Aliyekatia rufaa kifungo cha nje, atupwa gerezani

Muktasari:
Mahakama Kuu imeamuru atumikie kifungo cha miaka mitatu jela baada ya kutengua hukumu ya Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoa wa Dar es Salaam, Kisutu, iliyomhukumu adhabu hiyo ya kiufungo cha nje cha miezi 18 akifanya kazi za kijamii.
Dar es Salaam. Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imembadilishia adhabu aliyekuwa mmoja wa wamiliki wa Mikocheni Shopping Mall Ltd, John Kyenkungu kutoka kifungo cha nje cha miezi 18 na kuwa kifungo cha miaka mitatu jela, baada ya rufaa yake kutupwa na ile ya Serikali kukubaliwa.
Hukumu hiyo ya Mahakama Kuu ilitolewa mwisho wa Desemba 2023 na Jaji Griffin Mwakapeje, kufuatia rufaa aliyoikata Kyenkungu akipinga hukumu ya Mahakama ya Kisutu.
Hata hivyo, Kyenkungu amekimbilia Mahakama ya Rufani kukata rufaa kupinga hukumu hiyo ya Mahakama Kuu.
Wakili wake, Derick Kahigi ameliambia Mwananchi kuwa tayari wameshaanza mchakato wa rufaa hiyo.
"Tumeshachukua hatua za awali za kuwasilisha notice of appeal (taarifa ya kusudio la kukata rufaa). Kwa hiyo tutawasilisha sababu za rufaa na tunatarajia kuwa tutaziwasilisha Januari baada ya kupata nyaraka za kukatia rufaa,” amesema Wakili Kahigi.
Awali, Kyenkungu alihukumiwa na Mahakama ya Kisutu, adhabu ya kifungo cha nje akifanya kazi za kijamii kwa miezi 18, Juni 30, 2023, baada ya kumtia hatiani katika kesi ya jinai iliyokuwa inamkabili, kwa makosa manne ya kughushi nyaraka za Mikocheni Shopping Mall Ltd na kujipatia mkopo wa Sh350 milioni.
Alikata rufaa Mahakama Kuu akipinga kutiwa hatiani pamoja na adhabu aliyopewa, akiwasilisha sababu sita, pamoja na mambo mengine akidai kuwa Mahakama ilikosea kumtia hatiani bila upande wa mashtaka kuthibitisha mashtaka dhidi yake.
Pia alidai kwamba ilikosea kuzingatia ushahidi wa shahidi wa kwanza, shahidi mtaalamu ambao haukuungwa mkono, pamoja na vielelezo vya upande wa mashtaka yaani hati za Mikocheni Shopping Mall, ambazo hazikuwa sehemu ya nyaraka zilizodaiwa kughushiwa.
Ofisi ya DPP nayo iikata rufaa ikiwasilisha sababu moja tu kuwa Mahakama ya chini ilikosea kumhukumu adhabu ya kutumikia kazi za kijamii kinyume cha sheria.
Wakati wa usikilizwaji wa rufaa hiyo, mrufani Kyenkungu aliwakilishwa na wakili Kahigi na DPP aliwakilishwa na mawakili wa Serikali Clement Masua na Tumaini Mafuru.
Katika hukumu hiyo Jaji Mwakapeje ametupilia mbali rufaa ya Kyenkungu, baada ya kukubaliana na Mahakama ya Kisutu kumtia hatiani.
Pia imekubaliana na rufaa ya DPP na kutengua adhabu ya kufanya kazi za kijamii, ikisema kuwa matakwa ya kifungu cha 339A cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, hayakuzingatiwa na mahakama ya chini ilipomuadhibu kutumikia kazi za kijamii kwa miezi 18.
"Ninaibadilisha kuwa kifungo cha miaka mitatu jela kuanzia tarehe ya kutiwa hatiani. Vivyo hivyo nakubaliana na kutiwa hatiani na kufutilia mbali rufaa ya John Alfred Kyenkungu."
Katika kesi ya msingi jinai namba 51/2021, Kyenkungu alikuwa anakabiliwa na mashtaka manne ya kughushi nyaraka mbalimbali na kujipatia mkopo wa Sh350 milioni kutoka benki ya Equity.
Kwa mujibu wa upande wa mashtaka, tarehe isiyofahamika mwaka 2014 jijini Dar es Salaam, Kyenkungu alighushi hati ya haki ya umiliki wa kiwanja cha Mikocheni Shopping Mall.
Alidaiwa pia kughushi hati hiyo kwa kutumia jina na sahihi ya Said Nassoro ambaye alikuwa mkurugenzi mwenza katika kampuni ya Mikocheni Shopping Mall Ltd kuonyesha kuwa kwa pamoja wameridhia kuchukua mkopo.
Pia alidaiwa kughushi muhtasari wa kikao cha bodi ya wakurugenzi wa kampuni hiyo kilichofanyika cha Julai 18, 2014 kwa kuweka jina na sahihi ya Nassoro na fomu ya hati ya kiwanja namba 40 iliyoonyesha kusainiwa na Said Nassoro.
Vilevile tarehe isiyojulikana mwaka 2018, alighushi nyaraka inayoonyesha dhamana ya kampuni na kutumia jina la Said Nassoro kuonyesha kuwa amekubaliana kuweka rehani kampuni ya Jamaa Fast food Limited kama sehemu ya ulinzi wa mkopo huo wa Sh350 milioni.