanaomtegemea na mmoja wao ni mlemavu anayehitaji mwongozo maalumu wa baba yake, ni nguvu kazi ya Taifa na anajutia alichokifanya.


Atiwa hatiani

Jaji Mrisha amesema mahakama ilimkuta mshitakiwa huyo na hatia ya kosa la kuua bila kukusudia n ahata upande wa jamhuri ulidai mshtakiwa hana kumbukumbu za uhalifu, ila ulisisitiza apewe adhabu kali kwa sababu alimpiga marehemu kwenye sehemu nyeti ya mwili wake.

“Hapana shaka mshitakiwa huyo aliyetajwa ndiye anayehusika na kosa la mauaji ya Helena na kwa msingi huo hakuna namna yoyote anayoweza kujiepusha na madhara ya kuadhibiwa kutokana na hatia yake, kama ilivyoelezwa hapo juu,” amesema.

Hata hivyo, baada ya kuzingatia mambo yote mawili ya kuzidisha na kupunguza, ni maoni yangu kuwa mshtakiwa ni mkosaji wa kwanza na mtu ambaye amekiri shitaka dhidi yake, hivyo anastahili kupewa hukumu ndogo,”

Jaji Mrisha amesema hata hivyo, hiyo haimaanishi kitendo chake cha kusababisha kifo cha marehemu kilikuwa halali, bali kutokana na mazingira yaliyokuwapo ya utendaji wa kosa aliloshitakiwa, pamoja na sababu nyingine, ni maoni yake kwamba mshtakiwa anastahili adhabu hiyo ya miaka mitano jela ili imrekebishe.