Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Aliyeshtakiwa kwa kusafirisha mirungi kilo 116.69 aachiwa huru

Muktasari:

  • Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Moshi, imemuachia huru Nestory Machibya aliyekuwa ameshtakiwa kwa kosa la kusafirisha dawa za kulevya aina ya mirungi zenye uzito wa kilo 116.69, baada ya kubaini kuwa upande wa mashtaka haukuthibitisha kosa hilo bila kuacha shaka na hati ya mashtaka ilikuwa na kasoro za kisheria.

Simanjiro. Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Moshi imemuachia huru Nestory Machibya, aliyekuwa akikabiliwa na shtaka la kusafirisha dawa za kulevya aina ya mirungi zenye uzito wa kilo 116.69, baada ya kubaini kuwa upande wa mashtaka haukuthibitisha kosa hilo kwa kiwango kinachotakiwa kisheria.

Uamuzi huo ulitolewa Mei 29, 2026 na Jaji Safina Simfukwe katika kesi ya uhujumu uchumi namba 18604/2024, iliyokuwa ikimkabili mshtakiwa huyo kwa kosa la usafirishaji haramu wa dawa za kulevya.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, Julai 6, 2023 katika Kijiji cha Rikweni wilayani Same, mkoani Kilimanjaro, Machibya alidaiwa kukutwa akisafirisha dawa hizo kinyume cha sheria.

Katika kuendesha kesi hiyo, upande wa mashtaka uliwasilisha mashahidi sita na vielelezo tisa, huku mshtakiwa akiwa shahidi pekee wa utetezi.

Mahakama ilielezwa kuwa maofisa wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), walifanya operesheni ya kumkamata mshtakiwa baada ya kupokea taarifa kutoka kwa mtoa habari aliyedai kuwa alikuwa akijihusisha na kilimo na biashara ya mirungi.

Kwa mujibu wa ushahidi wa mashahidi wa mashtaka, maofisa hao walimkamata Machibya katika eneo la Rikweni na baadaye kudai kuwa aliwaongoza hadi shambani kwake ambako walikuta mifuko minne ya salfeti iliyokuwa imehifadhi majani mabichi yaliyoshukiwa kuwa dawa za kulevya.

Mahakama ilielezwa kuwa baada ya kukamata mizigo hiyo, maofisa waliweka alama maalumu kwenye mifuko, wakachukua sampuli na kuziwasilisha kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kwa uchunguzi wa kisayansi.

Ripoti ya uchunguzi wa maabara ilibaini kuwa majani hayo yalikuwa dawa za kulevya aina ya mirungi zenye uzito wa kilo 116.69. Baadaye dawa hizo ziliharibiwa kwa kuchomwa moto kwa amri ya mahakama kutokana na asili yake ya kuharibika kwa haraka.

Katika utetezi wake, Machibya alikana kuhusika na dawa hizo, akidai kuwa alikamatwa akiwa kwenye mazishi ya baba mkwe wake katika kijiji cha Heikonti wilayani Same pamoja na watu wengine kadhaa.

Alidai kuwa hakuwahi kuwaongoza maofisa wa DCEA kwenda kijiji cha Rikweni wala kuonyesha eneo lolote lililokuwa na dawa za kulevya. Pia alikana kuwepo wakati wa uharibifu wa vielelezo na kusisitiza kuwa hakufahamu chochote kuhusu mifuko ya salfeti iliyowasilishwa mahakamani.

Wakili wa utetezi, Desiderius Hekwe, aliiomba mahakama imuondolee mashitaka mteja wake akidai kuwa hati ya mashtaka ilikuwa na kasoro za kisheria.

Alisema shtaka lililomkabili mshtakiwa halikufafanua kwa uwazi namna alivyodaiwa kujihusisha na biashara haramu ya dawa za kulevya, hali iliyomnyima fursa ya kuandaa utetezi wake ipasavyo.

Kwa mujibu wa wakili huyo, sheria inataka shtaka lieleze wazi kama mtuhumiwa alihusika kuuza, kuhifadhi, kumiliki, kusambaza au kusafirisha dawa hizo, badala ya kutumia maelezo ya jumla yanayoweza kuleta mkanganyiko.

Pia alipinga utaratibu uliotumika katika upekuzi na ukamataji wa vielelezo, akidai kuwa masharti ya kisheria yanayohusu uwepo wa shahidi huru hayakuzingatiwa.


Mahakama ilivyofikia uamuzi

Katika uchambuzi wake, Jaji Simfukwe alikubaliana na hoja ya utetezi kwamba hati ya mashtaka ilikuwa na kasoro kwa kushindwa kubainisha kwa uwazi aina ya kitendo cha biashara haramu ambacho mshtakiwa alidaiwa kutekeleza.

Alisema maelezo ya shtaka yalieleza tu kuwa mshtakiwa alipatikana akisafirisha dawa za kulevya bila kufafanua mazingira na namna ya usafirishaji huo kama inavyotakiwa na sheria.

Kwa mujibu wa jaji huyo, kasoro hiyo ilikuwa na madhara kwa kuwa ilimnyima mshtakiwa nafasi ya kuelewa kikamilifu tuhuma zinazomkabili na hivyo kuathiri haki yake ya kujitetea.

Mahakama pia ilibaini mapungufu katika zoezi la upekuzi na ukamataji wa dawa hizo baada ya kubaini kuwa ofisa mmoja wa DCEA aliyeshiriki operesheni hiyo ndiye aliyekuwa shahidi wa upekuzi.

Jaji Simfukwe alisema mtu aliyeshiriki operesheni ya ukamataji hawezi kutambulika kama shahidi huru kwa sababu tayari ana masilahi katika matokeo ya operesheni hiyo.

“Shahidi huru anatakiwa kuwa mtu asiye na masilahi yoyote katika shauri husika na ambaye ushahidi wake unaweza kuaminika kuwa haujaathiriwa na upendeleo,” alieleza Jaji wakati akitoa hukumu hiyo.

Aidha, mahakama ilibaini dosari katika mchakato wa kuharibu dawa za kulevya zilizokamatwa.

Ingawa mashahidi wa upande wa mashtaka walidai kuwa mshtakiwa aliulizwa kama alikuwa na pingamizi kuhusu uharibifu wa vielelezo na akajibu kuwa hana, mahakama iliona kuwa jambo hilo halikuandikwa katika nyaraka rasmi za uharibifu.

Jaji alisema sheria na maamuzi ya mahakama za juu yanataka maoni ya mtuhumiwa kuhusu uharibifu wa vielelezo yawekwe katika kumbukumbu rasmi ili kuondoa mashaka kuhusu uhalali wa mchakato huo.

Alisisitiza kuwa baada ya vielelezo kuharibiwa, nyaraka zinazohusiana na uharibifu wake hubaki kuwa ushahidi muhimu mahakamani, hivyo zinapaswa kuandaliwa kwa kuzingatia taratibu zote za kisheria.

Hata hivyo, pamoja na mapungufu hayo, mahakama ilikubaliana na ushahidi wa Mkemia Mkuu wa Serikali kuwa majani yaliyokamatwa yalikuwa dawa za kulevya aina ya mirungi.

Mahakama ilisema upande wa mashtaka ulifanikiwa kuthibitisha kuwa majani yaliyokamatwa yalikuwa mirungi, lakini haukuweza kuthibitisha bila kuacha shaka kuwa dawa hizo zilikuwa chini ya usimamizi au udhibiti wa mshtakiwa kama ilivyodaiwa.

Kutokana na kasoro zilizobainika katika hati ya mashtaka pamoja na mapungufu katika mchakato wa upekuzi na uharibifu wa vielelezo, mahakama ilihitimisha kuwa ushahidi uliowasilishwa haukufikia kiwango kinachohitajika kuthibitisha hatia katika kesi ya jinai.

“Upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha bila shaka yoyote kwamba mshtakiwa alifanya biashara haramu ya dawa za kulevya kama alivyoshtakiwa,” alisema Jaji Simfukwe katika hukumu yake.

Kutokana na sababu hizo, Mahakama Kuu ilimtangaza Machibya kuwa hana hatia na kuamuru aachiwe huru mara moja isipokuwa kama anashikiliwa kwa sababu nyingine halali za kisheria.